Utiifu, katika maisha ya binadamu, ni aina ya "mwenendo ambayo mtu anafuata maelekezo au maagizo ya wazi aliyopewa na mwenye mamlaka".[1]
Ni tofauti na mtu kufuata athari ya wenzake au mkondo wa umati.
Kimaadili utiifu unaweza kutazamwa kwa namna mbalimbali, chanya au hasi, hasa kulingana na uadilifu au uovu wa agizo lenyewe, kwa mfano lile la Hitler kuhusu mauaji ya kimbari ya Wayahudi.[2]
Katika jamii
Utamaduni wa nchi nyingi unatazama utiifu kama adili; hasa jamii kwa kawaida inadai watoto waheshimu na kutii wazazi wao na wazee wengine, lakini pengine watumishi na watumwa walidaiwa kutii mabwana wao, na watu wa rangi fulani kutii wale wa rangi nyingine.
Mbali ya hayo, wananchi wanatarajiwa kutii watawala halali, na wanadini kumtii Mungu.
Katika dini
Utiifu ni muhimu katika dini mbalimbali. Hasa Uislamu unaufanya kiini cha imani (neno Islam linamaanisha "kukubali, kusalimu amri").[3]
Katika Ukristo, ni hasa watawa wanaowajibika kuishi kwa utiifu katika jumuia zao ili kutimiza kwa umoja mapenzi ya Mungu.
Mbali ya hao, kielelezo cha Wakristo wote ni Yesu Kristo, aliyesifiwa kwa kumtii Mungu Baba hata kufa - kufa msalabani (Fil 2:1-18).
Kwa Kigiriki, lugha ya Agano Jipya, utiifu ni sawa na usikivu (wa Neno la Mungu), hivyo Mtume Paulo alisisitiza utiifu wa imani.
Utawani
Lililo kuu kati ya mashauri ya Kiinjili ni utiifu, kama vile kiburi cha maisha kilivyo vurugu kubwa kuliko tamaa za mwili na macho (1Yoh 2:16). Ndiyo sababu Yesu aliwaambia wenye kiburi, “Amin, nawaambia, watoza ushuru na makahaba watatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohane alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini, lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini. Nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini” (Math 21:31-32). Hayo tunayajua kinadharia, lakini tunayasahau kwa urahisi katika utekelezaji. Tunazingatia vurugu za wazi zinazotokana na tamaa za mwili na macho, tusitambue kuwa kosa kuu ni lile la kusema, “Sitatumikia”. Ndilo dhambi hasa la ulimwengu “wa kisasa” unapodai kujitenga na Kanisa ili ufuate tu akili na utashi wake wenyewe: matokeo yake, unakwenda kinyume cha akili mradi usimtii Mwenyezi Mungu. Hatimaye, kama mwana mpotevu, unajikuta katika utumishi wa kuudhalilisha ambao unasambaratisha na kuangamiza jamii.
Ugonjwa wa namna hiyo unaponyeka tu kwa kushika utiifu mnyenyekevu na wa dhati; lakini mara nyingi ukuu wa utiifu haujulikani hata katika mazingira mema. Inasahaulika kuwa nadhiri za kitawa zinainua kwa ndani maisha yote yaliyowekwa wakfu. Katika vitabu vingi nadhiri za ufukara wa hiari na useja zinashika nafasi kubwa, kwa sababu kuzivunja kunatokea mara nyingi na kuzidisha dhambi hata za mauti. Kumbe utiifu unawekwa pembeni kwa sababu kwa nadra tu kuuvunja ni dhambi ya mauti. Inasahaulika thamani ya kujitoa mhanga kwa nadhiri; unasahaulika pia mpango mzima wa maisha ya kitawa kuwekwa wakfu kwa njia ya maadili ya ibada na utiifu. Hivyo kwa wengi utiifu ni nidhamu tu, utekelezaji wa nje unaodaiwa na kazi na ambao sanasana unaweza kuinuliwa kama vitendo vingine vyovyote. Ili tuthamini kwa dhati adili hilo, tutazingatia linatukomboa kutoka utumwa upi na linazaa matunda yapi.
Utumwa ambao utiifu unatukomboa nao
Kwanza ni kwamba utiifu unatukomboa kutoka utumwa wa matakwa yetu na wa maoni yetu.
Utiifu kwa Mungu na kwa wawakilishi wake (wa Kiroho na wa kidunia) unatuhakikishia ulinganifu wa matakwa yetu na yale ya Mungu. Sababu hasa ya kutii si kwamba agizo linaonekana la kufaa, bali kwamba limetolewa na kiongozi halali anayemwakilisha Mungu, asili ya mamlaka yote. Tukitii kwa sababu ya kuridhika tu na agizo, tunakosa stahili maalumu za utiifu (kama tunavyokosa zile za imani tukikubali kweli zile tu zilizo wazi, wakati sababu halisi ya kusadiki ni mamlaka ya Mungu anayetufunulia mafumbo). “Tunalotakiwa kutii ni agizo linaloonyesha matakwa ya kiongozi, liwe limetolewa wazi au la” (Thoma wa Akwino). Hivyo utiifu unatukomboa kutoka matakwa yetu, yaani matakwa ambayo hayalingani na yale ya Mungu, bali kwa kiburi yamepotea yakikataa kutenda inavyotakiwa.
Kwa maana hiyo matakwa yetu ndiyo sababu ya dhambi yoyote: “mkiondoa matakwa yetu hautakuwepo tena moto wa milele” (Bernardo wa Clairvaux). Ni ya hatari hasa kwa kuwa yanaweza kuharibu kila kitu. Hata matendo bora yanakuwa maovu yakifuata matakwa yetu badala ya kumtii Mungu. Bwana akiona matakwa yetu yanasababisha tendo la toba au la ibada analikataa kama yale ya Mafarisayo. Hata tusipofikia hapo, huwa tunashikilia matakwa yetu, tukijali pengine namna yetu ya kutenda jema kuliko jema lenyewe: tunataka kulitenda sisi, la sivyo tunazuia lisitendwe.
Utiifu unatakiwa kutekelezwa kwa imani, kwa kuona agizo la viongozi ni agizo la Mungu. Unapaswa kuwa wa mara moja, kuhusu jambo lolote (dogo au kubwa) na kwa viongozi halali wote (wawe wapendevu au la, wenye busara au la, watakatifu au la) mradi agizo lao halipingani na sheria ya juu. Utiifu huo unakomboa kwa sababu siku kwa siku unalinganisha matakwa yetu na yale ya Mungu na hivyo unanyosha na kuimarisha utashi wetu.
Utiifu unatukomboa pia kutoka utumwa wa maoni yetu yasiyo na msingi katika ukweli, yaani katika mtazamo wa Mungu. Maoni hayo yanasababisha mienendo ya pekee na ugumu wa vichwa katika utendaji. Ni maoni ya harakaharaka yatokanayo na maelekeo mabaya, umimi na kiburi. Pengine yananong’onezwa au kuthibitishwa na adui wa roho yetu. “Kadiri mtu alivyo anaona lengo fulani kuwa linamfaa” (Aristotle), yaani tunaona jambo kuwa jema au baya kadiri ya maelekeo ya matakwa na ya hisi zetu. Mwenye kiburi anayaona bora yale yanayomkuza, kumbe mnyenyekevu anaona kudhalilishwa kunamfaa zaidi. Mara nyingi maoni yetu yanatufikisha hata kuhukumu kinyume cha haki na upendo.
Huo ni utumwa halisi: utiifu unatukomboa ukihakikisha kwamba katika utendaji tunakubali maoni ya wakili wa Mungu aliye na haki ya kutuagiza kwa niaba yake. Agizo lenyewe linaweza likakosa busara: hapo hatudaiwi kulikubali kinadharia (labda siku za mbele kiongozi mwingine ataona tofauti), bali kuzingatia tu kwamba limetolewa kwetu rasmi, hapa na sasa na Mungu. Hata kama kiongozi anadanganyika, sisi tukimtii hatudanganyiki kiutendaji. Mjumbe wa maongozi ya Mungu anaweza akawa mlemavu, hata hivyo anatuletea agizo kutoka juu.
Utekelezaji wa shauri la utiifu unapatikana hasa utawani unapohakikisha ufishaji wa matakwa yetu: kwa hiyo ni njia ya kufikia Ukamilifu wa Kikristo mapema, kwa kuzidi kulingana na matakwa ya Mungu mpaka ndani katika vipengele vyote vya maisha ya kila siku. Lakini, ili tuufikie ukamilifu huo, walau tunapaswa kuwa na roho ya shauri hilo, yaani kutoambatana na matakwa yetu. Kama vile mtoto anavyopaswa kuwatii wazazi na walezi, kila Mkristo anapaswa kuwatii wale wote wanaomwakilisha Mungu kwake upande wa roho au wa jamii. Utiifu huo ukitekelezwa kwa imani (si kwa nje, kimwili na kwa hofu tu) unaunda utashi vizuri ajabu kwa kuufanya zaidi na zaidi uwe tayari na imara chini ya ule wa Mungu. Tukumbuke mara nyingi kwamba “hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imeamriwa na Mungu” (Rom 13:1); hivyo tunachofanya si kumtii mwenzetu, bali mkubwa wetu na kwa njia yake kumtii Mungu.
Ni lazima tujifunze kuyatii matukio pia kadiri yanavyotuonyesha matakwa ya Mungu kwa kuwa hapana lolote pasipo yeye kulitaka (likiwa jema) au kuacha litokee (likiwa baya). Ili utiifu uwe kamili unatakiwa kuzingatia hata ishara hizo za matakwa ya Mungu. Kwa mfano, kufaulu vizuri na kwa haki mtihani fulani kunatuwezesha kutenda mema zaidi; ni juu yetu kutoiharibu nafasi hiyo. Kinyume chake, tukishindwa au kuugua, pengine tunaonyeshwa kuwa njia tuliyoshika si ile aliyotupangia Mungu.
Kuna matukio ambayo yana maana ya pekee na kubadili hali ya familia au muundo wa jamii. Tunapaswa kufaidika nayo kadiri iwezekanavyo, badala ya kudai irudi hali iliyofaa wakati mwingine, lakini haitakiwi tena na Mungu. Hatuwezi kurudi nyuma katika maisha yetu wala katika historia; mzee hawezi kurudia ujana, wala karne yetu haiwezi kuirudia ile ya 13, ingawa inatakiwa kufaidika na mema yote ya karne za nyuma ili iandae za kesho zitawaliwe na Mungu.
Katika namna hizo zote za kuyatii yanayodhihirisha matakwa ya Mungu, yaani utiifu wa kutimiza wajibu wa sasa hivi, tuzingatie kielelezo cha Mwokozi aliyekuwa “mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba” (Fil 2:8). Ndivyo watakatifu wote walivyofurahi kuyafia matakwa yao ili kujilisha yale ya Mungu yaliyodhihirishwa na amri, mashauri na matukio.
Matunda ya utiifu
Tunda la kwanza ni unyofu mkubwa wa uamuzi unaotokana na kwamba utiifu unatushirikisha hekima ya Mungu: “Ninao ufahamu kuliko wazee, kwa kuwa nimeyashika mausia yako” (Zab 119:100). Katika nafasi ngumu, utiifu unatupa jawabu la hakika kiutendaji kwetu, sasa na hapa. Kama tuzo la uaminifu wake, utiifu kamili unapata mianga ya kipaji cha shauri inayotuongoza katika mambo ya Kiroho ambayo kiongozi huenda akashindwa kuyavumbua, na ambayo busara yetu haifikii kuyaeleza ipasavyo. Kipaji hicho kinahitajiwa hasa na wale wanaotakiwa kutoa amri, ili wasifanye hivyo kibinadamu tu; ndiyo sababu tusipotii vizuri kwanza, hatutaweza kamwe kuagiza inavyotakiwa.
Kinyume cha mtazamo wa wengi, utiifu unazidisha pia nguvu za utashi. Mtu asipotia shaka kuwa amri fulani imetoka kwa Mungu kumpitia kiongozi halali, ana hakika kwamba inaweza kutekelezwa kwa neema yake. Augustino alisema, “Mungu haagizi kamwe yasiyowezekana, bali anapotuagiza anatuambia tuyafanye tunayoyaweza na tumuombe neema ya kufanya tusiyoyaweza”. Ndiyo maana alikuwa akiomba, “Bwana, nipe unayoniagiza, halafu uniagize yoyote unayotaka”. Ndiyo sababu tukipaswa kufia dini, Mungu anatujalia uaminifu katika mateso, hata tukiwa watoto, wanawali au wakongwe. Utiifu unatenda miujiza nje ya nafasi hiyo pia. Tunapopewa amri kutoka kwa Mungu, tunapewa neema ya kuweza kuitekeleza, na tukisali ili tuwe waaminifu tutaitekeleza kwa hakika, ingawa kwa tabu.
Hatimaye utiifu, badala ya kuwa aina ya utumwa, unatia uhuru mkubwa wa wana wa Mungu, kama vile ufukara wa hiari unavyotia utajiri wa kweli, na vile useja mtakatifu unavyotia upendo wa dhati. “Alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru” (2Kor 3:17), kwa sababu ukweli wa Kimungu unakomboa kutoka udanganyifu. Basi, utiifu unaotia ukweli maishani, unakomboa kutoka dhana zisizo na msingi za ulimwengu, misimamo, mitindo na maelekeo yake; unakomboa kutoka mahangaiko kuhusu kuhukumiwa na watu (“watasemaje?”): tenda mema na kuacha waseme; utiifu unakomboa kutoka shaka, wasiwasi na mafadhaiko. Unayafanya maisha yawe sahili zaidi kwa kuyainua. Uhuru unaongezeka, kwa sababu unatokana na mwanga: kadiri tunavyoelewa kuwa Mungu ndiye wema mkuu, tuko huru tusifuate mivuto ya malimwengu, na tuko imara dhidi ya vitisho vya waovu. Nani aliwahi kuwa huru kuliko wafiadini ambao kwa upendo na utiifu walitoa damu yao, hata upanga na moto havikuweza kuwafanya waasi?
Ukuu wa utiifu unadokezwa na maneno yafuatayo: Kumtumikia Mungu ni kutawala. Ni kutawala maono yetu, roho ya ulimwengu, adui wa watu na vishawishi vyake; ni kuingia katika utawala wa Mungu na kushiriki uhuru wake kuhusu viumbe vyote; ni kujitia mikononi mwake kama chombo kilicho tayari kufanya chochote atakachotaka. Hakika utiifu unatuandaa kuzama katika mafumbo ya Mungu, kuona matakwa yake katika matukio yoyote (ya kupendeza na ya tabu), na kuelewa “ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema” (Rom 8:28).
Tanbihi
Viungo vya nje
Wikiwand in your browser!
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.