Alberto Mkuu
From Wikipedia, the free encyclopedia
Alberto Mkuu (Lauingen, Donau, leo nchini Ujerumani, 1205 hivi - Cologne, Ujerumani, 15 Novemba 1280) ni jina alilopewa kwa heshima askofu Alberto wa Bollstädt (au wa Cologne) kutokana na mchango wake mkubwa upande wa elimu ya kawaida na ile ya dini na vilevile upande wa uchungaji na wa upatanishi wa watu na watawala.
![Alberto Mkuu alivyochorwa na Tommaso da Modena mwaka 1352](http://upload.wikimedia.org/wikipedia/commons/d/d0/AlbertusMagnus.jpg)
Mtawa huyo wa Shirika la Wahubiri anahesabiwa kuwa mwanafalsafa na mwanateolojia bora wa Ujerumani katika Karne za Kati.
Alijitahidi kulinganisha imani na akili akiingiza falsafa ya Aristotle katika Ukristo, jambo lililoendelezwa na mwanafunzi wake bora, Thoma wa Akwino.
Alitangazwa na Papa Gregori XV kuwa mwenye heri mwaka 1622, na baadaye alitangazwa na Papa Pius XI kuwa mtakatifu na mwalimu wa Kanisa tarehe 16 Desemba 1931.
Mwaka 1941 Papa Pius XII alimtangaza msimamizi wa wanasayansi.
Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Novemba[1].