Namba ya mnyama
From Wikipedia, the free encyclopedia
Namba ya mnyama (kwa Kigiriki: Ἀριθμὸς τοῦ θηρίου) inayotajwa katika Ufunuo 13:18 humrejea Mpinga-Kristo.
Katika nakala nyingi za mstari huo, namba hiyo ni 666 inayoandikwa χξϛ (ambamo χ ni sawa na 600, ξni sawa na 60 na ϛ ni sawa na 6) [1] ila katika nyingine za zamani, kama vile Papyrus 115, namba yake ni 616.[2]
Maneno yenyewe ya kitabu hicho ni haya: "Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita." [3][4]
Katika historia ya Kanisa, changamoto hiyo ilipokewa na wengi kwa matokeo tofauti sana. Kwa kawaida waliojaribu kufafanua maana ya neno hilo la fumbo walilenga wapinzani wao ili kuonyesha kwamba walitabiriwa kuwa wabaya sana. Kwa mfano madhehebu ya Kikristo yalipogombana, kila upande uliweza kutafuta namna ya kutafsiri namba hiyo hivi kwamba iwataje wale wa upande wa pili.
Maarufu sana ni jaribio la baadhi ya Waprotestanti[5], hasa wa Marekani[6][7][8][9], la kusema huyo mnyama ni Papa wa Kanisa Katoliki kwa kuwa anadai kuwa wakili wa Yesu Kristo duniani[10]. Hivyo wakatunga wenyewe jina la Kilatini "Vicarius Filii Dei" (yaani "Makamu wa Mwana wa Mungu") na hata kusema jina au namba hiyo vimo katika kofia ya Papa. Halafu wakahesabu herufi chache za jina hilo ambazo zina thamani ya namba katika Kilatini na kupata namba 666.
Wakatoliki waliweza kujibu kwamba hakuna mtu mpumbavu kiasi cha kuandika katika kofia ya Papa namba ambayo imtambulishe kama Mpinga-Kristo: kati ya kofia 20 za Papa zilizotufikia, hakuna hata moja yenye jina hilo[11][12]. Pia kwamba Mtume Yohane hakujua Kilatini, na kwa vyovyote watumiaji wa lugha hiyo hawakuwa na desturi ya kuhesabu namba za majina, kwa sababu herufi nyingi za Kilatini hazikuwa pia tarakimu, isipokuwa zile ambazo wote tumejifunza shuleni kama namba za Kirumi, yaani I = 1, V = 5, X = 10, L = 50, C = 100, D = 500, M = 1,000.
Kumbe, tofauti na Kilatini na lugha nyingi, hasa za sasa, katika alfabeti za awali, kama ile ya Kiebrania na ile ya Kigiriki, kila herufi ilikuwa pia tarakimu iliyoweza kujumlishwa na ile ya herufi nyingine. Ndiyo sababu wasemaji wa lugha hizo walipenda kuhesabu herufi na kupata namba ya mtu. Kwa mfano, katika Kiebrania, jina Daudi linaandikwa דוד (DWD), ambamo herufi ya kwanza na ya mwisho ni ד (dalet), yenye thamani ya 4, na herufi ya katikati ni ו (waw) yenye thamani ya 6. Hivyo namba ya Daudi ni 14 = 4 + 6 + 4.
Kiebrania (au Kiaramu) na Kigiriki ndizo lugha alizozijua Yohane, hivyo tukitaka kuelewa alimaanisha nini, lazima tuangalie katika lugha hizo, ambazo ziliwezesha kuhesabu tarakimu zote.
Maelezo yanayokubalika zaidi[13][14][15][16][17][18][19] ni kwamba namba 666 ilimdokeza Kaisari Nero, wa kwanza kudhulumu Kanisa (64-68), kwa kuwa jina lake la Kigiriki likiandikwa kwa herufi za Kiebrania, jumla yake ni 666, na jina lake la Kilatini likiandikwa kwa herufi za Kiebrania, jumla yake ni 616. [20]
Huko Wadi Murabba'at limepatikana gombo lenye kutaja mwaka wa kuandikwa, yaani "mwaka wa pili wa Kaisari Nero", likitaja hivi pamoja jina na cheo chake.[21] Kwa Kiebrania ni Nron Qsr ("Nerōn Kaisar"). au Nro Qsr ("Nerō Kaisar").
- Nron Qsr
Kutokana na Kigiriki inaandikwa נרון קסר, na kuwa na thamani ya 666,[21] kama ifuatavyo:
Resh (ר) Samekh (ס) Qoph (ק) Nun (נ) Vav (ו) Resh (ר) Nun (נ) Jumla 200 60 100 50 6 200 50 666
- Nro Qsr
Kutokana na Kilatini inaandikwa נרון קסר, na kuwa na thamani ya 616,[13] kama ifuatavyo: ו קסר}}, yielding 616:[13]
Resh (ר) Samekh (ס) Qoph (ק) Vav (ו) Resh (ר) Nun (נ) Jumla 200 60 100 6 200 50 616
Basi, Yohane hakupenda kumtaja wazi Nero, pia kwa sababu aliandika akiwa uhamishoni katika kisiwa cha Patmos kutokana na dhuluma ya kaisari Domitian aliyetazamwa kama Nero aliyerudia kuishi[22][23], basi alimtaja kifumbo tu, labda akimaanisha pia huyo Domitian kama Nero mpya[24][25][26].