From Wikipedia, the free encyclopedia
Historia ya Eritrea inahusu eneo la Afrika Mashariki ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Eritrea.
Hadi karne ya 19 maeneo ya Eritrea yalikuwa sehemu ya Ethiopia.
Pwani ilikaa karne nyingi chini ya utawala wa Uturuki au baadaye Misri kama nchi zenye nguvu kwenye Bahari ya Shamu.
Historia ya Eritrea kama eneo la pekee jinsi ilivyopata uhuru mwisho wa karne ya 20 ilianza na ukoloni wa Italia.
Mnamo Novemba 1869 kampuni ya biashara ya Kiitalia ya Rubattino ilinunua bandari ya Assab kutoka kwa sultani wa Afar. Ilikuwa inatafuta kituo kwa meli zake zilizoanza kupita katika bahari ya Shamu baada ya kufunguliwa kwa Mfereji wa Suez mwaka uleule.
Serikali ya Misri ilipinga mapatano hayo kwa sababu ilidai eneo lilikuwa chini ya amri yake. Makubaliano hayakufikiwa hadi 1882, serikali ya Italia ilipochukua moja kwa moja mali ya kampuni kama koloni lake la kwanza katika Afrika.
Tangu kuporomoka kwa utawala wa Misri nchini Sudan, baada ya vita vya Al-Mahdi, Misri ilijiondoa pia katika pwani ya kusini mwa bahari ya Shamu. Italia ilitumia nafasi hiyo na tarehe 5 Februari 1885 ilipeleka wanajeshi mjini Massawa na kuitangaza kuwa koloni lake.
Waitalia waliendelea kuunganisha maeneo yao ya Assab na Massawa. Baadaye walijaribu kupanua utawala wao kutoka tambarare za pwani hadi nyanda za juu zilizokuwa chini ya Dola la Ethiopia.
Negus Yohanne IV hakufurahia kufika kwa Italia kwa sababu aliamini ya kwamba Massawa iliahidiwa kwake baada ya kuwasaidia Wamisri kujiokoa mbele ya jeshi la Al-Mahdi. Hivyo upanuzi wa Italia katika nyanda za juu ulikutana na upinzani.
Tarehe 26 Januari 1887 jeshi la Waitalia 587 walioelekea kaskazini lilishambuliwa karibu na Massawa kwenye kijiji cha Dogali na kushindwa na Ras Alula aliyekuwa mtemi chini ya Negus ya Ethiopia. Waitalia walipaswa kuongeza wanajeshi 13,000 ili kuhakikisha utawala wao.
Baada ya Yohanne IV kufariki katika mapigano na jeshi la Al-Mahdi, Waitalia walichukua nafasi hiyo ya kuziingia nyanda za juu za Tigray na kujenga vituo vyao huko.
Mfalme mpya Menelik II tarehe 2 Mei 1889 aliutia sahihi mkataba wa Wuchale uliokubali utawala wa Italia juu ya kanda ya pwani pamoja na maeneo kadhaa ya nyanda za juu za Tigray.
Waitalia walijaribu kumdanganya Negus katika mkataba huo kwa kuingiza maneno katika nakala ya Kiitalia yaliyosema "Ethiopia itakuwa chini ya ulinzi wa Italia". Menelik baada ya kuelewa haya alikana mkataba.
Italia ilijibu kwa kuvamia Ethiopia kwa jeshi kubwa. Jeshi hilo lilishindwa na Waethiopia katika mapigano ya Adowa tarehe 1 Machi 1896. Italia ilipaswa kukubali uhuru wa Ethiopia katika mkataba wa amani tarehe 26 Oktoba 1896. Ethiopia ilikubali mamlaka ya Italia juu ya koloni lake katika kaskazini.
Baada ya kumaliza mashindano na Ethiopia, Italia tarehe 1 Januari 1890 iliunganisha maeneo yake yote katika koloni lililoitwa Eritrea kufuatana na jina la kale "Bahari ya Eritrea".
Katika kipindi hiki cha utawala wa kikoloni Eritrea ilitokea kama jamii na eneo la pekee. Koloni la Eritrea liliunganisha maeneo matatu yenye tabia za pekee:
Italia ilianzisha miradi ya kufanya Eritrea chanzo cha malighafi kwa ajili ya uchumi wa Italia. Kijiji cha Asmara katika nyanda za juu kilikuwa mji mkuu wa koloni na kupanuliwa kuwa mji kwa ajili ya walowezi Waitalia. Asmara ilipambwa na majengo mazuri ya kisasa.
Katika miaka ya 1930 idadi ya motokaa zilizoendeshwa Asmara ilishinda idadi ya magari ya binafsi mjini Roma. Urithi huo wa majengo umekuwa sababu ya kuingiza Asmara katika orodha ya Urithi wa dunia ya UNESCO.
Waitalia walipanga na kujenga miji mingine kama vitovu vya biashara, mabandari, vituo vya kijeshi au vya kiuchumi.
Idadi ya wakazi wote ilikadiriwa kuwa takriban 200,000 mwaka 1890. Idadi hiyo iliongezeka haraka kufikia zaidi ya 600,000 mnamo 1939. Mabadiliko makubwa yalitokea hasa katika nyanda za juu ambako walowezi Waitalia walianzisha mashamba yao na miji mikubwa zaidi ilijengwa.
Idadi ya wasemaji wa Kitigrinya iliongezeka kutoka asilimia 35 mwaka 1905 kuwa asilimia 54 mwaka 1939.
Mwisho wa vita kati ya vikundi mbalimbali na kupatikana kwa huduma za kiafya pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa chakula, vyote vilichangia katika kuongezeka kwa idadi ya watu.
Kati ya mabadiliko makubwa ulikuwa ujenzi wa barabara na reli kati ya Massawa, Asmara, Keren na Agordat. Viwanda kadhaa vilianzishwa, pia migodi ya kuchimba mawe au madini.
Sehemu za Waeritrea waliingia katika maisha ya ajira ya kibepari. Hivyo maarifa ya wakazi wa Eritrea hasa katika nyanda za juu yalikuwa tofauti na wenzao katika Ethiopia yenyewe walioendelea kuishi chini ya utaratibu wa kikabaila. Waeritrea walisukumwa katika maisha ya kisasa na uchumi wa fedha.
Hadi mwaka 1940 Eritrea ilikuwa tayari na tabaka la wafanyakazi wa viwandani na katika miji pia tabaka la wasomi wenye elimu ya kisasa.
Baada ya Mussolini kushika serikali, siasa ya Italia ilibadilika. Wafashisti walidharau Waafrika na kuanzisha siasa ya ubaguzi wa rangi. Wenyeji walipewa tu shughuli duni kabisa katika utumishi wa serikali.
Italia ya kifashisti ilifanya mipango ya kulipizia kisasi mapigano ya Adowa ikiandaa vita dhidi ya Ethiopia. Vita vilianza mwaka 1935 kutoka ardhi ya Eritrea. Silaha mpya za Italia (zikiwemo za kikemikali) zilishinda jeshi la Negus, hivyo Ethiopia yote ikawa koloni la Italia kwa miaka michache.
Waitalia walishindwa katika Vita Vikuu vya Pili mwaka 1941, ambapo Waingereza waliteka Ethiopia pamoja na Eritrea.
Waingereza walitawala Eritrea hadi 1952.
Mwaka huo Umoja wa Mataifa ulikabidhi Eritrea kwa Ethiopia kama eneo la pekee lenye serikali na bunge lake katika shirikisho.
Mfalme wa Ethiopia, Haile Selassie hakupendezwa na utaratibu huoː alilenga kuunganisha tena Eritrea na Ethiopia na kwa mbinu mbalimbali alipata kura ya bunge la Eritrea ya kujivunja na kuwa jimbo la Ethiopia (1962).
Baada ya tukio hilo vikundi vya wanamgambo walienda porini kupigania kwa silaha uhuru wa Eritrea.
Vita vya Uhuru wa Eritrea vilitambakaa mwaka 1974 baada ya ufalme kupinduliwa na Umakisti kuingia na rundo la Jeshi lililoitwa Derg kuchukuwa mamlaka, na baadaye kuvamia Eritrea. Ukorofi wa serikali ya Mengistu Haile Mariam ilifanya mengi kuongeza waliotumaini uhuru wa Eritrea katika miaka ya 1980.
Ukombozi wa Eritrea ulitegemea rundo la Eritrean Liberation Front (ELF), ambayo pia inaitwa "Jebha", na Eritrean People's Liberation Front (EPLF), ambaye pia inaitwa "Shaabia". ELF ilikuwa na Waislamu wengi wa pwani na wahifadhi wa tedo za wananchi, na EPLF wengi Wakristo kutoka nyanda za juu za Tigrayi waamini Makisti-ULenin. ELF ilisaidiwa na wafadhili Waarabu, na EPLF kutoka nchi za kikomunisti zilizokuwa upande wa Urusi, lakini badaye nchi hizo zikapinduka na kusaidia Derg ya Mengistu Haile Mariam. ELF na EPLF hazikuweza kufanya kazi pamoja na kwa hiyo EPLF ikaimaliza ELF na kuendelea kutafuta uhuru.
Vita vya uhuru viliisha mwaka 1991, Waeritrea na waasi Waethiopia kutoka Tigray walishinda jeshi la Ethiopia na kuteka Addis Ababa; serikali ya Derg ikaanguka miaka miwili baadaye.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.