Remove ads
nchi huru katika Ulaya Mashariki na Asia ya Kaskazini From Wikipedia, the free encyclopedia
Urusi (kwa Kirusi: Россия, Rossiya) ni nchi ya Ulaya ya Mashariki na ya Asia.
| |||||
Kaulimbiu ya taifa: none | |||||
Wimbo wa taifa: Hymn of the Russian Federation | |||||
Mji mkuu | Moscow | ||||
Mji mkubwa nchini | Moscow | ||||
Lugha rasmi | Kirusi | ||||
Serikali | Jamhuri, Shirikisho serikali ya kiraisi Vladimir Putin Mikhail Mishustin | ||||
Uhuru {{{established_events}}} |
{{{established_dates}}} | ||||
Eneo - Jumla - Maji (%) |
17,075,400 km² (ya 1) 13 | ||||
Idadi ya watu - 1-1-2021 kadirio - 2002 sensa - Msongamano wa watu |
146,238,000 (ya 9) 145,164,000 8.3/km² (ya 217) | ||||
Fedha | Rubl (RUB ) | ||||
Saa za eneo - Kiangazi (DST) |
(UTC+2 to +12) (UTC+3 to +13) | ||||
Intaneti TLD | .ru, (.su reserved) | ||||
Kodi ya simu | +7
- | ||||
1 Rank based on Aprili 2006 IMF data |
Kwa eneo ni nchi kubwa kuliko zote duniani, ikiwa na km² 17,075,400.
Urusi imepakana na Norway, Ufini, Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Belarus, Ukraine, Georgia, Azerbaijan, Kazakhstan, China, Mongolia na Korea ya Kaskazini.
Iko karibu vilevile na maeneo ya Marekani (jimbo la Alaska liko ng'ambo ya mlango wa Bering) na Japani (kisiwa cha Hokkaido kiko ng'ambo ya mlango wa La Pérouse.
Kuna wakazi 146,238,000[1].
Hadi mwaka 1991 Urusi ilikuwa kiini cha Umoja wa Kisovyeti na kuitwa Shirikisho la Jamhuri ya Kisovyiet ya Kijamii ya Kirusi.
Urusi ilikuwa udikteta chini ya chama cha kikomunisti. Tangu 1990 imekuwa demokrasia.
Muundo wa utawala ni shirikisho la jamhuri chini ya rais mtendaji.
Eneo la Shirikisho la Kirusi linajumlisha sehemu kubwa ya kaskazini ya mabara ya Ulaya na Asia. Umbali kati ya upande wa magharibi na upande wa mashariki kabisa ni karibu kilomita 8,000.
Mkoa wa Kaliningrad haufuatani moja kwa moja na maeneo mengine ya Urusi: umetengwa nayo kijiografia na Lithuania.
Mara nyingi Urusi hutazamwa kama sehemu mbili: Urusi wa Ulaya hadi milima ya Ural na Siberia au Urusi wa Kiasia ambayo ni nchi pana kati ya Ural na Pasifiki.
Sehemu kubwa ya Urusi ni tambarare yenye vilima vidogo tu. Milima mirefu inapatikana kusini na mashariki mwa Siberia.
Bahari mpakani urusi - Bahari Nyeusi, Bahari ya Azov, Bahari Nyeupe, Bahari ya Barents, Bahari ya Kara, Bahari ya Laptev, Bahari ya Mashariki ya Siberia, Bahari ya Chukchi, Bahari ya Bering, Bahari ya Ohotsk na Bahari ya Japani.
Jumla Urusi ina pwani ndefu sana zenye urefu wa kilomita 37,000 kwenye Bahari Aktiki na Pasifiki, pia kwenye Bahari Baltiki, Bahari Nyeusi na Bahari ya Kaspi.[2]
Visiwa vikubwa vya Urusi ni Novaya Zemlya na Kisiwa cha Wrangel kwenye Bahari Aktiki na Sakhalin kwenye Pasifiki. Funguvisiwa muhimu ni Funguvisiwa ya Franz Josef, Severnaya Zemlya, Visiwa vya Siberia Mpya katika Bahari aktiki, halafu Kurili katika Pasifiki.
Eneo kubwa la Urusi hugawiwa kwa macho ya ekolojia kwa kanda asilia tano:
Maeneo makubwa ni uwanda, hasa uwanda wa Ulaya ya Mashariki na uwanda wa Siberia ya Magharibi, halafu nyanda za chini za Siberia Kaskazini na Kolyma. Nyanda za juu za Siberia ya Kati na Lena halafu safu za milima kwenye kaskazini-mashariki na kwenye mpaka wa kusini.
Sehemu kubwa za Urusi huwa na vipindi vya majira tofauti sana; joto kubwa inafuatana na baridi kali.
Tabianchi ya Urusi ni hasa ya kibara, kutokana na umbo la nchi na umbali wa sehemu nyingi na bahari. Maeneo mengi yana umbali wa kilomita 400 na zaidi kutoka ufukoni, na kitovu cha nchi kina umbali wa kilomita 3,840 kutoka bahari.
Zaidi ya hayo Urusi ina safu za milima mirefu hasa upande wa kusini na upande wa mashariki ambazo zinazuia kufika kwa urahisi kutoka Bahari Hindi na Pasifiki upepo wenye uwezo wa kupoza halijoto. Kinyume chake upepo kutoka Bahari Aktiki unaweza kuingia bila vizuizi vya aina hii na kuleta baridi kali.
Theluji hufunika uso wa ardhi kati ya siku 40 hadi 200 kwa mwaka katika Urusi ya magharibi, na siku 120 - 200 kila mwaka katika Siberia. Katika kaskazini karibu na Aktiki iko ardhi yenye hali ya jalidi ya kudumu kwa kina cha mita mia kadhaa. Halijoto ya wastani ya sehemu kubwa ya Siberia iko chini ya 0°C.
Sehemu kubwa za Urusi zina majira mawili tu ambayo ni majirajoto na majirabaridi yenye jalidi. Vipindi vya kati ni vifupi sana. Hii inaathiri pia njia za usafiri. Wakati wa majirabaridi, ambako maji yote kwenye mito na maziwa huwa yameganda, barabara zinafunguliwa juu ya barafu ya mito mikubwa au kupitia maziwa makubwa.
Kanda nyembamba la pwani kwenye Bahari Nyeusi huwa na tabianchi ya nusutropiki.
Wakati wa Januari halijoto ni −6°C huko Saint Petersburg, −27°C katika Siberia ya magharibi na −43°C huko Yakutsk katika Siberia ya Kati. Wakati wa majirajoto halijoto inapatikana kati ya wastani ya 4°C kwenye visiwa vya aktiki na wastani ya 20°C katika kusini.
Halijoto ya chini iliyopimwa ilikuwa −68°C huko Siberia ya kaskazini na +45°C kusini mwa nchi.
Ukali wa baridi una athari kubwa juu ya maisha yote, jinsi gani watu wanaweza kufanya kazi, na kama kilimo kinawezekana au la. Majengo yanapaswa kuwa na tabia za pekee hasa katika maeneo ya jalidi ya kudumu ambako ni lazima kuweka kila jengo juu ya nguzo zinazofikia kina cha jalidi kwa sababu uso wa ardhi unakuwa laini na matope wakati wa joto; mashine zinapaswa kutengenezwa kwa kutumia feleji inayovumilia tofauti kubwa za jalidi na joto.
Miezi ya jalidi ni pia kipindi cha giza, kwa hiyo kuna mahitaji ya pekee ya nishati na nguo.
Usimbishaji katika sehemu nyingi za Urusi si mkubwa kwa sababu maeneo mengi yako mbali na pwani, hivyo hayapokei hewa yenye unyevunyevu kutoka bahari.
Sehemu zinazopokea mvua nyingi ziko karibu na pwani, kama Sochi kwenye Bahari Nyeusi (mm 1500 kwa mwaka) na visiwa vya Kurili (mm 1000 - 1500, hasa theluji). Pwani ya Baltiki inapokea mm 600, Moscow mm 525 kwa mwaka. Maeneo yaliyo karibu na Kazakhstan hupokea mm 20 pekee kwa mwaka, na kwenye sehemu za pwani za Aktiki ni mm 15 pekee.
Kwa jumla kuna mito elfu kadhaa. Mingi iko sehemu ya beseni ya utiririshaji ya Bahari Aktiki ambako kuna watu wachache. Kwa hiyo sehemu kubwa ya maji haina matumizi kwa manufaa ya binadamu. Kinyume chake maeneo ya Urusi ya kusini kwenye vipindi vya joto na wakazi wengi yanaona vipindi vya uhaba wa maji kama vile beseni za mto Don na mto Kuban.
Upande wa mashariki wa Ural kuna mito 40 yenye urefu unaozidi kilomita 1,000. Ni hasa mito 3 inayobeba maji ya Siberia kwenda Bahari Aktiki:
Mito hii mitatu humwaga kila sekunde m³ 50,000 kwenye Bahari Aktiki.
Kati ya mito mingine mikubwa kuna:
Maziwa ya Urusi hushika takriban robo ya maji matamu yote duniani yasiyo barafu. [3]
Ziwa kubwa ni Ziwa Baikal ambayo ni ziwa yenye maji mengi duniani.[4] Maziwa mengine ni pamoja na Ladoga na Onega ambayo ni kati ya maziwa makubwa zaidi ya Ulaya.
Majiji mawili makuu ni Moscow na Sankt Peterburg.
Moscow ni mji mkuu wa kale uliyorudishiwa nafasi yake baada ya mapinduzi ya kikomunisti ya mwaka 1918.
Sankt Peterburg ilikuwa mji mkuu kuanzia mwaka 1703 hadi 1918 kama makao makuu ya tsar au kaisari wa Urusi. Miaka 1924-1989 ikaitwa Leningrad kwa heshima ya Lenin, kiongozi wa mapinduzi.
Miji mingine mikubwa ni pamoja na:
Historia ya Urusi kama nchi ya pekee ilianza polepole pale ambako makabila ya wasemaji wa Kislavoni cha Mashariki walipoanza kujenga maeneo yao kuanzia karne ya 8 BK.
Waskandinavia waliunda dola la kwanza katika eneo la Kiev, wakalitawala kama dola la Kislavoni. Wenyewe waliingia haraka katika lugha na utamaduni wa wenyeji, lakini waliacha jina lao kwa sababu "Rus" kiasili ilikuwa jina la Waskandinavia wale kutoka Uswidi ya leo.
Mwaka 988 Kiev ilipokea Ukristo wa Kiorthodoksi kutoka Bizanti. Tukio hilo liliathiri moja kwa moja utamaduni na historia yote iliyofuata.
Dola la Kiev liliporomoka kutokana na mashambulio ya Wamongolia baada ya Jingis Khan, na maeneo madogo zaidi yalijitokeza yaliyopaswa kukubali ubwana wa Wamongolia.
Kubwa kati ya maeneo yale madogo ulikuwa utemi wa Moscow. Watemi wa Moscow walichukua nafasi ya kwanza kuunganisha Waslavoni wa Mashariki dhidi ya Wamongolia na kupanua utawala wao.
Baada ya anguko la Konstantinopoli mwaka 1453 watawala wa Moscow walipokea cheo cha Kaisari wa Roma kilichoitwa "tsar" na kuwa cheo cha watawala wa Urusi hadi mwaka 1917.
Mpaka karne ya 18 eneo la Moscow lilikuwa tayari kubwa likabadilika kuwa Milki ya Kirusi iliyoendelea kupanuka katika Siberia na Asia ya Kati, ikawa kati ya milki kubwa kabisa za historia ikienea kutoka Poland upande wa magharibi hadi bahari ya Pasifiki upande wa mashariki.
Tsar Petro I (1689 - 1725) alitambua ya kwamba nchi yake ilikuwa nyuma upande wa teknolojia na elimu kulingana na mataifa ya Ulaya. Alianzisha mabadiliko mengi ya kuiga mfano wa Ulaya ya Magharibi akahamisha mji mkuu kutoka Moscow kwenda mji mpya aliounda sehemu ya magharibi ya milki yake akauita Sankt Peterburg.
Tangu wakati wa Petro I nchi ilishiriki katika siasa ya Ulaya pamoja na vita vingi vya huko.
Mwanzo wa karne ya 19 milki ikashambuliwa na Napoleon Bonaparte aliyeteka Moscow lakini Warusi walifaulu kuwafukuza maadui kwa msaada wa baridi iliyoua askari wengi wa Ufaransa.
Matsar wa Urusi waliendelea kutawala kwa kuwa na mamlaka zote bila kushirikisha wananchi jinsi ilivyokuwa kawaida katika sehemu nyingine za Ulaya. Miji iliona maendeleo ya viwanda na jamii ya kisasa, lakini sehemu kubwa ya wakulima waliendelea kukaa chini ya utawala wa makabaila.
Katika sehemu ya pili ya karne ya 19 Urusi ulipanua utawala wake juu ya maneo makubwa ya Asia ya Kati na milima Kaukasus ukashindana na Milki ya Osmani, Uajemi na athira ya Uingereza katika Asia.
Mwanzoni mwa karne ya 20 Urusi ukaonekana tena kuwa nyuma ya nchi za magharibi na sababu kuu ilikuwa nafasi kubwa ya serikali iliyojitahidi kusimamia mabadiliko yote katika jamii na kuzuia mabadiliko yaliyoonekana magumu machoni pa Tsar, pa makabaila na pa maaskofu wa Kanisa la Kiorthodoksi.
Mwaka 1904 upanuzi wa Urusi katika Asia uligongana na upanuzi wa Japan. Katika vita dhidi ya Japani Urusi ulishindwa na tukio hili lilisababisha mapinduzi ya Urusi ya 1905. Tsar Nikolas alipaswa kukubali uchaguzi wa bunge la duma kwa mara ya kwanza. Hata hivyo haki za duma zilikuwa chache na mabadiliko yalitokea polepole mno.
Urusi ulijiunga mwaka 1914 na vita kuu ya kwanza ya dunia ukisimama upande wa Uingereza na Ufaransa dhidi ya Ujerumani na Austria-Hungaria. Vita havikuenda vizuri, wananchi wakaona njaa na mapinduzi ya Februari 1917 yakamfukuza Tsar aliyejiuzulu.
Vita vikaendelea na Wajerumani walizidi kusogea mbele. Serikali mpya ya bunge ikapinduliwa katika mwezi wa Oktoba 1917 na mapinduzi ya Bolsheviki chini ya kiongozi wao Vladimir Ilyich Lenin.
Huo ulikuwa mwanzo wa vita ya wenyewe kwa wenyewe. Wakomunisti chini ya Lenin walishinda na kugeuza Urusi kuwa Umoja wa Kisoveti tangu mwaka 1922, wakitawala kwa mfumo wa kiimla wa chama chao. Ili kurahisisha utawala wao Wakomunisti waliamua kutawala Urusi wa awali kwa muundo wa shirikisho, wakaunda jamhuri mbalimbali kufuatana na mataifa ndani ya eneo hilo kubwa.
Urusi lilikuwa sasa jina la jamhuri kubwa katika umoja huu nao ukaitwa Shirikisho la Jamhuri ya Kisovyiet ya Kijamii ya Kirusi.
Kikatiba jamhuri hizo zote zilikuwa nchi huru lakini hali halisi zilitawaliwa zote kutoka makao makuu ya chama cha kikomunisti huko Moscow. Katiba hiyo ilipata umuhimu tangu 1989, wakati wa mwisho wa utawala wa Wakomunisti ambako jamhuri zote zilitafuta uhuru wao zikaachana na Umoja.
Mji mkuu Sant Peterburg ulibadilishwa jina kuwa Leningrad na baadaye makao makuu ya nchi yakahamishwa tena kwenda Moscow.
Kiongozi aliyemfuata Lenin mwaka 1924 alikuwa Josef Stalin aliyeweza kugeuza utawala wa chama kuwa utawala wake mwenyewe akiongoza kwa jina la Katibu Mkuu wa chama cha kikomunisti.
Mwaka 1939, mwanzoni mwa vita kuu ya pili ya dunia Stalin alipatana na Ujerumani wa Adolf Hitler kugawa maeneo ya Poland na nchi za Baltiki kati yao lakini mwaka 1941 Hitler alishambulia pia Umoja wa Kisovyeti.
Warusi walipoteza askari milioni kadhaa, lakini waliweza kuwazuia Wajerumani wasiteke Moscow na Leningrad. Kwa msaada wa Marekani Warusi waliweza kurudisha jeshi la Ujerumani na kusogea magharibi. Umoja wa Kisovyeti ukawa kati ya nchi washindi wa vita kuu ya pili ya dunia.
Tangu mwaka 1945 jeshi la Urusi lilikaa katika nchi zote za Ulaya ya Mashariki hadi katikati ya Ulaya. Katika nchi hizo zote serikali za kikomunisti zilianzishwa na kusimamiwa na ofisi kuu ya chama cha kikomunisti huko Moscow.
Urusi ulikuwa kiongozi wa nchi za kijamaa, ukishindana katika vita baridi dhidi ya nchi za magharibi zilizoongozwa na Marekani. Athira ya Umoja wa Kisovyeti ilipanuka hadi Afrika, Asia na Amerika ya Kati ambako nchi mbalimbali zilianza kuiga mtindo wa kikomunisti.
Utawala wa kikomunisti uliendelea hadi mwaka 1990. Mwishoni matatizo ya uchumi yalizidi kwa sababu mfumo wa uchumi ulioongozwa moja kwa moja na serikali kuu, pamoja na utaratibu wa kiimla uliozuia wananchi kupinga siasa ya viongozi na kuleta hoja tofauti, ulisababisha tena nchi kubaki nyuma.
Tangu mwaka 1990 jamhuri kadhaa za Umoja wa Kisovyeti ziliondoka katika umoja na kutangaza uhuru wao ilhali serikali ilishindwa nguvu ya kuwazuia. Mwaka 1991 jamhuri wanachama za mwisho Urusi, Belarus na Ukraine ziliamua kumaliza Umoja wa Kisovyeti.
Tangu mwaka 1991 Urusi ulipungukiwa na maeneo mengi yaliyotwaliwa katika karne ya 19 na ya 18, ukabaki peke yake ingawa bado ni dola kubwa kuliko yote duniani.
Marais wa Urusi baada ya 1991 walikuwa Boris Yeltsin na Vladimir Putin.
Dmitry Medvedev alichaguliwa kuwa rais wa Urusi mwaka 2008 na mtangulizi wake Vladimir Putin akawa waziri mkuu. Mwaka 2012 Putin aliruhusiwa tena kikatiba kugombea uraisi akachaguliwa na kurudishwa tena mwaka 2018.
Kulingana na katiba ya nchi, Urusi ni shirikisho na jamhuri ambako rais ni mkuu wa nchi [5]na waziri mkuu ni kiongozi wa serikali.
Shirikisho la Urusi linafuata muundo wa demokrasia yenye mfumo wa vyama vingi. Kuna serikali ya kiraisi yenye mikono mitatu:
Rais huchaguliwa kwa kura ya wananchi wote kwa kipindi cha miaka sita akiweza kurudishwa mara moja madarakani; anaweza kugombea tena baada ya kupumzika angalau kipindi kimoja. [6]
Baraza la mawaziri lina waziri mkuu na mawaziri wake wanaoteuliwa na rais kulingana na pendekezo ka waziri mkuu. Waziri mkuu anahitaji kukubaliwa na duma.
Vyama vya kisiasa muhimu ni Urusi wa Umoja, Chama cha Kikomunisti cha Urusi, Chama Huria cha Urusi na Urusi wa Haki.
Kuna Maeneo ya Shirikisho la Urusi 85.
Kulingana na katiba ya nchi kuna maeneo 85 yanayofanya shirikisho lake [7] pamoja na eneo la Krim na mji wa Sevastopol.[8]
Maeneo ya shirikisho yanawakilishwa sawa katika bunge na kila moja linapewa wawakilishi wawili. [9] Lakini hali halisi yana viwango tofauti vya madaraka ya kujitawala katika siasa ya ndani.
Maeneo yote ya Shirikisho yamepangwa katika kanda 9. Kila moja huwa na Mkuu wa Kanda anayeteuliwa na rais na jukumu lake ni kusimamia na kuangalia kazi ya serikali za maeneo.
Warusi asilia ni 81%, lakini kuna makabila mengine 160 katika shirikisho, ambayo yanatumia lugha 100 hivi[11] (angalia orodha ya lugha za Urusi).
Kufuatana na sensa ya mwaka 2002 kulikuwa na watu milioni 142.6 wasemaji wa Kirusi, wakifuatwa na wasemaji wa Kitatari milioni 5.3 na Kiukraina milioni 1.8.[12]
Lugha rasmi na ya kawaida ni Kirusi kwenye maeneo yote ya Shirikisho la Kirusi lakini katiba ya nchi inatoa kibali kwa Jamhuri za shirikisho kujiamulia lugha rasmi ya nyongeza kwa eneo lao pamoja na Kirusi.[13]. Kuna pia "maeneo huru" ya pekee yenye lugha zao pamoja na Kirusi.
Warusi wengi kabisa walikuwa wafuasi wa Ukristo wa Kiorthodoksi hadi mapinduzi ya 1917/18. Katika mapokeo yao wenyewe ni Mtume Andrea aliyeleta mara ya kwanza imani hiyo hadi Urusi.[14].
Chanzo cha mapokeo hayo yalitokeo kwenye eneo la Ukraine ya leo ambako mnamo mwaka 988 mtemi wa Kiev Vladimir Mkuu alipokea ubatizo kutoka kwa mapadre wa Kanisa la Bizanti uliofuatwa na ubatizo wa familia na wananchi wa Kiev[15].
Kanisa la Kiorthodoksi liliendelea kuwa dini rasmi katika milki za Kirusi hadi mapinduzi ya 1917. Wakomunisti walioshika utawala mwaka ule walikataa dini zote [16] Urusi pamoja na Umoja wa Kisovyeti ilikuwa nchi ya kwanza iliyoamua kufuata uatheisti kama itikadi kuu[17] [18][19] Serikali ya kikomunisti ilinyang'anya mali na majengo ya Kanisa, magazeti yake yalishambulia mafundisho ya dini, uatheisti ukafundishwa shuleni na waumini wakahangaishwa.[20] Makanisa mengi yaligeuzwa kwa matumizi ya ghala, ukumbi wa michezo na kadhalika au kubomolewa.
Mapadre, maaskofu na maimamu mara nyingi walikamatwa, kutupwa gerezani au kutumwa kwenye makambi ya GULAG. Kati ya miaka 1922 hadi 1926 jumla ya maaskofu 28 na mapadre zaidi ya 1,200 waliuawa. Wengi sana zaidi walidhulumiwa.[21]
Dini za awali ziliendelea chini ya ukomunisti lakini kwa matatizo makubwa. Waumini waliweza kusali kwao nyumbani na katika makanisa na misikiti michache iliyobaki. Wakati wa Vita Kuu ya Pili mateso yalipungua kidogo kwa sababu Joseph Stalin alitaka kuwaunganisha wananchi wote chini ya uongozi wake katika juhudi za vita.
Baada ya ukomunisti kuanguka mnamo 1990 jumuiya za kidini zimepata uhai mpya. Wafuasi wa dini hawahesabiwi katika sensa, hivyo kuna makadirio tu. Mnamo Agosti 2012 kulikuwa na kadirio la asilimia 46.8 za Warusi kuwa Wakristo [22] na asilimia 25 waliamini uwepo wa Mungu lakini bila kufuata dini yoyote. Makadirio mengine yalitaja asilimia 76 za Warusi kuwa Wakristo [23] au asilimia 65 [24].
Upande wa Wakristo, wengi wanakadiriwa kuwa Waorthodoksi (kati ya hao wengi hawashiriki kwenye ibada za mara kwa mara) na wachache ni Wakatoliki na Waprotestanti.[25]
Uislamu ni dini yenye wafuasi wengi baada ya Kanisa la Kiorthodoksi.[26] Ni dini kuu kati ya watu wengi wa Kaukazi kama vile Wachecheni, Waingushi na Wacherkesi, pia kati ya wasemaji wengi wa Lugha za Kiturki kama vile Watatari na Wabashkiri. Kwa jumla kuna kadirio la kuwepo kwa Waislamu milioni 9.4 ambao ni sawa na asilimia 6.5% ya wananchi wote. Walio wengi ni Wasunni, pamoja na wafuasi wachache wa Shia na Ahmadiya. Sehemu kubwa wanajihesabu kuwa Waislamu bila madhehebu.[27] [22][28]
Katika maeneo matatu kuna wafuasi wa Ubuddha ambayo ni Buryatia, Tuva na Kalmykia.
Dini za jadi hufuatwa bado katika sehemu za Siberia na Mashariki ya Mbali kama vile Yakutia na Chukotka.
Kwa jumla Waslavi mara nyingi ni Wakristo wa Kiorthodoksi, wasemaji wa lugha za Kiturki ni zaidi Waislamu, na wenye lugha za Kimongolia mara nyingi hufuata Ubuddha.[29]
Kuhusu watu wasio na dini kuna makadirio kuwa kati ya 16% na 48% ya wananchi wote.[30]
Idadi ya watu wanaojihesabu kuwa Waatheisti ni asilimia 7 na idadi yao imeendelea kupungua. [31]
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.