From Wikipedia, the free encyclopedia
Mtume Andrea alikuwa Myahudi wa karne ya 1, mmoja kati ya wawili wa kwanza kati ya Mitume wa Yesu.
Mitume wa Yesu |
---|
|
Anaheshimiwa na Wakristo wote kama mtakatifu, hasa tarehe 30 Novemba iliyo sikukuu yake[1].
Ni msimamizi wa Uskoti, Russia, Ugiriki, Romania, Malta, Prussia, na wa mabaharia, wavuvi, na waimbaji.
Inakadiriwa alizaliwa mwaka 6 K.K. huko Bethsaida akauawa 60 hivi huko Patrasso (Ugiriki).
Jina lake asili la Kiyahudi halijulikani. Kwa Kigiriki aliitwa Ανδρέας (Andreas, maana yake Mwanamume, Rijali). Anaitwa pia Protocletos yaani Wa kwanza kuitwa (na Yesu Kristo).
Agano Jipya linasema Andrea alikuwa ndugu wa Mtume Petro, mwana wa Yona au Yohana (Math 16:17; Yoh 1:42).
Wote wawili walihamia Kafarnaumu ili kufanya kazi ya uvuvi, na ndipo walipoitwa na Yesu kuwa "wavuvi wa watu" (ἁλιείς ἀνθρώπων, halieis anthropon).
Injili ya Yohane inaarifu kuwa Andrea aliwahi kuwa mwanafunzi wa Yohane Mbatizaji, mpaka nabii huyo alipomuelekeza amfuate Yesu Kristo, "Mwanakondoo wa Mungu" atakayekamilisha kazi yake mwenyewe (Yoh 1:35-40). Andrea akiwa wa kwanza kumtambua Yesu kuwa Masiya, alimtambulisha kwa ndugu yake (Yoh 1:41).
Ni baada ya hapo kwamba waliitwa kuacha yote wamfuate Yesu (Mk 1:17-18; Math 4:19-20; Lk 5:11).
Katika Injili Andrea anatajwa mara kadhaa kuwa karibu sana na Yesu (Mk 13:3; Yoh 6:8, 12:22), lakini katika Matendo ya Mitume anatajwa mara moja tu, katika orodha ya Mitume (1:13).
Mwanahistoria Eusebius wa Kaisarea anataja Asia Ndogo, Scizia, pwani ya Bahari Nyeusi na mto Volga hadi Kiev kuwa mahali pa utume wake baada ya ufufuko wa Yesu.
Mapokeo yanadai alisulubiwa huko Patrasso juu ya msalaba wenye umbo la X uliopewa jina lake.
Kati ya vitabu vilivyokataliwa na Kanisa (Decretum Gelasianum ya Papa Gelasio I) kuna Injili ya Andrea na Matendo ya Andrea vilivyoandikwa karne ya 3.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.