From Wikipedia, the free encyclopedia
Maria Magdalena, yaani wa Magdala (kwa Kigiriki: Μαρία ἡ Μαγδαληνή) ni mmoja kati ya wanafunzi maarufu zaidi wa Yesu wa Nazareti, hasa kutokana na sifa yake ya kuwa mtu wa kwanza kumuona amefufuka (Mk 16:9[1]; Yoh 20:16).
Kwa kuwa alitumwa naye kuwapasha habari hiyo Mitume, kuanzia Thoma wa Akwino anaitwa "Mtume wa Mitume"[2].
Ni kwamba, kadiri ya Injili, baada ya kushuhudia kifo cha Yesu na mazishi yake (Mk 15:40-16:1; Math 27:56-28:1; Yoh 19:25), upendo na juhudi vilimfanya mwanamke huyo awahi kwenye kaburi lake alfajiri ya siku ya Jumapili. Huko alitokewa na malaika na kuambiwa amefufuka.
Ndiye aliyewapasha habari hiyo mitume wa Yesu kabla hawajaenda kaburini na kulikuta halina maiti.
Baada ya Maria, hao pia walitokewa na Yesu mwenyewe, kuanzia mtume Petro.
Kabla hajaanza kumfuata, Maria alikuwa amepagawa na mapepo saba (Mk 16:9). Alipoponywa na Yesu, alijitolea kumhudumia na mali yake pamoja na wanawake wengine (Lk 8:2).
1 Alfajiri na mapema Jumapili, kukiwa bado na giza, Maria Magdalene alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa kaburi.
2 Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, "Wamemwondoa Bwana kaburini, na wala hatujui walikomweka."
3 Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda kaburini.
4 Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini.
5 Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini hakuingia ndani.
6 Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini; humo akaona sanda,
7 na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani. Hicho kitambaa hakikuwekwa pamoja na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa mahali peke yake.
8 Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyemtangulia kufika kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaaamini.
9 Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema kwamba ilikuwa lazima afufuke kutoka wafu).
10 Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani.
11 Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia. Huku akiwa bado analia, aliinama na kuchungulia kaburini,
12 akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni.
13 Hao malaika wakamwuliza, "Mama, kwa nini unalia?" Naye akawaambia, "Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!"
14 Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu amesimama hapo, lakini asitambue ya kuwa ni Yesu.
15 Yesu akamwuliza, "Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?" Maria, akidhani kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia, "Mheshimiwa, kama ni wewe umemwondoa, niambie ulikomweka, nami nitamchukua."
16 Yesu akamwambia, "Maria!" Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, "Raboni" (yaani "Mwalimu").
17 Yesu akamwambia, "Usinishike; sijakwenda bado juu kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu uwaambie: nakwenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu."
18 Hivyo Maria Magdalene akaenda akawapa habari wale wanafunzi kuwa amemwona Bwana, na kwamba alikuwa amemwambia hivyo.
Maria Magdalena anahesabiwa mtakatifu katika madhehebu mengi ya Ukristo, akiadhimishwa tarehe 22 Julai[3]. Katika Kanisa la Kilatini Papa Fransisko ameipa hadhi ya sikukuu.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.