nchi katika Afrika Magharibi From Wikipedia, the free encyclopedia
Ghana, kirasmi Jamhuri ya Ghana, ni nchi ya Afrika Magharibi inayopakana na Kodivaa upande wa magharibi, Burkina Faso upande wa kaskazini, Togo upande wa mashariki, na Ghuba ya Guinea upande wa kusini.
Jamhuri ya Ghana | |
---|---|
Kaulimbiu ya taifa: Freedom and Justice (Kiingereza) "Uhuru na Haki" | |
Wimbo wa taifa: God Bless Our Homeland Ghana "Mungu Ibariki Nchi Yetu Ghana" | |
Mahali pa Ghana | |
Ramani ya Ghana | |
Mji mkuu na mkubwa nchini | Accra |
Lugha rasmi | Kiingereza |
Eneo | |
• Eneo la jumla | km2 238 533[1] |
Idadi ya watu | |
• Kadirio la 2023 | 33 846 114[1] |
Kabla ya ukoloni Ghana ilikaliwa na idadi ya watu wa kale, hasa wa Falme za Akan, wakiwemo Waakwamu upande wa mashariki, Ufalme wa Ashanti ya bara na falme kadha wa kadha za Kifante, pia falme zisizo za Kiakan kama Waga na Waewe waliokuwa pwani na bara.
Biashara na nchi za Ulaya ilistawi baada ya kukutana kwao na Wareno katika karne ya 15, na Waingereza walianzisha nchi ya Gold Coast, chini ya himaya ya Uingereza mwaka wa 1874.[2]
Nchi ya Gold Coast ilijinyakulia uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka wa 1957, ikawa taifa la kwanza la Afrika Kusini mwa Sahara kufanya hivyo[3][4][5]
Ghana ni mwanachama wa mashirika mbalimbali ya kimataifa yakiwemo Jumuiya ya Madola, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, Umoja wa Afrika, na Umoja wa Mataifa.
Ghana ni nchi ya pili baina ya nchi zinazozalisha mmea wa kakao ulimwenguni kote, pia ni kiambo cha Ziwa Volta, ambalo ndilo ziwa kubwa zaidi ulimwenguni kuundwa na binadamu[6].
Vilevile, Ghana ni nchi inayojulikana sana katika ulimwengu wa soka. Tarehe 16 Oktoba 2009, Ghana lilikuwa taifa la kwanza la Kiafrika kushinda Kombe la Dunia la FIFA kwa walio chini ya umri wa miaka 20 (FIFA U-20 World Cup) kwa kushinda nchi ya Brazil kwa mabao 4 kwa 3 kupitia mikwaju ya penalti[7].
Neno Ghana lina maana ya "Shujaa Mfalme",[8] na lilikuwa jina la heshima walilopewa wafalme wa Himaya ya Ghana nyakati za kale za Afrika Magharibi.[9]. Limekuwa chimbuko la jina “Guinea” (kupitia kwa Kifaransa Guinoye), ambalo limetumika kurejelea pwani ya Afrika Magharibi (na ambalo linatumika katika Ghuba ya Guinea).
Jina hilo lilichaguliwa kwa taifa jipya ili kuashiria himaya ya kale ya Ghana, ambayo kwa wakati mmoja ilienea katika sehemu kubwa ya Afrika Magharibi, ingawa kijiografia, Himaya ya Ghana inakadiriwa ilikuwa kilomita 800 mile 500 (km 800) kaskazini na magharibi mwa Ghana ya kisasa, na ilitawala majimbo katika eneo la Mto Sénégal na mashariki kuelekea Mto wa Niger, katika maeneo ya sasa ya Senegal, Mauritania na Mali.
Ghana lilichaguliwa kuwa jina rasmi la nchi ya Gold Coast nchi hii iliponyakua uhuru mnamo tarehe 6 Machi 1957; hata hivyo, Ghana haikuweza kutangaza uhuru wake kamili kutoka kwa Uingereza hadi tarehe 1 Julai 1960 ambapo nchi ilianza kujulikana kama Jamhuri ya Ghana.
Nchi hii ina eneo la kilomita mraba 238,500 (maili mraba 92,085)km2 238 500 (sq mi 92 085). Eneo hili limezungukwa na Togo kwa upande wa mashariki, Cote d’Ivoire upande wa magharibi, Burkina Faso upande wa kaskazini na Ghuba ya Guinea (Bahari ya Atlantiki) upande wa kusini.
Ghana ni nchi ambayo inapatikana katika Ghuba ya Guinea, nyuzi chache kaskazini mwa Ikweta, jambo ambalo linaipa nchi hii hali ya joto. Vilevile mstari wa Greenwich Meridian hupita ndani ya Ghana, katika jiji la viwanda la Tema. Hivyo kijiografia Ghana iko karibu zaidi ya sehemu ya “katikati” mwa ulimwengu kuliko nchi yoyote ile, ingawa sehemu halisi ya katikati, (0°, 0°) inapatikana katika Ghuba ya Guinea, katika Bahari ya Atlantiki, kwa makadirio kilomita 614 (maili 382) km 614 (mi 382) kusini mwa Accra, Ghana.
Nchi hii ina maeneo tambarare, vilima vya chini na mito michache. Nchi ya Ghana inaweza kugawanywa katika maeneo matano tofauti ya kijiografia. Eneo la pwani ni sehemu ambayo ni ya chini na iliyo na ufuo wa mchanga huku ikipakana na koko na kukingamana na mito na vijito kadha wa kadha huku sehemu ya kaskazini ikiwa na maeneo ya juu yaliyo tambarare. Eneo la kusini magharibi na kusini ya kati mwa Ghana ni sehemu iliyoinuka sawa na pana yenye misitu ikiwa na vilima vya Ashanti na eneo sawa na pana (plateau) la Kwahu na safu ya vilima vya Akuapim-Togo vinapatikana kwenye mpaka wa mashariki mwa nchi. Bonde la Volta linachukua eneo la kati mwa Ghana. Sehemu ya juu zaidi nchini Ghana ni Mlima Afadjato ulio na urefu wa mita 855 (futi 2,904)m 885 (ft 2 904) na unaopatikana kwenye safu ya vilima vya Akwapim-Togo.
Hali ya hewa ni ya hari. Kanda ya pwani ya mashariki ni ya joto na iliyokauka (angalia Dahomey Gap); pembe ya kusini magharibi, huwa na joto jingi na unyevu hewani; huku sehemu ya kaskazini ikiwa yenye joto jingi na iliyokauka. Ziwa Volta, ziwa lisilo la asili kubwa zaidi ulimwenguni, linaenea kupitia katika mafungu makubwa mashariki mwa Ghana na ndicho chanzo kikuu cha vijito vingi kama vile vya Oti na Afram.
Kuna misimu miwili mikuu nchini Ghana, masika na kiangazi. Kaskazini mwa Ghana huwa na msimu wa masika kutoka Machi hadi Novemba huku sehemu ya kusini, ukiwemo mji mkuu wa Accra, ikiwa na masika kutoka Aprili hadi Novemba katikati.
Kusini mwa Ghana kuna misitu ambayo daima ni ya kijani kibichi na ile ambayo hupoteza majani yake wakati fulani wa mwaka ikiwa na miti kama mikangazi, odumu na mipingo. Sehemu hii inayo pia mingi ya mitende ya mafuta na mikoko. Miti ya Shea, mibuyu na mikakaya hupatikana kwa kawaida katika maeneo ya Volta na kaskazini mwa nchi.
Ghana imegawiwa katika mikoa 16, ambayo yamegawiwa zaidi katika wilaya 275[10][11][12][13], kila moja ikiwa na Bunge la Wilaya (District Assembly). Chini ya wilaya kuna aina kadhaa za mabaraza, yakiwemo mabaraza 58 ya miji au maeneo, mabaraza 108 ya kanda na mabaraza 626 ya maeneo. Kamati za vitengo 16,000 huwa katika daraja ya chini zaidi.[14]
Mikoa hiyo 16 ni:
|
|
Kuna ushahidi kutoka kwa maarifa ya mambo ya kale ambao unaonyesha kwamba watu wameishi katika eneo linalojulikana siku hizi kama Ghana kutoka karibu miaka ya 1500 KK (Kabla ya Kristo).[15]
Licha ya hayo, hakuna ushahidi wa kuonyesha kuwa wakazi hao wana uhusiano na wale wa eneo hili kwa sasa. Kwa mujibu wa mapokeo simulizi, mengi kati ya makabila ya Ghana, leo kama vile watu wa chimbuko la makabila kadhaa kama Waakan, Waga na Waewe, walifika Ghana mnamo karne ya 13.
Mengi ya maeneo ya Ghana yanajumuisha eneo lililokuwa la Himaya ya Ashanti, mojawapo ya falme zilizokuwa na ushawishi mkubwa katika eneo la Afrika Kusini mwa Sahara kabla ya enzi za ukoloni.
Wahamiaji Waakan walihama kuelekea kusini na kuanzisha mataifa kadhaa, likiwemo lile la kwanza la himaya kuu ya Akan ya Wabono, ambayo kwa sasa inajulikana kama eneo la Brong Ahafo nchini Ghana.
Sehemu kubwa ya eneo la sasa la kusini na kati mwa Ghana ilikuwa imeungana chini ya Himaya ya Ashanti ya Waashanti, tawi la Waakan wa karne ya 16.
Utawala wa Waashanti ilihudumu mwanzoni kama mtandao mlegevu kabla ya kuwa ufalme ulioungana huku ukiwa na urasimu ulioendelea na wenye uchanganuzi mkubwa uliokuwa na makao yake Kumasi. Inasemekana kuwa katika kilele chake, Waasantehene wangeweza kutuma askari 500,000 vitani na kuwa na ushawishi wa kijeshi wa kiwango fulani juu ya majirani wake wote.
Thuluthi moja ya Waashanti wote walikuwa watumwa.[16]
Waga walianzisha muungano wenye ufanisi mnamo 1500[17] na Wagonja, Wadagomba na Wamamprusi, pia walipigania uwezo wa kisiasa katika miaka ya 1620.[17]
Mawasiliano ya awali na Ulaya kutoka kwa Wareno, walioingia Ghana mnamo 1419, yalizingatia upatikanaji wa dhahabu. Wareno walitua kwanza katika jiji la pwani lililokuwa makazi ya ufalme wa Wafante na kuliita eneo hili Elmina, jina ambalo linamaanisha “mgodi” kwa Kireno.
Mwaka wa 1481, Mfalme John II wa Ureno aliagiza Diogo de Azambuja kujenga Kasri ya Elmina, ambayo ilikamilishwa mwaka uliofuata. Lengo lao lilikuwa kufanya ubadilishanaji wa dhahabu, pembe za ndovu na watumwa, ili kuimarisha mamlaka yao yaliyokuwa yanakua kwa kasi katika eneo hilo.
Kufikia mwaka wa 1598 Waholanzi walikuwa wameungana nao, na kujenga ngome katika maeneo ya Komenda na Kormantsi. Mwaka wa 1637, waliiteka Kasri ya Elmina kutoka kwa Wareno na vilevile Axim mwaka wa 1642 (Ngome ya Mtakatifu Antoni).
Wafanyabiashara wengine kutoka Ulaya walijiunga nao kufikia miaka ya kati ya karne ya 17, hasa Waingereza, Wadenmarki na Waswidi. Wafanyabiashara Waingereza, waliovutiwa na rasilimali katika eneo hilo, waliliita Gold Coast, (Pwani ya Dhahabu), huku nao wafanyabiashara Wafaransa, wakivutiwa na mapambo waliyokuwa wakivaa watu wa pwani, wakiliita eneo la sehemu ya magharibi “Côte d'Ivoire", au Ivory Coast (pwani ya pembe za ndovu).
Zaidi ya ngome na kasri thelathini zilijengwa na wafanyabiashara Wareno, Waholanzi, Waingereza na Wadenmarki.
Eneo la Gold Coast lilijulikana kwa karne nyingi kama ‘Kaburi la Mtu Mweupe’ kwa sababu wengi kati ya Wazungu walioenda huko kutoka Ulaya walikufa kutokana na malaria na magonjwa mengine ya eneo la hari.[18]
Baada ya Waholanzi kuondoka mwaka wa 1874, Uingereza iliiweka Gold Coast chini ya himaya yake. Kufuatia ushindi wa Uingereza mwaka wa 1896, hadi unyakuzi wa uhuru mnamo Machi 1957, eneo la Ghana ya sasa ghairi ya sehemu ya Volta Region (British Togoland), lilikuwa likijulikana kama Gold Coast.
Vita vingi vilitokea baina ya utawala wa kikoloni na baadhi ya mataifa ya eneo hilo vikiwemo Vita vya 1806 vya Ashanti-Fante na mapambano ya kudumu ya Waashanti dhidi ya Waingereza, ambayo yalikoma baada ya Vita vya Tatu baina ya Waashanti na Waingereza (the third Ashanti-British War) (1900-1901).[19]. ]
Hata chini ya utawala wa kikoloni machifu na watu wao walipinga mara kwa mara sera za Waingereza; hata hivyo, ushawishi wa kupinga ukoloni ulikolea baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Mwaka wa 1947 chama kipya cha United Gold Coast Convention (UGCC) kilitoa wito wa “utawala wa kujitegemea katika wakati mfupi iwezekanavyo.”[20]
Baada ya kuongezeka kwa maandamano mnamo 1948, wanachama wa chama cha United Gold Coast Convention walikamatwa, akiwemo Waziri Mkuu na Rais wa baadaye, Kwame Nkrumah. Baadaye, Nkrumah aliunda chama chake mwenyewe, the Convention People's Party (CPP) ambacho kiliongozwa na usemi ‘serikali ya kujitegemea sasa’ (self government now). Alianzisha kampeni ya ‘Vitendo Chanya’ na kupata ufuasi wa watu wa sehemu za mashambani na wa daraja la wafanyakazi.[19]
Kwa mara nyingine Nkrumah alishikwa na kuzuiliwa kwa kuwa msimamizi wa chama ambacho kilisababisha ususiaji, migomo na vitendo vingine vya uasi wa raia.
Hata hivyo, baada ya kushinda wingi wa viti katika Bunge ya Kuunda Sheria mnamo 1952, Kwame Nkrumah aliachiliwa na kuchaguliwa kuwa Kiongozi wa Masuala ya Serikali.
Baada ya mazungumzo na Uingereza, hatimaye tarehe 6 Machi 1957 saa sita usiku, Kwame Nkrumah alitangaza Ghana kuwa “huru milele”.[19]
Bendera iliyokuwa na rangi nyekundu, dhahabu, kijani kibichi na nyota nyeusi ilikuwa bendera mpya mnamo 1957. Bendera hiyo iliundwa na Theodosia Salome Okoh, na rangi nyekundu inawakilisha damu iliyomwagwa ili kupata uhuru, rangi ya dhahabu inawakilisha ukwasi wa madini wa Ghana, ile ya kijani kibichi inaashiria utajiri wa kilimo na ile nyeusi ni ishara ya Uhuru wa Waafrika.[21]
Huku ikiundwa kutoka kwa muungano wa maeneo ya Gold Coast na British Togoland kufuatia matokeo ya kura ya maoni ya watu yaliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa mnamo 1956, Ghana ilikuwa nchi ya kwanza ya Afrika Kusini mwa Sahara kunyakua uhuru mnamo 1957.
Kwame Nkrumah, Waziri Mkuu wa kwanza na baadaye Rais wa nchi ya sasa ya Ghana, hakuwa tu kiongozi wa Kiafrika wa kupigana dhidi ya ukoloni ila alikuwa pia mtu aliyekuwa na ndoto ya muungano wa Afrika ambayo haingejipata katika ukoloni mamboleo. Alikuwa kiongozi wa serikali ya kwanza Afrika kukuza Muungano wa Waafrika (Pan-Africanism), wazo ambalo alilipata wakati wa masomo yake katika Chuo Kikuu Cha Lincoln lililoko Pennsylvania (Marekani), wakati ambapo Marcus Garvey alikuwa anapata umaarufu kwa harakati zake za “Back to Africa Movement." Aliunganisha ndoto za Macus Garvey na zile za mwanachuo mashuhuri Mmarekani Mweusi W.E.B. Du Bois ili kuandaa Ghana kisasa.
Kanuni za Ghana za uhuru na haki, usawa na elimu ya bure kwa wote, bila kujali kabila, dini au mila, zinatokana na utekelezaji wa wazo la Pan-Africanism.
Ingawa lengo lake la muungano wa Afrika halikuwahi kuafikiwa, Osagyefo Dr. Kwame Nkrumah, kama ajulikanavyo sasa, alishiriki kwa kiwango kikubwa katika kuzinduliwa kwa Shirika la Umoja wa Afrika, ambalo lilifuatwa mnamo 2002 na Umoja wa Afrika (African Union). Ingawa Nkrumah aliheshimika sana ng’ambo, hakuwa akipendwa katika masuala ya ndani ya nchi.[22]
Hakufeli tu kuanzisha uchumi wa viwanda, ila hata sera zake hukusu uchumi ziliishia kuifanya nchi ya Ghana kuwa maskini kuliko ilivyokuwa wakati wa kupata uhuru. Mafanikio yake yalikuwa kutambuliwa na raia wa Ghana wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa Centenary wake na siku aliliweka kama likizo umma nchini Ghana.
Hatimaye Nkrumah aliondolewa madarakani na jeshi alipokuwa ng’ambo mnamo Februari 1966, na mabadiliko hayo yalikaribishwa na wengi wa wakazi wa Ghana. Inaaminika na wengi wa wachanganuzi wa masuala ya kisiasa kwamba shirika la Marekani la Central Intelligence Agency (CIA) lilihusika na mapinduzi hayo, lakini wazo hilo halijawahi kuthibitishwa.
Mfululizo wa baadaye wa mapinduzi kati ya 1966 na 1981 uliishia kwa kuingia madarakani kwa Liuteni wa Jeshi la Wanahewa (Flight Lieutenant) Jerry Rawlings mwaka wa 1981.
Mabadiliko hayo yalisababisha kusimamishwa kwa katiba ya nchi mnamo 1981 na kupigwa marufuku kwa vyama vya kisiasa. Uchumi ulishuka sana punde baadaye, na Waghana wengi walihamia nchi zingine. Ingawa wengi wa Waghana waliohama walienda Nigeria, serikali ya Nigeria iliwarudisha Ghana karibu Waghana milioni moja mwaka wa 1983.[23]
Punde baadaye, Rawlings aliafikiana na shirika la International Monetary Fund juu ya mkataba wa mpango wa maendeleo (structural development plan) na kubadili sera nyingi za awali za uchumi na hivyo uchumi ukaanza kukua.
Katiba mpya iliyorudisha mfumo wa siasa za vyama vingi ilitangazwa mwaka wa 1992, na Rawlings alichaguliwa kuwa Rais na tena mwaka wa 1996. Katiba ya mwaka wa 1992 ilimzuia kuwania kiti hicho kwa muhula wa tatu, kwa hivyo chama chake, National Democratic Congress, kilimchagua Makamu wake wa Rais, John Atta Mills, kuwania urais dhidi ya vyama vya upinzani.
Huku akishinda uchaguzi wa mwaka 2000, John Kufuor wa chama pinzani cha New Patriotic aliapishwa kama Rais mnamo Januari 2001, na kumshinda tena Mills mwaka wa 2004; hivyo kuhudumia kama Rais kwa mihula miwili.
Mwaka wa 2009, John Atta Mills alichukua mamlaka huku kukiwa na tofauti ndogo sana ya kura 40,000 ambazo ni 0.46% [24] kati ya chama chake, National Democratic Congress, na kile cha New Patriotic Party, tukio hili likiwa la pili la ubadilishanaji wa mamlaka kutoka kwa kiongozi mmoja aliyechaguliwa kihalali kwa mwingine, na hivyo kuimarisha hadhi ya Ghana kama demokrasia iliyo imara.[25]
Kwa mujibu wa Fahirisi ya Mataifa Yaliyoanguka (Failed States Index), Ghana inaorodheshwa katika nambari ya 53 baina ya mataifa ambayo hayajaanguka huku likiorodheshwa kwa nafasi ya pili baina ya mataifa ya Afrika baada ya Mauritius. Taifa la Ghana liliorodheshwa katika nafasi ya 124 baina ya nchi 177 katika fahirisi hii na liliainishwa kama taifa la wastani.[26] Vilevile, nchi ya Ghana imo katika nafasi ya 7 baina ya nchi 48 za Afrika zilizo Kusini mwa Sahara katika fahirisi ya mwaka wa 2008 ya Ibrahim Index of African Governance ambayo ilitokana na hakiki za mwaka wa 2006. Fahirisi ya Ibrahim ni kipimo chenye uchanganuzi mwingi kuhusu maswala ya utawala barani Afrika, kinachotokana na maswala ya mabadiliko tofautitofauti ambayo huashiria kufuzu kwa serikali wakati wa kutoa huduma muhimu za kisiasa kwa wananchi wao.[27]
Taifa la Ghana lilianzishwa kama demokrasia ya bunge wakati wa kupata uhuru mnamo mwaka wa 1957, ikifuatiwa na ubadilishanaji wa serikali za kijeshi na za kiraia. Mnamo Januari 1993, serikali ya kijeshi iliondoka na kuipisha Jamhuri ya Nne baada ya uchaguzi wa urais na ubunge mnamo mwisho wa mwaka wa 1992. Katiba ya 1992 inagawa mamlaka kati ya Rais, Bunge, Baraza la Mawaziri, Baraza la Taifa na mahakama huru. Serikali huchaguliwa na upigaji kura wa haki kwa wote; ingawa bunge halina uwiano kabisa kwani wilaya zilizo na watu wachache hupata wawakilishi wengi kwa kila mtu zikilinganishwa na wilaya ambazo zina idadi ya juu ya wakazi.[14]
Mfumo wa kisheria unatokana na ule wa Uingereza yaani British common law, sheria za kimila (kitamaduni), na katiba ya mwaka wa 1992. Daraja za mahakama hujumuisha Mahakama Kuu ya Ghana (mahakama ya juu zaidi), Mahakama za Rufaa na Mahakama Kuu za Kisheria. Chini ya mahakama hizi kuna mahakama za kuzunguka, mahakama za hakimu, na mahakama za kitamaduni. Taasisi zingine zisizo chini ya sheria ni pamoja na mahakama za umma. Tangu unyakuzi wa uhuru, mahakama zimekuwa huru kwa kiwango fulani; uhuru huu unaendelea chini ya Jamhuri ya Nne. Mahakama za chini zinadhahirishwa na kupangwa upya chini ya utawala wa Jamhuri ya Nne.[14]
Vyama vya kisiasa vilihalalishwa katikati mwa mwaka wa 1992 baada ya kupigwa marufuku kwa miaka kumi. Kuna vyama vingi vya kiasisa chini ya Jamhuri ya Nne; hata hivyo vile vikubwa ni National Democratic Congress kilichoshinda uchaguzi wa urais na ubunge mnamo 1992, 1996 na 2008; New Patriotic Party, chama kikubwa cha upinzani kilichoshinda uchaguzi wa mwaka wa 2000 na ule wa 2004; People’s National Convention, na Convention People’s Party, ambacho kilichukua mahali pa chama cha awali cha Kwame Nkrumah kilichokuwa na jina lilo hilo.[14]
Tangu unyakuzi wa uhuru, Ghana imefuata kwa dhati mwelekeo wa kutojiunga na upande wa kibepari au ule wa kikomunisti (nonalignment) na pia siasa zinazopendelea siasa za umoja wa Afrika (Pan-Africanism); mawazo ambayo yanahusishwa na rais wa kwanza, Osagyefo Dr. Kwame Nkrumah. Nchi ya Ghana inapendele31ushirikiano wa kimataifa na wa kikanda wa kisiasa na wa kiuchumi, na ni mwanachama mwenye mashuhuri wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.[onesha uthibitisho]
Wanadiplomasia na wanasiasa wengi Waghana wana vyeo katika mashirika ya kimataifa. Hawa ni pamoja na mwanadiplomasia Mghana na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, Jaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai Akua Kuenyehia, na rais wa zamani Jerry Rawlings, ambaye alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (Economic Community of West African States).[14]
Nchi ya Ghana ina idadi ya watu inayokadiriwa kuwa milioni 27.
Ingawa Ghana ni kiambo cha zaidi ya makabila 70 tofauti, haijashuhudia migogoro ya kikabila kama ile ambayo imesababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi nyingi za Afrika[28].
Makabila nchini Ghana ni ya Waakan (ambalo linajumuisha Fante, Akyem, Ashanti, Kwahu, Akuapem, Nzema, Bono, Akwamu, Ahanta na makabila mengine) 45.7%, Wamole-Dagbon 18.5%, Waewe 12.8%, Waga-Adangbe (likijumuisha Ga, Adangbe, Ada, Krobo na makabila mengine) 7.1%, Wabassare 5.9%, Wakonkomba 5.7%, Waguan 3.2%, Wagurunsi 2.7%, Wakusasi 2.2%, Wabissa 1.1%, mengine (Wahausa, Wazabarema, Wafula) 1.4% (sensa ya 2021).
Lugha rasmi ni Kiingereza; hutumika sana katika masuala ya serikali na biashara. Lugha hiyo vilevile ndiyo inayotumika katika mafundisho ya elimu. Kifaransa pia kinajulikana sana na kiko mbioni kufanywa lugha rasmi ya pili.
Hata hivyo, Waghana wengi pia huzungumza kwa kiasi lugha moja ya kikabila.
Ingawa wataalamu wengine wanasema nchini Ghana huzungumzwa zaidi ya lugha na lugha ndogo 250, Ethnologue inaziorodhesha 79 tu (angalia pia orodha ya lugha za Ghana). Lugha za asili za Ghana zimegawanywa katika jamii mbili ndogo kutokana na jamii ya lugha za Kiniger-Kongo.
Lugha za jamii ndogo ya Kwa zinapatikana zaidi katika maeneo ya kusini mwa Mto Volta, huku zile za jamii ya Gur zikipatikana katika eneo la kaskazini. Kikundi cha Kwa, lugha ambayo huzungumzwa na takribani 75% ya wakazi wa nchi, kinajumuisha lugha za Akan, Ga-Dangme na Ewe. Kikundi cha Gur kinajumuisha lugha za Gurma, Grusi, na Dagbani.[29]
Lugha kumi na moja zina hadhi ya kuwa lugha zinazodhaminiwa na serikali: Akuapem Twi, Ashanti Twi, Fante, Nzema, Dagaare/Wale, Dagbani, Dangme, Ewe, Ga, Gonja na Kasem.
Ingawa si lugha rasmi, Kihausa ndiyo lugha ya mawasiliano inayozungumzwa na Waislamu wa Ghana.[30]
Kwa mujibu wa sensa ya serikali ya mwaka 2021, mgawanyiko wa kidini ni: Wakristo 71.3% (hasa Waprotestanti 49% na Wakatoliki 10%), Waislamu 20%, dini asilia za Kiafrika 3.2% [31].
Kufikia mwaka wa 2009, matarajio ya urefu wa maisha (life expectancy) wakati wa kuzaliwa ni takriban miaka 59 kwa wanaume na 60 kwa wanawake [32] huku makisio ya vifo vya watoto wachanga yakiwa 51 kwa watoto 1000 waliozaliwa hai [32].
Hesabu ya watoto wanaozaliwa pia ni takriban watoto wanne kwa kila mwanamke. Kuna takriban madaktari 15 na wauguzi 93 kwa watu 100,000.[33]
Asilimia 4.5 ya Pato la Taifa lilitumika kwa masuala ya afya mwaka wa 2003.[33]
Ghana ni nchi iliyo na makabila mbalimbali; kwa hivyo ni mchanganyiko wa tamaduni wa makabila yake yote, Ashanti, Fante, Akyem, Kwahu, Ga, Ewe, Mamprusi na Dagomba, baina ya mengine. Jambo hili linadhihirika katika upishi, sanaa na desturi ya mavazi ya Ghana.
Maadhimisho ya tamasha nchini Ghana ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Ghana na kuna tamasha nyingi kama vile Homowo, Odwira, Aboakyer, Dodoleglime na Sandema baina ya zingine. Ibada na mila kadha wa kadha hufanywa wakati wote wa mwaka katika sehemu mbali mbali za nchi, zikiwemo zile za kuzaliwa, ibada za mpito maishani kama vile kubalehe, ndoa na kifo.
Soka ndiwo mchezo ulio na umaarufu zaidi nchini. Timu za kitaifa za soka ya wanaume zinajulikana kama The Black Stars, the Black Satellites na the Black Starlets na timu hizi hushiriki katika michuano mingi ikiwemo ile ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Kombe la Dunia la FIFA na Kombe la Dunia la FIFA kwa walio chini ya miaka 20. Timu ya the Black Satellites ilishinda Kombe la Dunia la FIFA kwa walio chini ya miaka 20 mnamo 2009 baada ya kushinda timu ya Brazili ya Seleção. Kuna timu za soka kadhaa nchini Ghana za kutajika zaidi zikiwa Accra Hearts ya Oak SC na Asante Kotoko baina ya zingine. Baadhi ya wachezaji wa soka wa Ghana wanaojulikana katika daraja ya kimataifa au waliopata ufanisi katika soka ya Ulaya ni Abedi Pele, Ibrahim Abdul Razak, Tony Yeboah, Anthony Annan, John Paintsil, Asamoah Gyan, Samuel Osei Kuffour, Richard Kingston, Sulley Muntari, Laryea Kingston, Stephen Appiah, Andre Ayew, Emmanuel Agyemang-Badu, Dominic Adiyiah na Michael Essien.
Kufumwa kwa vitambaa ni kitengo muhimu cha utamaduni wa Ghana. Vitambaa hivi hutumika kutengeneza mavazi ya kiasili na ya kisasa. Michoro na rangi tofauti humaanisha vitu tofauti. Pengine Kente ndicho kitambaa mashuhuri zaidi baina ya vitambaa vyote vya Ghana. Kente ni kitambaa cha sherehe cha Waashanti ambacho kinatengenezwa kwa mkono kwenye kitanda cha mfumi. Vipande vya takribani inchi nne kwa upana hushonwa pamoja ili kuwa vitambaa vikubwa zaidi. Vitambaa hivi huwa katika rangi, ukubwa na namna tofautitofauti na huvaliwa wakati wa hafla muhimu sana za kijamii au kidini.
Katika muktadha wa kitamaduni, kitambaa cha kente kina umuhimu zaidi ya vazi tu. Ni uwakilishi wa kuonekana wa historia, na pia aina ya lugha iliyoandikwa kwa kufuma. Neno Kente lina mizizi yake katika neno la Kitwi kenten ambalo lina maana ya kikapu. Wasusi wa kwanza wa kente walitumia nyuzi za ukindu kufuma vitambaa vilivyoonekana kama kenten (kikapu); na hivyo vilikuwa vinaitwa kenten ntoma; kumanisha kitambaa cha kikapu. Jina la kiasili la Kiasante la kitambaa hiki lilikuwa nsaduaso au nwontoma, kumaanisha “kitambaa kilichotengenezwa kwa mkono kwenye kitanda cha mfumi”; hata hivyo neno kente ndilo hutumika zaidi na watu wengi siku hizi. Aina nyingi tofauti za vipande vyembamba vya vitambaa vinavyofanana na kente hufumwa na makabila mengi tofauti nchini Ghana kama Ewe, Ga na mengine ya Afrika. Kente pia hupendwa na Waafrika wanaoishi katika nchi za ng’ambo.
Nchi ya Ghana ina aina nyingi ya muziki wa kitamaduni na wa kisasa. Midundo hii hutofautiana kutoka kabila moja hadi jingine na eneo moja hadi lingine. Muziki wa Ghana unajumuisha aina nyingi tofauti za vyombo vya muziki kama vile ngoma za talking drum ensembles, zeze ya goje na kinubi cha koloko, muziki wa jumba la mfalme, ikiwemo miziki ya Waakan wa Atumpan, wa Waga wa mitindo ya Kpanlogo, na marimba ya gogo itumikayo katika muziki wa Waasonko. Aina za muziki ambazo zinajulikana zaidi kutoka Ghana ni Afro-jazz ambayo ilifumbuliwa na msanii Mghana Kofi Ghanaba.[34] na aina ya awali zaidi ya muziki wa kidunia inayoitwa Highlife. Highlife ni muziki uliochimbuka katika miaka ya mwisho ya 1800 na miaka ya mwanzo ya 1900 na kuenea kote Afrika Magharibi hasa Sierra Leone na Nigeria. Katika miaka ya 1900 aina mpya ya muziki ilizinduliwa na vijana huku ikiunganisha jinsi za Highlife, Afro-reggae, Dancehall na Hiphop. Mchanganyiko huu huitwa Hiplife. Wasanii wa Ghana kama vile mwimbaji wa R&B na Soul Rhian Benson, mwimbaji wa Highlife Kojo Antwi na msanii wa rap Tinchy Stryder (Kwasi Danquah) wamekuwa na ufanisi wa kimataifa.
Ngoma (densi) ya Ghana ina tofauti mithili ya muziki wake. Kila kabila lina ngoma zake za kitamaduni na kuna ngoma tofauti tofauti kwa hafla tofauti tofauti. Kuna ngoma za mazishi, sherehe za maadhimisho, usimulizi wa hadithi, sifa na kuabudu na kadhalika. Baadhi ya ngoma hizi ni:
Bamaya Ngoma hii huchezwa na watu wa eneo la kaskazini mwa Ghana. Inasimulia hekaya ya wakati wa ukame mkubwa. Miungu iliwaambia watu kuwa ukame huo ulikuwa umeletwa na jinsi wanaume walikuwa wakiwakandamiza na kuwatweza wanawake. Ilisema pia kwamba ukame ungeondolewa tu pale wanaume wangejizusha na kuchukua majukumu waliyokuwa wamewatwika wanawake kwa kuvaa marinda na kushiriki katika ngoma hii. Wanaume walipofanya hivi, mvua ilianza kunyesha. Kwa sasa ngoma hii huchezwa wakati wa mavuno katika eneo la kaskazini magharibi mwa Ghana na wanaume pamoja na wanawake wa Dagbani.
Adowa Ngoma ya watu wa Ashanti wa Ghana. Ngoma hii inatajika hasa kwa madaha na weledi wa mzunguko wa wachezaji. Upigaji ngoma pia unasifika kwa weledi wa mfuatano wa sauti zinazochanganyika na ngoma mbili za atumpan ambazo zinatumika kama ngoma za kuongoza au ngoma simamizi. Ngoma hii ilikuwa awali ikichezwa katika mazishi, lakini kwa sasa inachezwa pia katika tamasha za kila mwaka na mikusanyiko ya kijamii.
Kpanlongo huchezwa na watu wa Ga wa Ghana. Ngoma hii ya Kpanlongo ambayo mara nyingi huitwa “ngoma ya vijana,” ilianza kuchezwa punde tu baada ya unyakuzi wa Uhuru wa Ghana kama aina ya muziki wa burudani jijini Accra. Kpanlongo huchezwa kwa sasa kwa matukio yanayohusu maisha, tamasha na mikutano ya kisiasa.
Klama Huu ni muziki na ngoma ambayo inahusishwa na ibada za kubalehe kati ya watu wa Krobo wa Ghana. Inasisitiza kusonga kwa madaha kwa mikono na miguu. Huku wakipiga hatua ndogo kuambatana na muziki na wakigeuza vichwa kwa utaratibu kuangalia chini, wacheza ngoma huwa mfano wa madahiro tulivu. Tofauti baina ya hatua za wachezaji zinanuiwa kuonyesha uzuri wa wacheza ngoma. Mara kwa mara, wachumba wanaotazama ngoma hii kutoka pembeni huzuru jamii ya msichana baada ya sherehe kwa madhumuni ya kumposa msichana huyo.
Vyombo vya habari vya Ghana ni mojawapo ya vile vilivyo na uhuru zaidi barani Afrika. Hapo awali, vilikuwa vimewekewa vizuizi vingi wakati wa mfululizo wa mapinduzi ya serikali na viongozi wa jeshi. Sura ya 12 ya katiba ya 1992 ya Ghana inatoa hakikisho la uhuru na kujisimamia kwa vyombo vya habari huku Sura ya 2 ikizuia uthibiti.[35]
Baada ya kujinyakulia uhuru, serikali na vyombo vya habari vimekuwa mara kwa mara vikiwa na uhusiano ulio na mvutano, huku mashirika ya kibinafsi yakifungwa wakati wa mapinduzi ya kijeshi na sheria kali ili kuzuia ukosoaji wa serikali.[36] Uhuru wa vyombo vya habari ulirejeshwa mnamo mwaka wa 1992, na baada ya uchaguzi wa 2000 wa John Kufuor mivutano kati ya vyombo vya habari vya kibinafsi na serikali ilipungua. Kufuor alikuwa mtetezi mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari na alifuta sheria ya masingizio, ingawa alisisitiza kuwa ni lazima vyombo vya habari vifanye kazi kwa uwajibikaji.[37] Vyombo vya habari vya Ghana vimeelezwa kuwa “baadhi ya vile visivyo na uthibiti mkubwa na serikali mwingi” barani Afrika, huku vikifanya kazi vikiwa na masharti machache mno kwa vyombo vya habari vya kibinafsi. Vyombo vya habari vya kibinafsi mara kwa mara hukosoa sera za serikali.[38] Vyombo vya habari vilifanya kazi kwa bidii wakati wa uchaguzi wa rais wa Ghana wa mwaka wa 2008, na Chama cha Wanahabari wa Ghana (Ghanaian Journalists Association (GJA)) kilimpongeza John Atta Mills kwa ushindi wake, huku kikinuia kukuza uhusiano mwema baina ya vyombo vya habari na serikali.[39]
Kiwango cha kujua kusoma na kuandika kwa watu wazima kilikuwa 65% mnamo 2007, huku wanaume wakiwa 71.7% na wanawake wakiwa 58.3%.
Nchi ya Ghana ina mfumo wa elimu ya msingi wa miaka 6 kuanzia umri wa miaka sita, na, chini ya mageuzi ya elimu yaliyotekelezwa mnamo 1987 na kurekebishwa mnamo 2007, watoto huingia katika mfumo wa miaka mitatu wa elimu ya upili ya daraja la chini.
Mwishoni mwa mwaka wa tatu katika shule ya upili ya Junior High, kuna mtihani wa lazima unaojulikana kama Basic Education Certificate Examination (BECE).
Wale wanaoendelea na masomo ni lazima wamalize masomo ya miaka mitatu ya shule ya upili ya daraja ya juu (senior high school - SHS) na kufanya mtihani wa kukubaliwa kuingia katika masomo ya chuo kikuu au taasisi yoyote ile.
Kwa sasa, Ghana ina shule za msingi 21,530, shule za upili za daraja ya chini 8,850, shule za upili za daraja ya juu 900, vyuo vya mafunzo vya umma, 52, vyuo vya mafunzo vya kibinafsi, 5[40] vyuo vya elimu ya sanaa, 5[40] taasisi za umma ambazo si vyuo vikuu, 4[40] zisizo chuo kikuu Msingi umma taasisi, 8[40] vyuo vikuu 4 na zaidi ya taasisi za kibinafsi 45.[40]
Wengi baina ya Waghana wanaweza kupata huduma za elimu ya msingi na ya upili kwa urahisi. Idadi hizi zinaweza kutofautishwa na zile za chuo kikuu kimoja tu na shule chache tu za upili na za msingi zilizokuwepo wakati wa kujinyakulia uhuru mnamo 1957.
Gharama ya nchi ya Ghana kwa elimu imekuwa kati ya asilimia 28 na 40 ya bajeti yake ya mwaka katika mwongo mmoja uliopita.
Mafunzo yote hufanywa kwa lugha ya Kingereza ambayo ndiyo lugha rasmi ya Ghana, na hufanywa na walimu Waghana waliohitimu.
Masomo yanayofunzwa katika Shule ya Msingi au ya Mwanzo ni pamoja na Kingereza, Lugha na Utamaduni wa Ghana, Hisabati, masomo ya masuala ya Mazingira, Masomo ya Kijamii na Kifaransa kama lugha ya tatu, yakiongezwa masomo ya Sayansi Jumuishi au ya Ujumla, masomo ya mwanzo ya Ustadi wa Ufundi (Pre-vocational Skills and Pre-technical skills) Elimu ya Dini na Maadili na shughuli za utendaji kama vile Muziki, Ngoma na Elimu ya Mazoezi ya Viungo.
Mtaala wa daraja la upili la Senior High una masomo ya Lazima na yale ya Kuchagua. Wanafunzi wanapaswa kuchukua masomo manne ya lazima ya Lugha ya Kingereza, Hisabati, Sayansi ya Ujumla (yakiwemo masomo ya Sayansi, Kilimo na Masomo ya maswala ya Mazingira) na Masomo ya Kijamii (uchumi, jiografia, historia na serikali). Wanafunzi wa shule ya upili vilevile hufanya masomo matatu ya kuchaguliwa kati ya matano yafuatayo: Mtaala wa Kilimo, Mtaala wa Kijumla (chaguo la Sanaa au Sayansi), Mtaala wa somo la Biashara, Mtaala wa Ufundi (Vocational Programme and Technical Programme).[41]
Mbali na shule za msingi na za upili zinazofuata mfumo wa elimu wa Ghana, kunazo shule za kimataifa kama vile Ghana International school, Lincoln Community School na SOS-Hermann Gmeiner International College ambazo hufuata mfumo wa International Baccalaureat, Advanced Level General Certificate of Education na International General Certificate of Secondary Education (IGCSE).
Huku ikiwa na asilimia 83 ya watoto wake shuleni, kwa sasa nchi ya Ghana ni baina ya nchi zilizo na viwango vya juu zaidi vya uandikishaji shuleni katika eneo la Afrika Magharibi.[42]
Uwiano wa wasichana na wavulana katika ujumla wa mfumo wa elimu ni 1:0.96, ambao kwa nchi ya Afrika Magahribi, ni mafanikio makubwa.[43] Kadiri ya watoto 500,000 hawaendi shuleni kwa sababu ya ukosefu wa mapato ya kuwezesha ujenzi wa shule, kutoa vitabu vya kusoma vya kutosha na kutoa mafunzo kwa walimu wapya.[43]
Chuo Kikuu cha zamani zaidi nchini Ghana, Chuo Kikuu cha Ghana, ambacho kilianzishwa mnamo mwaka wa 1948, kilikuwa na takriban jumla ya wanafunzi 29,754 katika mwaka wa 2008.[44] Tangu unyakuzi wa uhuru wa Ghana, nchi hii imekuwa mojawapo ya vitovu vya elimu katika eneo la Afrika Kusini mwa Sahara na imekuwa mwenyeji wa watu maarufu kama vile Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, Alhaji Sir Dauda Jawara wa The Gambia na Cyprian Ekwensi wa Nigeria baina ya wengine. Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Kwame Nkrumah, ambacho ndicho chuo kikuu cha pili kuanzishwa nchini Ghana, ndicho chuo cha kwanza cha masomo ya sayansi na teknolojia nchini humo na katika ukanda wa Afrika Magharibi.
Ikiwa imejaliwa sana na maliasili, nchi ya Ghana ina mapato yanayokadiriwa kupata kila mtu (per capita output) yaliyo mara mbili yakilinganishwa na yale ya nchi zilizo maskini zaidi za Afrika Magharibi. Hata hivyo, Ghana imebakia kutegemea kwa kiwango fulani biashara na usaidizi wa kimataifa na vilevile shughuli za uwekezaji kutokana na Waghana wanaoishi nchi za ng’ambo. Karibu 28% ya wakazi wanaishi chini ya mstari wa kimataifa wa umaskini wa dola za kimarekani 1.25 kwa siku,[45] na kwa mujibu wa wa Benki ya Dunia, kisio la mapato ya kila mtu (per capita income) ya Ghana yamekuwa mara dufu lakini kwa shida kwa miaka 45 iliyopita.[46]
Nchi ya Ghana, ikijulikana kwa dhahabu yake katika enzi za ukoloni, bado ni kati ya wazalishaji wakuu ulimwenguni wa dhahabu. Mauzo yake mengine nje ya nchi kama vile kakao, mbao, umeme, almasi, bauxiti, na manganisi ni uzalishaji mkuu wa fedha za kigeni.[47] Kiwanja cha mafuta kinachoripotiwa kuwa na hadi pipa bilioni 3 (480,000,000 m3 billion barrels 3 (m3 480 000 000) za mafuta mepesi kiligunduliwa mnamo mwaka wa 2007.[48] Utafutaji wa mafuta bado unaendelea na kiasi cha mafuta kinaendelea kuongezeka.[49]
Bwawa la Akosombo, ambalo lilijengwa juu ya Mto Volta mnamo mwaka wa 1965 linatoa umeme unaozalishwa na maji kwa nchi ya Ghana na nchi zinazoizunguka.
Nguvukazi ya Ghana katika mwaka wa 2008 ilikuwa jumla ya watu milioni 11.5. Uchumi unaendelea kutegemea sana kilimo ambacho huchangia 37% ya Pato la Taifa na kutoa ajira kwa kwa 56% ya watu wanaofanya kazi, hasa wenye ardhi ndogo. Sekta ya viwanda ni sehemu ndogo tu ya uchumi wa Ghana iliyochangia kwa ujumla 7.9% ya Pato la Taifa mnamo 2007.[50]
Sera za kiuchumi zisizofaa za serikali za kijeshi zilizopita na masharti ya vikosi vya kulinda usalama katika maeneo ya kanda vimechangia mfumuko katika fedha za nakisi, kushuka thamani kwa Sidi, na kuongezeka kwa kutoridhika kwa umma katika maswala ya hatua za kupunguza ugumu wa maisha. Hata hivyo, Ghana inabakia kuwa mojawapo baina ya nchi za Afrika nzima ambazo zina ustawi wa kiuchumi.
Mnamo Julai 2007, Benki ya Ghana ilianzisha shughuli ya kugeuza sarafu, kutoka kwa Sidi (¢) hadi kwa sarafu mpya, Sidi ya Ghana (GH¢). Kiwango cha ubadilishanaji ni Sidi moja ya Ghana kwa kila Sidi 10,000. Benki ya Ghana ilizindua kampeni kabambe katika vyombo vya habari ili kuelimisha umma juu ya mageuzo haya.
Sarafu mpya ya Sidi ya Ghana iko imara kwa kiwango kikubwa na katika mwaka wa 2008 ilibadilishwa kwa ujumla kwa thamani ya dola moja ya marekani kwa Sidi 1.1 ya Ghana.[51] Kodi ya Ongezeko la Thamani ni kodi ya matumizi itozwayo nchini Ghana. Utaratibu huu wa kodi ambao ulianza mnamo 1998 ulikuwa wa kiwango kimoja lakini tangu Septemba 2007 utaratibu wa viwango kadhaa ulizinduliwa.
Mnamo 1998, kiwango cha kodi kilikuwa ni 10% na na kilirekebishwa mnamo mwaka wa 2000 na kuwa 12.5%. Hata hivyo baada ya kupitishwa kwa Sheria ya 734 (Act 734) ya mwaka 2007, kodi ya usawa ya 3% (a 3% VAT Flat Rate Scheme (VFRS) ) ilianza kufanya kazi kwa sekta ya usambazaji wa rejareja. Hii inawezesha wauzaji wa rejareja wa bidhaa zinazotozwa ushuru chini ya Sheria ya 546 (Act 546) kotoza ushuru wa pambizoni wa 3% kwa mauzo yao na kuhesabu ushuru huu pamoja na ule wa VAT. Hii inanuia kurahisisha utaratibu wa uchumi na kuongezeka kwa maafikiano.
Shirika | Ukaguzi | Nafasi |
---|---|---|
Heritage Foundation / The Wall Street Journal | Faharisi ya Uhuru wa Uchumi (Index of Economic Freedom) | 91 juu ya 157[52] |
Reporters Without Borders | Faharisi ya Ulimwengu mzima ya Uhuru wa Vyombo vya habari (Worldwide Press Freedom Index) | 31 juu ya 173[53] |
Transparency International | Fahirisi ya Matazamo wa Ufisadi) Corruption Perception Index | 69 out of 179[54] |
United Nations Development Programme | Fahirisi ya Maendeleo ya Binadamu (Human Development Index) | 135 juu ya 177[55] |
Maono ya Ubinadamu | Fahirisi ya Amani katika ngazi za Kimataifa (Global Peace Index) | 40 juu ya 121[56] |
World Economic Forum | Ripoti ya Ushindani katika ngazi za Kimataifa (Global Competitiveness Report) | hakuna nafasi zilizotolewa[57] |
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.