Remove ads
From Wikipedia, the free encyclopedia
Yohane Mbatizaji (7 K.K. - 29 B.K. hivi) alikuwa nabii wa Uyahudi aliyeishi wakati wa Yesu wa Nazareti na kumtangulia miezi tu kuzaliwa, kuanza utume na kuuawa.
Kufuatana na Injili ya Luka sura 1-2 Yohane na Yesu walikuwa ndugu na mama zao walikuwa wazito kwa wakati mmoja.
Habari zake zinapatikana katika Biblia ya Kikristo na katika vitabu vya mwanahistoria Yosefu Flavius.
Anaheshimiwa na Wakristo na Waislamu kama nabii na mtakatifu.
Pengine sikukuu yake muhimu zaidi ni ile ya kuzaliwa [1] (inayoadhimishwa na Kanisa la magharibi tarehe 24 Juni [2], miezi sita kabla ya Krismasi), lakini ipo pia sikukuu ya kifodini chake [3] tarehe 29 Agosti [4].
Kadiri ya Injili ya Luka, Yohane alizaliwa kimuujiza na kuhani mzee Zakaria na mke wake tasa Elizabeti[5].
Bado mtoto alikwenda kuishi jangwani, labda kutokana na kifo cha wazazi. Wataalamu mbalimbali wanadhani kwamba huko alikuwa akiishi kati ya Waeseni, wafuasi wa madhehebu ya Kiyahudi yenye msimamo mkali hata kuliko ule wa Mafarisayo.
Alipofikia utu uzima alianza kuhubiri "mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberio" (Luka 3,1) yaani mnamo 27/29 BK.
Yohane alikuwa mhubiri aliyewaonya kwa ukali wasikilizaji wake na kudai wajiandae kwa hukumu ya Mungu.
Akawakaribisha wapate ubatizo wa maji kama alama ya utakaso na mwanzo wa maisha mapya.
Injili ya Mathayo katika sura ya 3 inasimulia: "4 Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni. 5 Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka mkoa wote wa Yudea na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea, 6 wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani."
Alimbatiza pia Yesu ambaye naye baadaye akaanza kuhubiri.
Hivyo katika Injili Yohane anatazamwa kama mtangulizi wa Yesu aliyetangaza ujio wake na kumtambulisha kama "Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu" na atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu.
Yohane katika mahubiri yake alipinga bila hofu matendo ya mfalme Herode Antipa hata akakamatwa naye na kufungwa katika ngome ya Makeronte, katika Yordani ya leo.
Kufuatana na Injili ya Marko sura ya 6 aliuawa gerezani huko alivyotaka Herodia mke wa mfalme, akakatwa kichwa kwa ombi la Salome, binti yake, nacho kilipelekwa katika sinia au bakuli mbele ya mfalme na wageni wake wakiwa wanasherehekea sikukuu yake ya kuzaliwa.
Hivyo huyo mtangulizi wa Bwana, kama taa iwakayo na kung'aa, alishuhudia ukweli kwa maisha na mauti yake vilevile.
Yohane alikuwa pia na kundi la wafuasi walioendelea kama ushirika baada ya kifo chake.
Dini ya Wamandayo inadai kuwa imetokana na ushirika huo: katika Kurani hao wanaitwa "sabiyuna" au wabatizaji.
Yohane anatajwa kwa heshima katika Kurani pia, kwa jina la nabii Yahya (يحيى بن زكريا, Yahya ibn Zakariya).
Kichwa cha Yohane kiliaminiwa kimeweza kutunzwa kikaheshimiwa kama salia takatifu.
Kuna vichwa mbalimbali vilivyotajwa kuwa kichwa cha Yohane.
Kaburi moja la kichwa kipo mjini Dameski kilipokuwa ndani ya kanisa kuu, na baada ya Waislamu kubomoa kanisa, kaburi lilitunzwa na liko sasa ndani ya msikiti wa Umawiya.
Kichwa kingine kinachoitwa ni cha Yohane chaonyeshwa katika kanisa la "San Silvestro in Capite" mjini Roma; kingine huko Amiens (Ufaransa).
Kuna pia mikono ya Yohane inayoonyeshwa mahali mbalimbali.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.