Remove ads
From Wikipedia, the free encyclopedia
Frumensyo, kwa Kigeez ፍሬምናጦስ, Frēmnāṭōs (Turo, Lebanon, mwanzoni mwa karne ya 4 - Ethiopia, 383 hivi) alikuwa askofu wa kwanza wa Aksum, akiwa ndiye aliyeingiza Ukristo katika ufalme wa Aksum.[1]
Mwaka 316 hivi, wakati alipotawala Kaisari Konstantino Mkuu kule Roma, meli moja ilikuwa safarini kutoka Shamu kwenda Bara Hindi ikaharibika kwenye pwani ya Ethiopia. Vijana wawili waliokolewa wakapelekwa mbele ya mfalme kule Aksum.
Mmojawao, kwa jina Frumensyo, alipata haraka sifa za kuwa mwenye elimu na hekima. Akapanda ngazi kuwa mshauri wa mfalme na mwalimu wa mwana wa mfalme aliyeitwa Ezana. Frumensyo aliweza kupanda mbegu za imani moyoni mwa kijana huyo. Baada ya kuwa mfalme, Ezana akaendelea kumtumia Frumensyo kama mshauri wake.
Siku moja Frumensyo aliomba ruhusa ya mfalme aende nyumbani kuangalia kama wazazi wake bado wanaishi. Mfalme akamruhusu akamwomba atafute kule walimu wanaoweza kufundisha elimu aliyokuwa nayo Frumensyo pamoja na imani ya Kikristo. Frumensyo akamwendea Atanasi wa Aleksandria, Askofu Mkuu wa Misri, aliyemweka wakfu kuwa askofu kwa ajili ya Waethiopia[2]. Hivyo Kanisa lilianza katika nyanda za juu za Ethiopia. Mfalme Ezana akabatizwa akifuatwa na watu wengi wa makao makuu.
Anaheshimiwa kama mtakatifu na Wakristo Waorthodoksi wa Mashariki, Waorthodoksi na Wakatoliki.
Sikukuu yake inaadhimishwa nao katika tarehe tofauti: 20 Julai[3], 18 Desemba[4], 30 Novemba na 27 Oktoba, lakini huko Ethiopia tarehe 1 Agosti.[5]
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.