Njozi za Bikira Maria
From Wikipedia, the free encyclopedia
Njozi za Bikira Maria ni maono ya Bikira Maria yaliyoripotiwa na watu mbalimbali, hasa Wakristo wa madhehebu mbalimbali, kwamba yamewapata nje ya ndoto, na kwamba walimuona akiwa yuko sehemu fulani, na si kusikia tu sauti yake [1].
Njozi zinaweza zikawa za kweli au siyo. Mtu anaweza akadanganya kwa makusudi, anaweza akadanganyika mwenyewe katika inavyofafanuliwa na saikolojia kwa nafasi mbalimbali[2], lakini kwa wenye imani ya dini ni jambo ambalo linawezekana kutokea kweli[3].
Kwao Bikira Maria kutokea watu ni uthibitisho wa uwajibikaji wake kama mama wa Kanisa na wa waumini wake. Anaweza kuwatokea kuitikia maombi yao, kuahidi msaada wake[4] , kufariji au kuonya, akikumbusha kweli za imani na maadili yanayotakiwa n.k.[5]
Kanisa Katoliki lina taratibu zake katika kutathmini ukweli wa njozi hizo; kati ya vigezo vinavyotumika kuna unyofu na uadilifu wa wanaodai kutokewa, usahihi wa imani wa ujumbe wanaosimulia wamepewa, matunda mazuri yanayofuata [6].
Pamoja na kwamba Kanisa hilo limekataa njiozi nyingi[7], hata likithibisha ukweli wa njozi fulani, hakuna anayelazimika kuiamini kwa sababu ni mafunuo binafsi tu[8][9], ambayo ni tofauti na ufunuo rasmi uliokamilika wakati wa Mitume wa Yesu.
Njozi kadhaa za Bikira Maria zimeathiri sana maisha ya watu, kama ile ya Bikira Maria wa Guadalupe huko Mexico ambayo iliwavuta wakazi asili kukubali ubatizo kwa mamilioni na ni sehemu ya utambulisho wa taifa.
Mara nyingi njozi zinasababisha ujenzi wa patakatifu panapokuwa mahali pa hija kwa wengi, karne hata karne[10][11][12], lakini pia uanzishwaji wa mashirika ya kitawa, vyama vya kitume, sala mpya n.k.