Redio

From Wikipedia, the free encyclopedia

Redio

Redio (au rungoya) ni njia ya mawasiliano ambayo hutumia mawimbi ya umeme kurusha sauti na habari kupitia nafasi ya bure. Katika muktadha wa elektroniki, redio inahusisha vifaa kama vile redio za FM, AM, au vifaa vya redio vya dijitali ambavyo hupokea, kusindika, na kusikiliza mawimbi ya redio yaliyorushwa na vituo vya redio. Redio inatumika sana kwa burudani, habari, mawasiliano ya dharura, na matumizi ya kibiashara. Teknolojia ya redio inahusisha mifumo ya kupeleka na kupokea mawimbi ya redio, ikiwa ni pamoja na antena, vipokezi, vifaa vya usindikaji wa sauti, na maudhui ya redio. Redio imekuwa moja ya njia muhimu za mawasiliano ulimwenguni kote kwa miongo kadhaa.

Thumb
Redio mnamo 1950.
Thumb
Redio mnamo 2000.

Historia

Mwaka 1886 Mjerumani Heinrich Hertz alitambua mawimbi ya sumakuumeme. Wataalamu na muhandisi mbalimbali walifanya majaribio katika miaka iliyofuata kutumia mawimbi haya kwa mawasiliano, kati yao Mwitalia Guglielmo Marconi, Mmarekani Nikola Tesla na Mrusi Alexander Popov. Kila mmoja ametajwa kama "mtu wa kwanza aliyegundua rungoya".

Kituo cha kwanza cha rungoya kilianzishwa na Mholanzi Hanso Schotanus à Steringa Idzerda tarehe 6 Novemba 1919 aliposambaza muziki kutoka nyumba yake. Kituo cha kwanza cha kibiashara kilianza kazi mwaka 1920 Marekani mjini Pittsburgh.

Katika miaka iliyofuata redio ilisambaa kote duniani. Ni njia muhimu ya kusambaza habari pamoja na utamaduni, hasa muziki.

Matumizi ya redio

Thumb

Hapo zamani, redio zilitumika na mabaharia kwa kutuma jumbe toka chombo majini hadi nchi kavu kwa kutumia kodi za Morsi (Morse code). Wakati chombo kilichojulikana kama Titanic kilikuwa kinazama mwaka 1912, jumbe zilitumwa kutoka kwa mabaharia waliokuwa kwenye chombo hicho kwa vyombo vilivyokuwa karibu.

Wanajeshi pia walitumia redio kutuma jumbe na kuwasiliana na makao yao makuu.

Leo, redio hutumika kwa mawasiliano, matangazo na muziki. Kabla ya uvumbuzi wa televisheni, redio zilitumika kwa uigizaji na vichekesho. Redio za leo zinatumia wavu za dijitali na huweza kushika wavu kwa urahisi zaidi.

Pia kuna redio za kushikwa kwa mikono.

Maendeleo ya Redio nchini Tanzania

Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki inayokua kwa kasi katika teknolojia ya mawasiliano na uchumi pamoja na Uganda na Kenya. Unapozungumzia teknolojia ya mawasiliano ina upana wake lakini hapa tutaegemea katika redio.

Tanzania imegawanyika katika mikoa, wilaya, kata, vijiji, vitongoji na mitaa. Hivyo katika ukuaji wa mawasiliano ya tasnia ya habari, redio imekuwa ikiaminiwa zaidi kwa utoaji wake wa taarifa kwa haraka ikifuatiwa na magazeti na runinga (televisheni).

Redio nchini hapa zimekuwa zikiongezeka kwa kadri mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanavyokuwa na sera mbalimbali za nchi katika uhuru wa utoaji wa habari.

Pia zinaongezeka kutokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibara ya 18 kutoa uhuru wa kila raia kutoa mawazo yako. Katika Katiba ya mwaka 1977 kifungu kidogo cha kwanza (1) na cha pili (2): "(1) Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati. (2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.”

Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ndiyo redio ya kwanza ya taifa hilo, ambayo sasa inajulikana kama TBC (Tanzania Broadcasting Coorporation) baada ya kufanyiwa mabadiliko kadhaa. Ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1970.

Kuna redio binafsi kubwa zinazosikika nchi nzima katika mikoa takribani thelathini (30), kama vile Radio Free Africa (RFA), Kiss FM, Radio One Stereo na Clouds FM.

Kuanguka kwa Umoja wa Kisoshalisti wa Kisovyeti (USSR) mwishoni mwa miaka ya 1990, uliokuwa ukiabudu ujamaa, kulifanya mabadiliko makubwa ya maisha kwa Watanzania baada ya dola la Moscow kuanguka utamaduni wake hivyo kuupa nafasi utamaduni wa Kimagharibi kuchukua nafasi yake.

Redio zilizo nyingi zimepata kuinuka zaidi mwanzoni mwa karne ya 21 na rika la vijana likichukua hatamu katika kuongoza vipindi mbalimbali katika redio hizo.

Hilo tu halitoshi kusema teknolojia pekee imezifanya kusikika nchi nzima bali uwepo wa sera mahsusi za kibiashara ndizo zimekuwa chachu ya kukua kwa redio hizo.

Aidha redio nyingine zinasikika katika kanda fulani tu, au mkoa au wilaya husika; kutokana na kutokuwa na uwezo wa kiuchumi kufika mbali kama nyingine.

Hata hivyo redio za mikoani na wilayani zimekuwa zikitoa changamoto kubwa kwa zinazosikika nchi nzima.

Mkoa mmoja unaweza kuwa na redio zisizopungua mbili, hivyo unaweza kuona ni kwa kiasi gani redio za nchi nzima zinavyopata changamoto katika matangazo yake. Kwa mfano, mkoa wa Mbeya (Nyanda za Juu za Kusini) una redio kama vile Mbeya FM, Bomba FM, Generation, Southern Highlands, Rock FM, Baraka FM na Ushindi FM.

Mkoa wa Dar es Salaam ambao unasifika kwa umahiri wake wa kibiashara ndio wenye redio nyingine kubwa na ndogo zikiwamo TBC Taifa, TBC FM, Radio One Stereo, Capital Radio, E-FM, Clouds FM na City FM.

Pia hata zilizoko nje ya mkoa wa Dar es Salaam zinapambana kila kukicha kuhakikisha zinakuwa na studio nyingine kwenye jiji hilo lenye idadi kubwa ya watu nchini Tanzania. Kwa mfano RFA na Kiss FM zinarusha matangazo yake kutoka jijini Mwanza (Kanda ya Ziwa Viktoria), lakini kutokana na ushindani uliopo zimejikuta zikiweka studio nyingine jijini Dar es Salaam ili kupambana na ushindani huo.

Kwa upande mwingine ushindani unatoka kwa wanaofanya kazi ambao ni watangazaji, ambao kila mmoja anatafuta namna ya kupata wasikilizaji wa vipindi vyake.

Tanbihi

Wikiwand in your browser!

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.

Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.

Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.