From Wikipedia, the free encyclopedia
Makala hii inahusu nchi ya Malawi. Kwa maana mbalimbali za neno taz. Malawi (maana)
| |||
Lugha rasmi | Chichewa, Kiingereza | ||
Mji Mkuu | Lilongwe | ||
Serikali | Jamhuri | ||
Rais | Lazarus Chakwera | ||
Eneo | km² 118.484 | ||
Wakazi | 18.143.217 (Julai 2018) | ||
Wakazi kwa km² | 153.1 | ||
JPT/Mkazi | 157 US-$ (2004) | ||
Uhuru | kutoka Uingereza tarehe 06.07.1964 | ||
Pesa | Kwacha ya Malawi | ||
Wimbo wa Taifa | Mlungu salitsani Malawi | ||
Malawi (wakati wa ukoloni iliitwa Unyasa au Nyasaland) ni nchi ya bara la Afrika iliyopo kusini-mashariki, ikipakana na Tanzania, Msumbiji na Zambia.
Jina la nchi limeteuliwa kutokana na ufalme wa kihistoria wa Maravi.
Sehemu kubwa ya eneo lake ni ziwa linaloitwa na majirani "Ziwa Nyasa" au "Niassa", lakini "Ziwa Malawi" hapa nchini. Kati ya Malawi na Tanzania kuna mzozo kuhusu eneo la ziwa ambao unazidi kufanyiwa kazi.
Wakazi wa kwanza wa Malawi walikuwa wawindaji-wakusanyaji Wasan.
Katika karne ya 10 BK walifika Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi. Wengi walizidi kuelekea kusini, lakini wengine walihamia nchini.
Hakuna habari za kimaandishi kabla ya kufika kwa Wazungu. Tangu karne ya 16 ufalme wa Wamaravi ulikuwepo upande wa kusini wa ziwa. Wamaravi walipanua utawala wao. Lakini katika karne ya 19 walishambuliwa sana na Wayao walioendesha biashara ya watumwa wakiwakamata katika eneo la ziwa na kuwapeleka hadi pwani ya Bahari Hindi kama vile Kilwa.
Mwaka 1859 Mwingereza David Livingstone alifika ziwani.
Wamisionari walimfuata, hasa Wapresbiteri kutoka Uskoti, waliotafuta wafuasi wa Ukristo na kumpambana na wafanyabiashara ya utumwa.
Mwaka 1891 serikali ya Uingereza iliweka nchi upande wa magharibi na kusini kwa ziwa chini ya ulinzi wake ikawa „Nyassaland Protectorate“, halafu tangu 1907 koloni la Unyasa.
Wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Waingereza waliogopa kushambuliwa kutoka Afrika ya Mashariki ya Kijerumani wakachukua hatua za kudai huduma za nyongeza kutoka kwa wananchi. Hii ilisababisha ghasia ya John Chilembwe dhidi ya wakoloni.
Baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia Waingereza waliunganisha Unyasa na Rhodesia (leo Zambia na Zimbabwe) kuwa Shirikisho la Afrika ya Kati mwaka 1953. Shirikisho hilo halikudumu hadi mwisho wa ukoloni kutokana mielekeo tofautitofauti katika sehemu tatu za shirikisho.
Katika Unyasa daktari Hastings Kamuzu Banda alijitokeza kuwa mwanasiasa aliyependelewa na wananchi wengi, akawa waziri mkuu wakati wa Unyasa kupata madaraka ya kujitawala katika mambo ya ndani na baadaye rais wa kwanza wa taifa.
Mwaka 1964 Unyasa (Nyassaland) ilikuwa nchi huru kabisa lakini bado sehemu ya Jumuiya ya Madola chini ya malkia wa Uingereza kwa miaka miwili ya kwanza.
Mwaka 1966 Banda alitangaza kura ya katiba mpya iliyopokewa na wananchi. Nchi ilipata jina la Malawi na chama cha Malawi Congress Party kikawa chama pekee.
Banda aliendelea kutawala, akatangazwa kuwa rais kwa muda wote wa maisha yake mwaka 1971.
Mabadiliko ya kimataifa baada ya kuporomoka kwa Ukomunisti na ukuta wa Berlin miaka 1989/1990 yalileta shinikizo kote Afrika dhidi ya serikali zilizofuata mtindo wa chama kimoja. Shinikizo hilo lilimkuta Banda mzee na mgonjwa ilhali watu wa familia yake wakitawala kupitia yeye. Hali ya uchumi ilikuwa duni, rushwa na magendo juu.
Mwaka 1993 serikali yake ililazimishwa kukubali kura ya wananchi wote walioamua kumaliza mfumo wa chama kimoja na kuanzisha kipindi kipya.
Uchaguzi huru wa mwaka 1994 ulimaliza utawala wa MCP ukamfanya Bakili Muluzi wa United Democratic Front (UDF) ndiye rais aliyechaguliwa mara ya pili 1999.
Katika uchaguzi wa mwaka 2004 alishinda tena mgombea wa UDF, ndiye Bingu Mutharika aliyeapishwa kuwa rais wa Malawi tarehe 24 Mei 2004 huko Blantyre.
Malawi ilikuwa na siasa ya chama kimoja chini ya rais wa kwanza Hastings Kamuzu Banda tangu kupata uhuru mwaka 1964 na masahihisho ya katiba 1966.
Tangu kura ya wananchi mwaka 1993 Malawi imeanzisha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.
Kutokana na katiba ya 1995 rais wa taifa anayechaguliwa na wananchi ndiye mkuu wa dola pia mkuu wa serikali. Makamu wa rais anachaguliwa pamoja naye lakini rais ana haki ya kumteua makamu wa pili asiyetoka katika chama chake.
Mawaziri huteuliwa ama kati ya wabunge au nje ya bunge.
Wabunge 193 wanachaguliwa moja kwa moja na wananchi kwa muda wa miaka mitano.
Mahakama zinafuata mtindo wa Uingereza. Majaji huteuliwa kwa muda wa maisha; wanatakiwa kuwa huru na kutoathiriwa na siasa.
Utawala hutekelezwa katika mikoa mitatu ya nchi zinazogawiwa katika wilaya 28. Wakuu wa mikoa na wilaya huteuliwa na serikali kuu.
Mnamo Novemba 2000 palitokea uchaguzi wa kwanza wa ngazi ya chini mjini na vijijini.
Serikali za mitaa zimeundwa na wilaya 28 katika maeneo matatu (Kaskazini, Kati na Kusini) yanayotawaliwa na Watawala wa Maeneo na Wakuu wa Wilaya ambao wanachaguliwa na serikali kuu.
Chini ya ngazi ya wilaya kuna tarafa na vijiji vinavyoitwa maeneo madogo ya machifu.
Uchaguzi wa kwanza wa Serikali za mitaa katika historia ya mfumo wa vyama vingi ulifanyika mnamo 21 Novemba 2000. UDF ilishinda asilimia 70 ya viti hivi katika uchaguzi huu.
Wilaya ni hizi zifuatazo:
Wakazi wengi ni wa makabila ya Wabantu na wanatumia lugha za Kibantu, hasa Kichewa (zaidi ya 57%), lakini lugha rasmi ni Kiingereza.
Upande wa dini, kadiri ya sensa ya mwaka 2018, wakazi wengi ni Wakristo (77.5%, kati yao Wakatoliki 17.2%), wakifuatwa na Waislamu (13.8%).
Nchi za Afrika | |
---|---|
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe | |
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika | |
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira |
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Malawi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.