From Wikipedia, the free encyclopedia
Mitazamo juu ya Yesu ni tofauti sana kati ya watu waliopo duniani, ambao karibu wote wamesikia walau kwa kiasi fulani habari zake.[1]
Uenezi wa habari hizo na wa mafundisho ya Yesu, hasa kwa njia ya vitabu 27 vya Agano Jipya, umeathiri sana historia ya binadamu, hasa ya mabilioni waliomsadiki kuwa Kristo na Mwana wa Mungu (ambao kwa sababu hiyo wanaitwa Wakristo).[1][2][3]
Hao wanaamini kwamba katika Pasaka yake (labda mwaka 30 BK) yeye alikufa kwa kulipia dhambi za wote akafufuka mtukufu kama Bwana wa vyote ili avikamilishe ndani mwake milele.[4][5][6]
Wakristo, wakiguswa na upendo wake, wanakubali changamoto ya kumfuata kwa kujitoa moja kwa moja kwa ajili ya watu wote.
Mbali na wafuasi wake, ambao wa kwanza walitokea dini ya Uyahudi, wana wa Israeli walimkataa moja kwa moja. Wataalamu wa Tanakh (Biblia ya Kiebrania) hawaoni utabiri wa manabii wa kale kutimia ndani mwake.
Katika Uislamu, Yesu (akiitwa kwa heshima nabii Isa bin Mariamu) ni kati ya manabii wakuu na wanaopendwa zaidi, lakini ni mtu tu, asiyetakiwa kabisa kulinganishwa na Mungu.
Dini ya Bahai inamtambua Yesu kama tokeo mojawapo la Mungu pekee, ambaye pamoja na wengine waliwaonyesha watu sifa za Mungu. Bahá'í inakanusha uwezekano wa Umungu kuwemo katika mwili wa mtu fulani tu.
Ubuddha na dini nyingine, hasa za Asia Mashariki, hazina mtazamo maalumu juu ya Yesu, kwa sababu zilianzishwa kabla ya ujio wake.
Watu wasio na dini wanamuona Yesu kama mtu wa kawaida, hata kama aliathiri sana historia ya dunia, au kama shujaa wa upendo aliyefundisha na kutekeleza maadili ya hali ya juu.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.