From Wikipedia, the free encyclopedia
Mzingo aktiki (kwa Kiingereza: Arctic circle) ni mstari wa kudhaniwa kwenye uso wa Dunia kwa latitudo ya 66° 33' 49 hivi[1]. Umbali wake na ncha ya kaskazini ni takriban kilomita 2,600.
Kinyume chake ni mzingo antaktiki upande wa kaskazini ya Dunia.
Mzingo aktiki unafafanuliwa na latitudo ambako Jua linaanza kuonekana kwa saa 24 mfululizo kwenye solistasi ya Juni, mnamo tarehe 21 au 22. Latitudo yake unabadilika kidogo mara kwa mara pamoja na kucheza kwa mhimili wa mzunguko wa Dunia.
Maana kwenye siku ya solistasi ya Juni (mnamo 21 Juni), Jua halitui tena chini ya upeo wa macho ndani ya mzingo aktiki hata saa za usiku wa manane. Kadiri latitudo inavyopungua, yaani tukielekea zaidi kwenda kaskazini na kukaribia ncha, kipindi cha mchana kinarefuka hadi kufikia nusu mwaka nchani kabisa.
Kinyume chake, ndani ya mzingo aktiki kwenye siku ya solistasi ya Desemba (mnamo 21 Desemba), Jua halichomozi tena juu ya upeo. Hii haimaanishi giza kabisa wakati wa mchana lakini hakuna zaidi ila nuru ya mapambazuko saa 6 mchana. Kadiri tunavyokaribia ncha yaani kufika kaskazini, kipindi cha usiku na giza kabisa hurefuka hadi kufikia nusu mwaka nchani kabisa.
Mzingo aktiki una urefu wa kilomita 16,000 hivi. [2] Maeneo ndani yake ni takribani kilomita za mraba 20,000,000 ambayo sawa na asilimia 4 za uso wa Dunia. [3]
Mzingo Aktiki hupita kwenye sehemu zifuatazo: Bahari Aktiki, Rasi ya Skandinavia, Asia ya Kaskazini (Siberia), Amerika Kaskazini, na Greenland. Nchi nane huwa na maeneo ndani ya mzingo aktiki: Norwei, Uswidi, Ufini, Urusi, Marekani (Alaska), Kanada (Yukon, Northwest Territories, na Nunavut), Denmark (Greenland), na Iceland (kisiwa cha Grímsey).
Tabianchi ndani ya mzingo aktiki kwa jumla ni baridi. Lakini pwani za Norwei si baridi sana kwa sababu zinapitiwa na maji ya Mkondo wa Ghuba unaopeleka maji ya vuguvugu kutoka ikweta hadi Norwei na Urusi kaskazini-magharibi ambako hayaruhusu maji ya bahari kuwa barafu wakati wa baridi kali. Hata ndani ya mzingo aktiki inawezekana kuwa na vipindi vya joto kabisa kwa muda mfupi; mfano mjini Norilsk (Krasnoyarsk Krai, Urusi) halijoto inaweza kupita sentigredi 30 kwenye mwezi wa Julai, lakini wakati wa Januari inaweza kushuka hadi sentigredi -50 (chini ya sifuri).
Kutokana na ukali wa tabianchi hakuna watu wengi wanaoishi ndani ya mzingo aktiki, kote duniani hawazidi milioni 4 kwa jumla. Kuna wakazi asilia waliowahi kuishi huko kwa miaka elfu kadhaa, kama vile Waeskimo au Waindio wa kaskazini. Siku hizi hao ni takriban asilimia 10 ya watu wote wanaoishi upande wa kaskazini wa mzingo aktiki[4] Takriban miaka 20,000 hadi 30,000 iliyopita makundi ya watu walihama kutoka Siberia wakivuka mlangobahari wa Bering na kuingia Amerika Kaskazini.
Miji mikubwa ndani ya mzingo aktiki iko katika Urusi, Norwei na Uswidi: Murmansk (wakazi 295,374), Norilsk (178,018), Tromsø (75,638), Vorkuta (58,133), na Kiruna (16,936).
Kwa upande wa Amerika hakuna miji mkubwa: Sisimiut (Greenland), ina wakazi wapatao 5,000 na Utqiagvik, Alaska ina wakazi 4,000.
Kuanzia meridiani ya sifuri na kuelekea mashariki, mzingo aktiki unapita hapa:
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.