Marekani

nchi katika Amerika Kaskazini From Wikipedia, the free encyclopedia

Marekani

Marekani (Kiingereza: America au United States, kifupi: US), kirasmi Muungano wa Madola ya Amerika (Kiingereza: United States of America, kifupi: USA) ni nchi iliyomo Amerika Kaskazini, na inapakana na Kanada upande wa kaskazini na Meksiko upande wa kusini. Inajumuisha majimbo 50, wilaya ya shirikisho, na maeneo ya nje. California na Texas ndiyo majimbo yaliyokuwa na watu wengi zaidi. Marekani ina takriban watu milioni 340 na kuwa nchi ya tatu duniani kuwa na watu wengi sana. Aidha, ni nchi ya tatu kwa ukubwa duniani, ikiwa na eneo la takriban kilomita za mraba milioni 9.8, ikienea kutoka Bahari ya Atlantiki hadi Bahari ya Pasifiki. Ilianzishwa rasmi mwaka 1776, baada ya majimbo 13 kupata uhuru kutoka Uingereza.

Ukweli wa haraka Muungano wa Madola ya Amerika United States of America (Kiingereza), Mji mkuu ...
Muungano wa Madola ya Amerika
United States of America (Kiingereza)
Kaulimbiu: "In God We Trust"
Wimbo wa taifa: "The Star-Spangled Banner"
Thumb
Mji mkuuWashington, D.C.38°53′N 77°1′W
Mji mkubwaNew York
40°43′N 74°0′W
Lugha rasmiHakuna katika
serikali ya shirikisho
Lugha za taifaKiingereza
SerikaliJamhuri ya shirikisho
  Rais
Donald Trump
  Naibu Rais
JD Vance
Uhuru kutoka Ufalme wa Muungano
  Tangazo
4 Julai 1776
  Muungano
1 Machi 1781
  Kutambuliwa
3 Septemba 1783
  Katiba
21 Juni 1788
Eneo
  Jumlakm2 9 833 520[1] (ya 3)
  Maji (asilimia)7.0[2]
  Ardhikm² 9 147 593[1]
Idadi ya watu
  Kadirio la 2024335 893 238[3]
  Msongamano33.6/km2
PLT (PPP)Kadirio la 2024
  Jumla USD trilioni 29.168[4]
  Kwa kila mtu USD 86 601[4]
PLT (kawaida)Kadirio la 2024
  Jumla USD trilioni 29.168[4]
  Kwa kila mtu USD 86 601[4]
HDI (2022) 0.927[5] - juu sana
Gini (2022) 41.3[1]
SarafuDola ya Marekani
Majira ya saaUTC−4 hadi −12, +10, +11
Upande wa magariKulia
Msimbo wa simu+1
Tovuti rasmi:
https://www.usa.gov
Funga

Mji mkuu wa Marekani ni Washington DC. Los Angeles, New York na Chicago ndio miji mikubwa.

Demografia

Katika makadirio ya mwaka wa 2023, takriban watu milioni 334,914,895 wanaishi nchini humo. Demografia inaonyesha tofauti za kijamii, kikabila, lugha, na dini.

Idadi ya watu

Maelezo zaidi Mwaka, Idadi ya watu ...
MwakaIdadi ya watuKiwango cha ukuaji (%)
2020331,449,2810.35%
2021332,031,5540.58%
2022333,287,5570.38%
2023334,914,8950.49%
2024 (makadirio)340,110,988
Funga

Sababu kuu za ukuaji wa idadi ya watu ni: kuzaliwa kwa watu wapya (zaidi ya vifo) na uhamiaji.

Jamii na makabila

Ofisi ya Sensa ya Marekani inagawanya watu kwa makundi yafuatayo (makadirio ya 2021):

Maelezo zaidi Jamii/kabila, Asilimia ...
Jamii/kabilaAsilimiaMaelezo
Wazungu (Wasio Wahispania)57.8%Wengi; imepungua kutoka 63.7% (2010)
Wahispania au Walatino18.9%Kundi kubwa la wachache; pamoja na Wamexico, Wapuerto Rico, n.k.
Weusi au Waafrika12.1%Wengi huko kusini mwa nchi
Waasia6.0%Kundi linalokua kwa kasi; pamoja na Wachina, Wahindi, Wafilipino
Watu wenye asili mbili au zaidi2.7%Ongezeko kutokana na utambulisho wa jamii mchanganyiko
Wenyeji wa Marekani/Waalaska0.7%Pamoja na makabila ya asili
Wenyeji wa Hawaii/Pasifiki0.2%Wengi huko Hawaii na Pwani ya Magharibi
Funga

Lugha

Kiingereza ndiyo lugha inayotumika zaidi (78.5%), ikifuatiwa na:[6]

  • Kihispania (13.2%)
  • Kichina (1.1%)
  • Kitagalog, Kivietinamu, Kiarabu, Kifaransa, n.k. (7.2% pamoja).

Dini

Sinagogi ya Magen David, New York

Mgawanyo wa kidini (data ya Pew Research 2022):[7]

Maelezo zaidi Dini, Asilimia ...
DiniAsilimia
Ukristo63%
Wasiokuwa na dini29%
Uyahudi2%
Uislamu1%
Uhindu1%
Ubudha1%
Nyingine3%
Funga

Muundo wa Umri

Umri wa kati: miaka 38.5 (2021).

Maelezo zaidi Kikundi cha umri, Asilimia ...
Kikundi cha umriAsilimia
0–14 miaka18.2%
15–64 miaka64.6%
65+ miaka17.2%
Funga

Elimu

  • 91% ya watu wazima (25+) wana stahili ya shule ya upili.
  • 36% wana shahada ya kwanza au juu zaidi.

Kipato na Umaskini

  • Kipato cha kati kwa kaya: $70,784 (2021).[8]
  • Kiwango cha umaskini: 11.6% (2021).[8]

Eneo

Marekani bara

Thumb
Picha kutoka angani ikionyesha majimbo 48 ya Marekani yanayopakana

Eneo la Marekani lina ukubwa wa kilometa mraba 9,826,675 na liko hasa katika bara la Amerika Kaskazini kati ya Kanada upande wa kaskazini na Meksiko upande wa kusini.

Marekani imeunganisha upana wote wa bara kutoka Bahari ya Atlantiki hadi Pasifiki, ikigawanywa kwa majimbo 48 yanayojitawala.

Eneo hilo lagawiwa katikati na mto mkubwa Mississippi unaoanza mpakani kwa Kanada na kuishia katika Ghuba ya Meksiko.

Alaska

Jimbo la Alaska liko pia kwenye bara la Amerika Kaskazini upande wa kaskazini kutoka Kanada kuelekea Urusi, lakini halipakani na jimbo lolote la Marekani.

Hawaii

Funguvisiwa la Hawaii ni jimbo la visiwani katika bahari ya Pasifiki. Ni jimbo la 50 na la mwisho mpaka sasa.

Visiwa vya ng'ambo vya Marekani

Maeneo ya ng'ambo ya Marekani ni visiwa kadhaa ambavyo ni maeneo ya Kimarekani ingawa si sehemu ya jimbo lolote. Zamani yalikuwa kama makoloni hata kama Marekani ilidai kutokuwa na ukoloni. Siku hizi maeneo haya yamepata viwango mbalimbali vya kujitawala. Kwa kawaida maeneo haya huchagua pia wawakilishi kwa ajili ya bunge la Marekani lakini wawakilishi hao si wabunge wa kawaida, bali wana haki ya kusema na kushauri tu bila haki ya kupiga kura.

Visiwa muhimu kati ya hivyo ni kama ifuatavyo:

Milima

angalia: Orodha ya milima ya Marekani

Safu ya milima ya Rocky Mountains inavuka Marekani yote kutoka kaskazini hadi kusini upande wa magharibi.

Mito

angalia: Orodha ya mito ya Marekani

Mto mkubwa wa Marekani ni Mto Mississippi.

Historia

Thumb
Uenezi wa nchi hatua kwa hatua.

Historia ya awali inaanza na kilele cha Enzi ya barafu, watu wa Asia walipoweka kuingia Alaska kupitia nchi kavu. Baada ya hapo watu hao na wajukuu wao hawakuwa tena na uhusiano na wale wa "Dunia ya zamani" (Afrika, Asia na Ulaya) mpaka walipofikiwa na Wazungu kutoka Norway (karne ya 10) na Christopher Columbus mwaka 1492.

Hao wakazi wa kwanza walikuwa wawindaji-wakusanyaji; wakifuata mawindo yao walifika taratibu hadi ncha ya kusini ya Amerika (Tierra del Fuego).

Polepole utamaduni wa baadhi ya makabila, ingawa kwa kuchelewa kuliko Dunia ya zamani, ulifikia hadhi ya ustaarabu, kama vile ule wa Mississippi.

Safari za baharia Christopher Columbus kuanzia mwaka 1492, zilivuta hasa Hispania, Ureno na halafu Uingereza, Ufaransa na Uholanzi kujianzishia makoloni ili kunyonya maliasili nyingi za "Dunia mpya".

Kwa namna hiyo, mazingira ya Amerika yalibadilika kabisa mpaka zikatokea aina mpya za utamaduni na hatimaye mataifa mapya, hasa kutokana na mchanganyiko ya wenyeji (Waindio) na walowezi kutoka Ulaya, halafu pia watumwa kutoka Afrika.

Marekani ilianza kama muunganiko wa makoloni ya Uingereza kwenye pwani ya mashariki ya Amerika ya Kaskazini tangu karne ya 17. Walowezi kutoka Uingereza walijipatia ardhi wakipigana na wenyeji Waindio.

Tangu karne ya 19 wahamiaji walifika pia kutoka Asia, hasa China na Japani.

Katika vita dhidi ya Hispania na Meksiko, Marekani ilipanua eneo lake kwenda kusini.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Marekani ilipigwa kuanzia 1861 hadi 1865 kati ya majimbo ya kusini na majimbo ya kaskazini nchini Marekani. Sababu mojawapo muhimu ya vita ilikuwa suala la utumwa. Majimbo ya kaskazini yaliwahi kupiga utumwa marufuku lakini majimbo ya kusini yaliendelea na sheria zilizoruhusu utumwa na matajiri wengi wa kusini walitegemea kazi ya watumwa hao. Mafarakano yalianza kuhusu swali kama madola mapya yaliyoanzishwa katika Amerika Kaskazini na kujiunga na Muungano yangeruhusiwa kukubali utumwa au la. Mwaka 1861 madola ya kusini-mashariki yalitangaza kujiondoa katika Muungano na kuanzisha "Shirikisho la Madola ya Amerika". Vita vilianza na kudumu miaka minne na watu 650.000 walikufa, lakini mwishoni kaskazini ilishinda. Utumwa ulipigwa marufuku na watumwa walipewa haki za kiraia. Lakini watumwa wengi wa awali waliendelea kuwa maskini na baada ya muda, sheria mpya katika majimbo ya kusini zilinyima haki nyingi za kiraia za Wamarekani weusi waliopaswa kuishi chini mfumo wa ubaguzi wa rangi.

Thumb
Noti ya Dola 100.

Katika miongo iliyofuata, Marekani ilitwaa maeneo yaliyowahi kubaki chini ya mamlaka ya Waindio na kuyafanya maeneo yake. Katika Vita vya Marekani dhidi ya Hispania kwenye mwaka 1898 ilijipatia utawala juu ya Ufilipino na Puerto Rico, makoloni ya awali ya Hispania, na kuwa yenyewe nchi iliyotawala makoloni.

Wahamiaji kwa mamilioni waliendelea kufika hasa kutoka Ulaya. Kabla ya mwaka 1880 idadi kubwa walitoka Ujerumani, Eire, Uingereza na Uskoti, pamoja na Wachina waliotafuta kazi hasa Kalifornia. Baada ya mwaka 1880 hadi Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1914-1918) wengi walifika kutoka Ulaya ya Kusini na ya Mashariki, hasa Waitalia, Wayahudi kutoka Milki ya Urusi, Wapolandi na wenyeji wa nchi nyingine za Kislavi. Wahamiaji hao walileta pia tamaduni zao na kukubali mishahara midogo kuliko wenyeji waliowahi kufika mapema; hali hiyo ilileta mara kadhaa sheria zilizolenga kuweka mipaka; sheria ya mwaka 1882 ilikataa kufika kwa Wachina, sheria ya mwaka 1922 ililenga kupunguza idadi ya Waitalia, Wayahudi na watu wa Ulaya ya Mashariki kwa kutaja mipaka kwa kila nchi ya asili[9].

Katika siasa ya nje, Marekani iliwahi kutangaza tangu mwaka 1823 kwamba ilitazama Amerika yote kama eneo ambalo haikubali kuingiliwa na nchi za Ulaya; wakati ule makoloni mengi ya Amerika ya Kusini yalikuwa yakifaulu kupata uhuru kutoka Hispania, na Marekani ilitaka kusisitiza isingekubali kuingia kwa mataifa mengine ya Ulaya.

Katika miongo iliyofuata uchumi wa Marekani uliimarika pamoja na kukua kwa sekta ya viwanda na wafanyabiashara wa Marekani walipanua biashara yao kimataifa; mnamo 1854 manowari za Marekani ziliilazimisha Japani kukubali kufunguliwa kwa ubalozi na kupokea wafanyabiashara. Meli za wafanyabiashara wa Marekani zilifika kote duniani, tangu miaka ya 1830 hadi Zanzibar ambako ubalozi mdogo ulifunguliwa mwaka 1837[10]. Wakati wa vita dhidi ya Hispania Marekani ilihakikisha pia nafasi yake katika biashara ya China dhidi ya mipango ya mataifa ya Ulaya ya kuigawa nchi hiyo.

Mwaka 1917 Marekani iliingia katika Vita Vikuu vya Kwanza upande wa Uingereza na Ufaransa; baada ya vita rais Woodrow Wilson alishawishi mataifa mengine kuanzisha Shirikisho la Mataifa lakini bunge lilizuia kuingia kwa Marekani katika umoja huo.

Mdororo Mkuu wa mwaka 1929 ulileta matatizo makubwa kwa uchumi na hata njaa kwa raia wengi lakini ulileta pia siasa mpya ya "New Deal" chini ya rais Franklin D. Roosevelt ambako kwa mara ya kwanza programu za kisiasa zilitumia mapato ya serikali kwa shabaha ya kusaidia idadi kubwa ya wananchi waliokuwa bila kazi, bila nyumba na bila kipato; vijana kwa mamilioni waliajiriwa na serikali kwa kazi ya kujenga miundombinu (barabara, mifereji) na kuboresha hifadhi za taifa.

Mwaka 1941 Marekani iliingia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia baada ya kushambuliwa na Japani na kupokea tangazo la vita kutoka Ujerumani. Uwezo wa kiuchumi wa Marekani ulileta ushindi wa mataifa ya ushirikiano. Uwezo wake wa kisayansi ulipanuliwa na wanasayansi kama Albert Einstein waliopaswa kukimbia udikteta wa Adolf Hitler katika Ujerumani na kuiwezesha kutengeneza mabomu ya kwanza ya nyuklia yaliyotumika mnamo Agosti 1945 kuteketeza Hiroshima na Nagasaki.

Katika miongo ya vita baridi iliyofuata, Marekani ilikuwa taifa la kuongoza nchi zenye demokrasia na pia zile ambazo zilisimama upande wa ubepari tu bila demokrasia dhidi ya nchi za kikomunisti zilizoongozwa na Umoja wa Kisovyeti.

Mwanzo wa miaka ya 1960 ilishindana na Umoja wa Kisovyeti katika mbio wa kuingia katika anga-nje ikafaulu kupeleka watu wa kwanza hadi Mwezi mnamo Agosti 1969. Kutokana na ushindani na nchi za ukomunisti Marekani iliingia katika Vita ya Vietnam hadi kushindwa mwaka 1975.

Vilevile miaka ya 1960 ilikuwa kipindi cha mapambano kwa ajili ya haki za Wamarekani weusi, wajukuu wa watumwa wa awali hasa kusini mwa Marekani. Sheria zilizotenganisha watu pamoja na matumizi ya shule, vyuo, majengo na taasisi za burudani kulingana na rangi ya ngozi, zilizozuia ndoa kati ya watu wa rangi tofauti na kuzuia watu maskini wasitumie haki za kiraia zilipigwa marufuku bila kuondoa tofauti katika uwezo wa kiuchumi kati ya makundi katika jamii.

Mapinduzi ya kiteknolojia ya kompyuta na intaneti yalienea Marekani haraka kushinda sehemu nyingine za Dunia.

Watu maarufu

Tazama pia

Marejeo

Viungo vya nje

Wikiwand - on

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.