Io (mwezi)
From Wikipedia, the free encyclopedia
Io ni mmoja wa miezi ya sayari Mshtarii (Jupiter). Kwa ukubwa ni mwezi wa tatu wa sayari hiyo na kipenyo chake ni km 3,642. Hii ni kubwa kidogo kuliko Mwezi wa Dunia yetu.
Io ilitambuliwa mwaka 1609/1610 na Simon Marius na Galileo Galilei wakati hao walipokuwa watu wa kwanza kutumia darubini kuangalia nyota wakaona miezi minne mikubwa zaidi ya Mshtarii. [1] [2]. Marius alipendekeza majina ambayo yamepokewa hadi leo kwa miezi hiyo minne waliyoiona.
Tabia ya pekee ya Io ni idadi kubwa ya volkeno hai zilizotazamwa hadi sasa. Hakuna gimba jingine katika Mfumo wa Jua lenye idadi kubwa hivi.[3][4]
Volkeno hizo zatoa mawingu makubwa ya sulfuri na dioksidi ya sulfuri yanayoenea hadi kimo cha km 500 juu ya uso wa Io. Mwezi huwa pia na milima mirefu, mingine inashinda kimo cha Mlima Everest, ambao ni mlima mrefu kabisa duniani.[5]
Tabia za Io hazikujulikana kwa muda mrefu lakini vipimo na picha zilizopigwa na vipimaanga Voyager 1 na 2, baadaye na "Galileo" iliyopita karibu mara kadhaa, zilileta data kama hizo.
Sawa na mwezi wa Dunia, mzunguko wa Io kwenye mhimili wake unashikamana kabisa na muda wa obiti yake ("tidally locked"); kwa hiyo ni upande uleule unaoangalia sayari yake.
Tofauti na miezi mingine katika Mfumo wa Jua, hakuna kasoko nyingi zinazoonekana; inaaminiwa kwamba vumbi kutoka volkeno linajaza kasoko zinazotokea baada ya kupigwa na asteroidi.