Remove ads

Kitabu cha Isaya kinashika nafasi ya kwanza kati ya vitabu vya kinabii vya Tanakh (Biblia ya Kiebrania) na vya Agano la Kale ambayo ndiyo sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo.

Thumb
Nakala ya zamani ya kitabu cha Isaya iliyopatikana kati ya magombo ya Bahari ya Chumvi.
Thumb
Kitabu cha Isaya kwa Kiebrania.

Utunzi na mada

Nabii Isaya (kwa Kiyahudi יְשַׁעְיָהוּ, yaani "YHWH anaokoa"), kuhani wa Yerusalemu mwenye elimu nzuri, alizaliwa katika Ufalme wa Yuda (Israeli Kusini) mwaka 765 hivi KK, akatabiri kwa muda usiopungua miaka 40 akiingilia kati matukio yote ya siasa, ambayo yalikuwa ya kutisha kutokana na nguvu za Waashuru ambao waliangamiza ufalme wa Israeli (Kaskazini) na kukaribia kufuta hata ufalme wa Kusini.

Maandishi yake yanapendeza kuliko yote ya Kiyahudi, hasa upande wa ushairi. Lakini ukuu wa Isaya uko hasa upande wa imani.

Kuanzia wito wake alioupata hekaluni, alipong’amua kwamba Mwenyezi Mungu ni mtakatifu kabisa, yaani tofauti mno na yeyote na chochote (6), alitawaliwa na wazo la utukufu wa Mungu na la unyonge wa binadamu anayehitaji kutakaswa naye. Kwa msingi huo alidai wafalme na wananchi wote wa Yuda wamtegemee Mungu tu, si mataifa yenye nguvu, hata upande wa siasa na mbele ya hatari kubwa namna gani.

Lakini toka mwanzo aliambiwa hatasikilizwa, hivyo ikambidi atabiri adhabu. Kweli hali haikuwa shwari, ndiyo sababu wengi walishindwa kuamini na kutulia, wakaendelea kujifanyia mipango na kutafuta msaada kutoka kwa binadamu, hasa Farao wa Misri. Hapo Mungu alimuagiza Isaya atembee uchi mwaka mmoja unusu ili kudokeza kuwa Wamisri watafanywa watumwa wa Waashuru wasiweze kusaidia kitu (20:1-6).

Katika kutuliza watu alimtabiria mfalme Ahazi kwamba mwanamwali atamzaa mtoto wa kiume atakayethibitisha uwepo wa Mungu pamoja na watu wake, jina lake Emanueli litakavyomaanisha. (7:1-17) Kweli mke wa Ahazi alimzaa Hezekia atakayeendeleza ufalme wa ukoo wa Daudi, lakini Wakristo wanaona utabiri huo ulimlenga zaidi Yesu, mwana wa Bikira (walivyoelewa watafsiri wa kwanza wa Biblia katika Kigiriki) ambaye kweli ni Mungu pamoja nasi, na ni mwana wa Daudi ambaye atatawala milele kwa amani na haki (11:1-9).

Hivyo, pamoja na adhabu kwa utovu wao wa imani (22:1-14), Isaya aliwatabiria watu wa Yuda kuwa Mungu hataangamiza kabisa taifa lake, bali ataacha mabaki yake ambayo yataleta wokovu (10:20-23): katika mabaki hayo Bikira atamzaa Masiya ambaye ni Mungu pamoja nasi, mwana wa Daudi ambaye ataleta amani na haki duniani.

Nafasi ya mwisho kwa Isaya kutuliza watu ilikuwa mwaka 701 KK ambapo jeshi kubwa la Waashuru lilizingira Yerusalemu na kutamka maneno ya kumkufuru Mungu. Isaya aliwarudishia jibu la dharau, nao kweli wakakimbia haraka baada ya kupatwa na tauni.

Isaya ni maarufu pia kwa ubora wa mashairi yake yaliyofanya ujumbe wake upendeze na uguse zaidi. Kwa sababu hiyo wengi walipenda kuyakariri na kuyasoma na hata kuiga mtindo wake: ndiyo maana kitabu chake kiliongezewa maandishi mengine mengi mpaka miaka mingi baada ya mwenyewe kuuawa kwa kukatwa kwa msumeno wakati wa mfalme Manase.

Isaya wa Pili

Katika kitabu chake unapatikana pia unabii wa wafuasi wake wasiojulikana, waliofanya kazi katika miaka 550-500 hivi K.K.

Ni kwamba, ingawa Ezekieli alifanya kazi nzuri, waliokuwa uhamishoni sehemu za Babuloni waliendelea kuzoea na kufurahia mazingira mapya yenye ustawi wa kiuchumi wakazidi kupotewa na hamu na tumaini la kurudi Yerusalemu.

Ndiyo sababu Mungu aliwatumia nabii mwingine mkubwa: hatujui jina lake, lakini tunamuita Isaya II kwa kuwa alifuata mapokeo ya Isaya na kulingana naye kwa ufasaha wa mashairi aliyoyatumia kutolea ujumbe wake; hivyo maandiko yake yamepangwa katika kitabu cha Isaya (40-55).

Sehemu hiyo inaitwa pia kitabu cha faraja ya Israeli kwa sababu ililenga kuwatia moyo Wayahudi wenzake huko Babeli kwamba Mungu atawarudisha kwao akitumia kama chombo chake mfalme Mpagani, kwa kuwa yeye anatawala watu wote pamoja na mioyo yao (Is 40:1-11). Hivyo akawafanya watamani kurudi badala ya kukwama katika kujitafutia maendeleo ya kidunia.

Kwa uchangamfu wa hali ya juu Isaya II alitabiri ukombozi na mwanzo mpya wa taifa kama ajabu kubwa kuliko lile la mababu wao kutoka Misri chini ya Musa. Alilifananisha na uumbaji mpya utakaowezekana kwa sababu Mungu wa Israeli si mmoja kati ya wengi, walivyodhani kwa muda mrefu, bali kweli ni peke yake, hakuna mwingine: ndiyo sababu anaweza yote. Imani hiyo ilizidi kutia mizizi kati ya Wayahudi na kuwaimarisha dhidi ya kishawishi cha kuabudu wengine.

Pamoja na hayo, katika sura hizo mna mashairi manne bora kuhusu mtumishi mteswa wa Bwana ambayo ndiyo utabiri bora juu ya Yesu na juu ya wokovu atakaoleta kwa kuteseka mwenyewe ili kufidia dhambi za wote (42:1-4; 49:1-6; 50:4-9; 52:13-53:12). Hatimaye Isaya II ndiye aliyeandaa dini ya Kiyahudi kupokea mataifa yote.

Isaya wa Tatu

Isaya 56-66 ni sura za baadaye tena (Isaya III, mwaka 500 hivi K.K.) ambazo zinawakaribisha watu wa mataifa yote kujiunga na Israeli katika kumuabudu Mungu pekee. Kiini chake ni Isa 61:1-3.

Remove ads

Ufafanuzi

Wikiwand in your browser!

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.

Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.

Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.

Remove ads