Remove ads
From Wikipedia, the free encyclopedia
Sahara ni jangwa kubwa kaskazini mwa Afrika. Ni jangwa kubwa kabisa barani, ni la kwanza duniani kati ya majangwa joto na jangwa la tatu kwa ukubwa ulimwenguni baada Bara la Antaktiki na Aktiki.[1]
Ina eneo la kilometa za mraba 9,200,000[2], sawa na eneo la Marekani au karibu sawa na eneo lote ya Ulaya.
Jina lake ni neno la Kiarabu (صحراء, sahra') linalomaananisha "jangwa".
Sahara inafunika sehemu kubwa ya Afrika Kaskazini isipokuwa kanda lenye rutuba kwenye ufuko wa Bahari Mediteranea, milima ya Atlas kwenye Maghreb na bonde la mto Naili huko Misri na Sudan. Inaenea kuanzia Bahari ya Shamu upande wa mashariki hadi Atlantiki upande wa magharibi, na kutoka Mediteranea upande wa kaskazini hadi kanda la Sahel upande wa kusini.
Wataalamu wa jiografia husema Sahara haikuwa hivyo wakati wote. Kutokana na utafiti wa dalili katika udongo na mawe yake eneo la Sahara katika milenia zilizopita lilikuwa na vipindi vya ukame vikifuatana na vipindi vya mvua.
Sahara iko kaskazini mwa Afrika. Ina nchi za Moroko, Algeria, Tunisia na Libya upande wa kaskazini. Upande wa kusini kuna nchi za kanda la Sahel kama Chad, Mali, Mauritania na Niger. Sahara ya Magharibi ina sehemu ufukoni mwa Atlantiki, na upande wa mashariki ni Sudani na Misri ambako oasisi ya mto Nile inakata eneo lake.
Upande wa magharibi Sahara inaanza kwenye pwani ya Atlantiki ikielekea hadi pwani ya Bahari ya Shamu kwa umbali wa km 5000. Kwa jumla maeneo ya Sahara ni takriban asilimia 30 za bara lote la Afrika.
Uso wa Sahara ni takriban asilimia 80 mawemawe na miamba. Takriban asilimia 20 umefunikwa na mchanga unaosukumwa na upepo kuwa na umbo la matuta ya mchanga ambao yanaweza kuwa na kimo cha mita 180 au zaidi. [3] Kama kila jangwa uso wake unafanyizwa na upepo na maji kutokana na mvua inayonyesha mara chache.
Kuna milima ambayo mara nyingi ina asili ya kivolkeno kama vile Aïr, Ahaggar, Tibesti, Adrar des Iforas na milima ya Bahari ya Shamu. Mlima mrefu ni volkeno ya Emi Koussi iliyo sehemu ya safu ya Tibesti kaskazini mwa Chadi.
Mito ya Sahara haiendelei mwaka wote ikiwa na maji kwa majira tu au hata kila baada ya miaka kadhaa kama mvua imenyesha. Mfano pekee wa kinyume ni mto Naili unaovuka jangwa lote kutoka vyanzo vyake katika Afrika ya Kati hadi kuishia katika Bahari Mediteranea.
Tabianchi ni ya joto na yabisi. Halijoto ni kati ya +58 °C wakati wa mchana ikishuka usiku hadi +13 °C (mlimani hadi -10 °C). Wastani wa mvua katika Sahara ni mm 45.5 kwa mwaka lakini kuna miaka bila mvua yoyote.
Katikati yake Sahara ni yabisi sana, uoto ni haba mno. Katika sehemu za kaskazini na kusini kuna maeneo yenye kiwango cha nyasi na vichaka vidogo kadhaa. Kama unyevu unaweza kudumu kwa muda katika mabonde, vichaka vinakuwa vikubwa zaidi na huko na huko kuna pia miti. Sehemu za milima ya juu ambako joto si kama vile kuna kiwango kidogo cha usimbishaji na hapo mabaki ya misitu ya zamani yapo.
Sehemu za katikati ambazo ni yabisi sana mara nyingi hazipokei mvua kwa miaka mfululizo.
Upande wa kaskazini katika Misri na sehemu za Libya jangwa la Sahara linafika moja kwa moja hadi ufuko wa Mediteranea. Lakini katika nchi za Maghreb jangwa linaishia mguuni pa milima ya Atlas ambayo ina tabianchi ya Kimediteranea yenye majira ya joto na ya baridi pamoja na mvua. Halihewa hiyo inaruhusu uoto wa miti na misitu pamoja na kilimo. Mpaka wa kaskazini wa Sahara unalingana na mpaka wa kaskazini wa kilimo cha mitende[4] na pia mpaka wa kusini wa uoto wa manyasi ya esparto ambayo ni nyasi ya Maghreb na rasi ya Iberia. Mpaka wa kaskazini unalingana pia na mwisho wa maeneo yanayopokea angalau milimita 100 za mvua kwa mwaka.[5]
Upande wa kusini Sahara inapakana na Sahel ambayo ni kanda la savana kavu yenye majira ya mvua na kanda hili laenea upana wote wa Afrika kutoka magharibi hadi mashariki. Mpaka wa kusini wa Sahara unalingana na mstari wa mwisho wa maeneo yanayopokea angalau milimita 150 za mvua kwa mwaka.[5]
Miji muhimu katika Sahara ni pamoja na:
Sahara haikuwa jangwa wakati wote. Michoro ya watu wa zamani katika milima ya Tibesti na Air inaonesha wawindaji na wanyama kama viboko na mamba wanaohitaji maji mengi. Wataalamu wamegundua kutokana na utafiti wa mawe na udongo ya kwamba eneo la Sahara lilikuwa na vipindi vikavu na vipindi vya mvua nyingi.
Mnamo miaka 7000 iliyopita Sahara ilikuwa eneo nusu yabisi lenye maji katika mito mirefu. Inawezekana kuilinganisha na Kenya Kaskazini ya leo. Watu waliwinda na kufuga wanyama.
Mnamo miaka 5000 iliyopita Sahara ilikauka hadi kufikia hali yabisi kama leo. Lakini maji ya mvua ya nyakati zile bado yapo chini ya ardhi. Misri na Libya ina miradi mikubwa ya kutumia maji yale kwa pampu na kuanza kilimo jangwani kabisa.
Flora ya Sahara ina mimea tofauti sana kulingana na mazingira mbalimbali ndani yake. Kuna kanda tatu za flora ambazo ni kaskazini, kati na kusini. Zinatofautiana kwa kiwango cha mvua inayonyesha. Wataalamu hutofautisha pia kanda mbili za mpito - mpito wa Mediteranea-Sahara na mpito wa Sahel.[6]
Kuna spishi 2800 za mimea ya juu, na robo ya spishi hizi inapatikana katika Sahara pekee. Nusu ya spishi ni za kawaida katika jangwa kuanzia huko hadi Uarabuni.[7]
Sahara ya Kati, ambayo ni kanda yabisi zaidi, ina spishi 500 za mimea pekee. Hii ni idadi ndogo kulingana na ukubwa wa eneo. Mimea kama miti, mitende, vichaka na manyasi imerekebisha kwa ajili ya mazingira haya kwa kuwa ndogo zaidi, kuhifadhi maji katika shina, na kukuza mizizi ya mlalo kwa kusudi la kukusanya maji na unyevu na pia kuwa na majani yenye ngozi nene (au umbo la sindano) ili kutopoteza maji mengi kwa njia ya uvukizaji. Mimea ina uwezo wa kukauka kabisa halafu kurudi baada ya miaka wakati mvua inanyesha.
Fauna ya Sahara pia ina spishi zilizorekebisha maumbile au maisha kulingana na mazingira. Kuna spishi za bweha na spishi za paa na swala. Paa anayeitwa addax anaweza kuishi mwaka mzima bila kunywa.
Duma ya Sahara imepungua sana kutokana na uwindaji lakini bado yuko Algeria, Togo, Niger, Mali, Benin na Burkina Faso. Lakini idadi ni chini ya duma 250 kwa jumla. Paka huyu anaepukana na jua kuanzia Aprili hadi Oktoba akipumzika wakati wa mchana mahali pa kivuli. [8][9]
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.