Katiba hiyo inaeleza kuwepo kwa kaunti 47 nchini katika mafungu 191 na 192, pamoja na ‘County Governments Act of 2012”. Kaunti hizi zilichukua nafasi za Mikoa ya Kenya. Mipaka ya kaunti iliwekwa kulingana na mipaka ya wilaya za kenya zilizokuwa zimeanzishwa kisheria mwaka wa 1992.
Mipaka ya kaunti hizo ni pia msingi wa maeneo ya uchaguzi wa mwakilishi mwanamke wa kaunti, seneta na gavana. [2][3]
Utendaji katika Kaunti
Utendaji wa kaunti una wajibu wa kutekeleza madaraka ya serikali ya kaunti. Gavana ndiye mtendaji mkuu na husaidiwa na naibu wa gavana. Kila kaunti ina kamati ya utendaji iliyoundwa na[4]:
Gavana
Naibu wa gavana
Kamati ya watu wasiozidi thuluthi ya wabunge wa kaunti au watu kumi, ambapo bunge la kaunti lina watu zaidi ya 30
Katibu wa kaunti
Kazi ya utendaji ni:
Kutekeleza sheria za bunge la kaunti
Kutekeleza sheria za kitaifa ndani ya mipaka ya kaunti
Kuendesha na kuratibu shughuli za utawala wa kaunti na idara zake
Kutayarisha miswada ya sheria na kuzipeleka katika bunge la kaunti
Kuwajibika kwa bunge la kaunti na wananchi wa kaunti
Bunge la Kaunti
Kila kaunti ina bunge. Wajumbe huchaguliwa kutoka wadi za kaunti katika uchaguzi mkuu. Pia, kuna wajumbe wa kuteuliwa ambao huwakilisha vikundi vilivyotengwa, vijana na kwa ajili ya kusawazisha uwakilishi wa jinsia. Wajumbe hutumikia kwa muhula wa miaka mitano. Bunge huongozwa na spika ambaye hafai kuwa mjumbe.
Majukumu yake ni:
kuchuja na kuthibitisha waliopendekezwa kuteuliwa katika ofisi za umma katika kaunti
Kutengeneza sheria za kaunti
kuthibitisha bajeti na matumizi ya serikali ya kaunti
Serikali za kaunti zina wajibu wa kutunga sheria katika mabunge ya kaunti na utendaji katika kaunti. Kazi ya kaunti kulingana na kiambatisho cha nne cha katiba ni:
Ukulima, ikiwa ni pamoja na:
mimea na ufugaji wa wanyama
maeneo ya uuzaji wa mifugo
vichinjio vya kaunti
udhibiti wa magonjwa ya wanyama na mimea
uvuvi
Huduma za afya
vifaa vya afya vya kaunti na maduka ya dawa
huduma za ambulensi
ukuzaji wa huduma msingi za afya
utoaji leseni na udhibiti wa shughuli zinazohusu uuzaji wa vyakula kwa umma
huduma za afya ya mifugo
makaburi, mochari na vifaa vya uchomaji maiti
kuondoa taka na maeneo ya kutupia taka
Udhibiti wa uchafuzi wa hewa, kelele, kero zinginezo kwa umma na matangazo ya nje
Shughuli za kitamaduni, burudani za umma na maeneo ya umma, ikiwa ni pamoja na:
kamari, kasino na aina nyingineyo ya kamari
mbio
utoaji leseni za pombe
sinema
maonyesho ya video na ukodishaji wake
maktaba
makumbusho
shughuli za michezo na utamaduni na maeneo yake
bustani, fuko na maeneo ya starehe
Usafiri katika kaunti, ikiwa ni pamoja na:
barabara za kaunti
mataa ya barabarani
trafiki na maegesho
usafiri wa umma barabarani
feri na bandari, isipokuwa udhibiti wa mambo yanayohusiana na usafiri wa meli wa kitaifa na kimataifa .
Udhibiti wa wanyama na ustawi wao, ikiwa ni pamoja na:
kutoa leseni za mbwa
maeneo ya malazi, utunzaji na uzikaji wa wanyama
Uendelezaji wa biashara na udhibiti wake, ikiwa ni pamoja na:
masoko
kutoa leseni za biashara (isipokuwa udhibiti wa wataalamu)
shughuli za biashara zilizo haki
utalii wa ndani kwa ndani
vyama vya ushirika
Upangaji wa kaunti na uendelezaji, ikiwa ni pamoja na:
takwimu
usoroveya wa ardhi na uchoraji ramani
mipaka na nyua
makazi
maelekezo ya usambazaji wa umeme na gesi na udhibiti wa nishati
Elimu ya chekechea, vyuo vya ufundi vijijini, vituo vya ufundi na maeneo ya malezi ya watoto
Utekelezaji wa sera maalum za serikali ya kitaifa kuhusu raslimali za kiasili na uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na:
uhifadhi wa udongo na maji
misitu
Huduma za kaunti kwa umma, ikiwa ni pamoja na:
mifumo ya kudhibiti maji kutokana na kibunga
huduma za maji na usafi
Huduma za zimamoto na udhibiti wa majanga
Udhibiti wa dawa za kulevya na ponografia
Kuhakikisha na kuratibu ushiriki wa jamii na kata katika utawala katika ngazi za mashinani na kusaidia jamii na kata zipate uwezo wa kitawala kwa sababu ya utekelezaji wenye ufanisi wa nguvu na kazi na ushiriki katika utawala katika ngazi za mashinani.