Migoli
From Wikipedia, the free encyclopedia
Remove ads
From Wikipedia, the free encyclopedia
Migoli ni mji mdogo kwenye Wilaya ya Iringa Vijijini katika Mkoa wa Iringa, Tanzania, yenye Postikodi namba 51221. Iko mita 700 juu ya usawa wa bahari.
Unapatikana katikati ya barabara inayounganisha Iringa na Dodoma, kando ya Bwawa la Mtera ambako wakazi wengi hutegemeza maisha yao katika uvuvi.
Eneo hili lina rutuba lakini mvua ni chache (kwa kawaida haifikii mm. 300 kwa mwaka), hivyo wakazi hawajishughulishi sana na kilimo, wananunua nafaka kutoka sehemu ambazo zinalimwa kwa wingi, kama vile Ismani tarafani na Mtamba mkoa wa Dodoma.
Kumbe ni eneo maarufu kwa ufugaji, hasa wa ng'ombe na mbuzi, wanaostawi katika mbuga isiyo na malale.
Eneo hili, ambapo inapita barabara kuu ya Afrika kutoka Kairo (Misri) hadi Cape Town (Afrika Kusini), ni endelevu hasa ukilinganishwa na vijiji vingine vya nchi ya Tanzania, kwa kuwa una huduma nyingi za jamii ambazo zimetokana na juhudi za serikali na wananchi wenyewe.
Wafadhili wa miradi mbalimbali ni kama vile parokia katoliki ya Migoli na makampuni ya mawasiliano kama vile Zain, Tigo, Vodacom na Zantel.
Kijiji asili kilikua sana baada ya serikali kuanza kujenga bwawa la Mtera na kulazimisha watu walioishi bondeni na pembezoni mwa mkondo wa mto Ruaha wasogee ikiwa ni miaka ya 1980. Wazee wa kwanza walioshi katika mitaa miwili ya Migoli na Makonge walikuwa Maulidi Ndilwa, Nyakunga, Simili Magomba, Paulo Magomba, Madekedeke, Kinyaga pamoja na familia zao.
Tangu kuanzishwa kwa Bwawa la Mtera na kijiji cha Migoli, shughuli ya uvuvi ilikikuza sana kijiji cha Migoli ambacho kimekuwa mahali pa biashara yaani watu kutoka makambini (makazi yasiyo rasmi ya uvuvi) walikuwa wakiuzia samaki kwenye kijiji cha Migoli.
Hata hivyo wafanyabiashara wa samaki wamekitumia kijiji cha Migoli kuwa sehemu yao ya kufikia kabla ya kwenda kwenye makambi. Makambi yanayokitegemea kijiji cha Migoli ni Nyegere, Mabati, Maperamengi, Mandela, Kilambakitali, Changalawe na mengine mengi.
Hatimaye kijiji kimemegwa na kuzaa kijiji kipya cha Mtera upande wa kaskazini.
Katika sensa iliyofanyika mwaka 2022 wakazi walihesabika kuwa 15,139 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ya Migoli ilikuwa na wakazi wapatao 10,937 waishio humo.[2]
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.