Picha takatifu (pia "ikona" kutoka Kigiriki εἰκών, eikōn "picha" kwa kupitia Kiingereza icon) kwa kawaida ni mchoro unaoheshimiwa kidini hasa katika Ukristo wa Mashariki lakini pia katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo wa Magharibi, kama vile Kanisa la Kilatini.
Mara nyingi picha hizo zinamhusu Yesu, Bikira Maria, watakatifu wengine, malaika na msalaba.
"Sanaa ya Kikristo" inatajwa kwanza kati ya karne ya 2 na karne ya 3 katika maandishi ya Tertuliani (160 hivi - 220) na Klemens wa Aleksandria (150 hivi - 212).
Matumizi ya picha hizo yalipingwa na baadhi ya Wakristo, hasa wa mashariki, baada ya Uislamu kutokea na kuenea katika maeneo yao. Hapo kaisari Leo III wa dola la Roma Mashariki alikataza picha hizo ili kujilinganisha na Waislamu na kujenga uhusiano mzuri nao.
Kumbe wamonaki na Wakristo wengine wengi walipinga katazo hilo. Ndio mwanzo wa mabishano makubwa yasiyoishia katika hoja na maandishi, bali yalichukua uhai wa watu, hasa waliodhulumiwa na serikali.
Hatimaye Mtaguso wa pili wa Nisea (787) ulithibitisha uhalali wa picha hizo na wa heshima ambazo zinapewa, kama ulivyotetewa hasa na mtakatifu Mwarabu Yohane wa Damasko.
Pamoja na kwamba picha takatifu zinasema na mioyo ya waamini wanyofu, mara nyingi utaalamu wa ikonografia unahitajika hasa katika kufafanua picha takatifu za Ukristo wa Mashariki, kwa kuwa hizo hazilengi kuiga sura halisi zinavyoonekana na macho, bali kudokeza mafumbo ya imani ili kuona yasiyoonekana.
Tanbihi
Marejeo
Marejeo mengine
Viungo vya nje
Wikiwand in your browser!
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.