Epidemiki (kutoka Kiingereza epidemic, kiasili ni Kigiriki; pia: epidemia, magonjwa ya mlipuko, mlipuko wa magonjwa) hutokea wakati maambukizi ya ugonjwa fulani yanaenea haraka na kuathiri watu wengi kwa muda mfupi katika eneo fulani.

Thumb
Maendeleo ya epidemiki ya Ebola katika Afrika ya Magharibi katika kipindi cha 2014/15 (mabadiliko kwa wiki)

Kwa mfano, kama maambukizi kutokana na bakteria ya meningococcus (yanayosababisha meninjitisi, yaani ugonjwa wa uti wa mgongo) yanazidi watu 15 kati ya 100,000 katika kipindi cha wiki 2, hali hutazamwa kuwa epidemiki.[1]

Epidemiki inayozidi kuenea na kuathiri nchi mbalimbali, hata Dunia nzima, huitwa pandemia.

Katika kulinda watu dhidi ya kuibuka kwa milipuko mipya, hatua kadhaa mwafaka zimependekezwa na Shirika la Afya Duniani [2]

Magonjwa endemiki

Kama magonjwa ya kawaida yanatokea mara kwa mara lakini kwa kiwango duni kulingana na idadi ya watu, huitwa "endemiki (endemic)." Mfano wa ugonjwa wa endemiki ni malaria katika baadhi ya maeneo ya Afrika (kwa mfano, Liberia) ambapo sehemu kubwa ya wakazi wanatabiriwa kupata malaria wakati fulani katika maisha yao).

Sababu za kutokea kwa epidemiki

Thumb
Tauni ya Athini (1652–1654 hivi), picha ya Michiel Sweerts ambapo msanii aliwaza hali ya epidemiki ya tauni mjini Athens mwaka 432 KK, jinsi ilivyoelezwa na mwanahistoria Thucydides.

Kuna mabadiliko mbalimbali yanayoweza kuchangia epidemiki itokee. Haya ni pamoja na:

  • Kuongezeka kwa ukali au uwezo wa vimelea wa kuleta ugonjwa (increased virulence, mfano kutokea kwa virusi vipya ambavyo watu hawana kinga nayo bado)
  • Kufika kwa virusi au bakteria katika mazingira mapya ("novel setting", mfano kufika kwa virusi vya mafua pamoja na Wazungu wa kwanza huko Amerika kulisababisha vifo vya mamilioni ya wenyeji Waindio ambao hawakujua mafua bado)
  • Mabadiliko katika uathirikaji wa watu (host susceptibility) kwa vimelea, yaani virusi au bakteria (mfano: kama nchi ilikuwa na kipindi cha njaa, wananchi hudhoofika, na kufika kwa virusi vipya kunaweza kusababisha wengi kuwa wagonjwa hadi kufa; mfano ni epidemiki ya mafua kwenye mwisho wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia katika Tanganyika, ambako wengi walikufa kwa sababu walikosa nguvu ya kinga mwilini baada ya miaka ya njaa iliyosababishwa na vita nchini).

Sababu za kutokea kwa epidemiki ni pamoja na kupatikana kwa maji yasiyo safi (yenye vimelea ndani yake) na uhamiaji wa wanyama kama panya au mbu wanaoweza kubeba vimelea viambukizi. Mfano ni tauni (plague) iliyoua mamilioni katika karne za kati huko Ulaya. Inasababishwa na bakteria wa yersinia pestis waliopo katika utumbo wa viroboto wanaoshi kwenye panya. Usambazaji wa panya hao kupitia jahazi za mizigo kwenye bahari ya Mediteranea ulileta ugonjwa huu kutoka Asia hadi Ulaya.

Epidemiki huweza kutokea pia kufuatana na majira; katika nchi za kaskazini hutokea kila baada ya miaka kadhaa homa ya mafua kwa sababu katika vipindi vya baridi uathirikaji wa watu wengi unaongezeka, hasa kama aina mpya ya virusi inasambaa.

Kwa ufafanuzi wa WHO si lazima epidemiki ihusu ugonjwa wa kuambukiza, imetumiwa pia kwa kutaja kuenea kwa unene wa kupindukia[3])

Hali zinazochochea milipuko

Hali ambazo zimeelezwa na Marko Woolhouse na Sonya Gowtage-Sequeria zinazochochea kuongezeka kwa milipuko [4] ni pamoja na:

  1. Mabadiliko katika kilimo na matumizi ya ardhi
  2. Mabadiliko katika jamii na demografia ya binadamu
  3. Afya ya watu maskini (mfano, utapiamlo, maambukizi ya kiwango cha juu ya HIV)
  4. Hospitali na taratibu za matibabu
  5. Kubadilika kwa viini vya magonjwa (mfano, kuongezeka kwa virulence, kutoaThiriwa na dawa)
  6. Kuchafuliwa kwa vyanzo vya maji na vya chakula
  7. Usafiri wa kimataifa
  8. Kutofaulu kwa mipango ya afya ya umma
  9. Biashara ya kimataifa
  10. Mabadiliko ya hali ya hewa

Sababu nyingine kadhaa zimetajwa pia katika taarifa mbalimbali, kama vile ripoti ya profesa Andy Dobson [5] na ripoti ya profesa Akilesh Mishra [6]Hizi ni pamoja na:

  1. Kupunguka kwa ngazi za viumbe hai (kwa mfano kupitia uharibifu wa mazingira)
  2. Mipango duni ya miji

Mifano

  1. Epidemiki za tauni zinaaminiwa kuwa milipuko ya ugonjwa iliyoua watu wengi zaidi; ikifahamika kama "black death" (kifo cheusi) iliangamiza theluthi moja ya wakazi wa Ulaya katika karne ya 14.[7]
  2. Mlipuko wa homa ya mafua wa 1918 (influenza A/H1N1) ulienea katika miaka 1918-1920, maarufu kama "Spanish Flu", iliyoua watu milioni 20-50
  3. Agosti 2007 - Shirika la Afya Duniani liliripoti ueneaji wa kasi mno wa magonjwa ya kuambukiza. [8]
  4. Pandemia ya Covid-19 iliyoanza kuenea duniani tangu mwaka 2019 na kuua angalau watu milioni 5.1 hadi 2021.[9]

Tanbihi

Viungo vya nje

Wikiwand in your browser!

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.

Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.

Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.