Mwinjili Luka (kwa Kigiriki Λουκᾶς, Lukas) ni Mkristo wa karne ya 1 ambaye tangu zamani za Mababu wa Kanisa anasadikiwa kuwa mwandishi wa Injili ndefu kuliko zote za Biblia ya Kikristo. Humo alisimulia kwa ufasaha na kupanga kwa utaratibu mzuri matendo na mafundisho ya Yesu, akastahili kuitwa "mwandishi wa upole wa Kristo" (Dante Alighieri)[1].

Luka akimchora kwa mara ya kwanza Bikira Maria, kielelezo cha imani katika Injili yake.

Vilevile anasadikiwa kuwa mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume kinachoendeleza Injili hiyo ili kuonyesha kazi ya Yesu Kristo ilivyoendelea katika Kanisa lake kwa nguvu ya Roho Mtakatifu hadi mwaka 63 BK.

Hivyo Luka, mtunzi pekee wa Agano Jipya asiye Myahudi, anahesabiwa kuwa ameandika robo ya sehemu hiyo ya pili ya Biblia nzima ya Ukristo.

Pamoja na Wakristo wengine wengi, Kanisa Katoliki linamheshimu kama mtakatifu na msimamizi wa madaktari hasa katika sikukuu yake, tarehe 18 Oktoba[2].

Maisha

Luka alizaliwa katika familia ya Kiyunani, labda mjini Antiokia ya Syria, leo nchini Uturuki.

Inasadikiwa aliongozwa na Mtume Paulo kumpokea Yesu na alifanya naye kazi kwa takribani miaka 18. Pamoja na ukaribu huo, hata hivyo hakuandika tu mitazamo ya Paulo, hii ni kuonesha kuwa aliyaandika yale aliyovuviwa na Roho Mtakatifu baada ya utafiti wa kihistoria katika vyanzo mbalimbali.

Anatajwa na Paulo katika barua zake kama mganga aliye jirani naye katika majaribu yake: Waraka kwa Filemoni, mstari 24; Waraka kwa Wakolosai 4:14 na Waraka wa pili kwa Timotheo 4:11.

Uaminifu huo wa Luka kwa Paulo unalingana na habari za Matendo ya Mitume, ambapo Luka hajitaji, lakini anasimulia safari za Paulo akitumia mara nyingi neno "sisi". Hivyo anajishuhudia kuwa mshiriki wa utume wake.

Tazama pia

Tanbihi

Marejeo

Viungo vya nje

Wikiwand in your browser!

Seamless Wikipedia browsing. On steroids.

Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.

Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.