Remove ads
From Wikipedia, the free encyclopedia
Filioque ni neno la Kilatini lenye maana ya "na (kwa) Mwana".
Linapatikana katika Kanuni ya Imani inayotumiwa na Wakatoliki hasa katika ibada ya siku ya Jumapili mwishoni mwa liturujia ya Neno kama itikio la kukubali Neno la Mungu lililotangazwa.
Neno hilo liko mwanzoni mwa sehemu ya tatu ya Nasadiki, ambayo inakiri imani kwa Roho Mtakatifu:
"Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya manabii."
Neno hilo ni maarufu kutokana na suala la teolojia lililojitokeza baada ya baadhi ya makanisa ya Kilatini kuliongeza (mwishoni mwa karne ya 6) katika Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli iliyoanza kutumika katikati ya Misa.
Bila makubaliano ya kimataifa, neno hilo liliingizwa katika hiyo fomula rasmi ambayo ilipitishwa na Mtaguso wa kwanza wa Nisea (325)[1] ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake.
Ndiyo sababu neno Filioque lilipingwa na Makanisa ya Kiorthodoksi kama upotoshaji wa imani juu ya mahusiano kati ya nafsi tatu za Mungu.[2][3]
Suala hilo lilichangia sana farakano la miaka 1000 hivi kati ya Ukristo wa Mashariki na Ukristo wa Magharibi kwa sababu lilihusu kiini chenyewe cha imani, yaani fumbo la Utatu Mtakatifu.
Baada ya ekumeni kustawi katika karne ya 20, idara husika ya Kanisa Katoliki huko Vatikano iliweka wazi mwaka 1995 kwamba, kama maneno ya Kigiriki καὶ τοῦ Υἱοῦ ("na kwa Mwana") yangeongezwa kwa ἐκπορεύομαι yangekuwa ya kizushi kweli[4][5][6] lakini neno Filioque si la kizushi likiongezwa kwa neno la Kilatini procedit kwa kuwa hilo si sawa na ἐκπόρευμαι[7][8]
Ni kwamba neno la Kigiriki ἐκπόρευμαι lina maana ya kuvuviwa, nalo linaeleza namna gani Roho Mtakatifu anatokana na Baba, tofauti na ile ya Mwana ambayo ni ya kuzaliwa. Kumbe neno la Kilatini procedit lina maana ya kufuata, kuandamana na, nalo linaeleza kwamba Roho Mtakatifu si nafsi ya kwanza; basi Wakristo waliotumia lugha hiyo waliona afadhali kuweka wazi kwamba si nafsi ya pili pia, bali ya tatu, baada ya Baba na Mwana.
Itikio la Waorthodoksi kwa maelezo hayo linaweza kutia tumaini la uelewano kwa siku zijazo, huku majadiliano yakiendelea.[9]Kamati ya pamoja ilitamka mwaka 2003 kwamba suala hilo halitoshi tena kudai farakano lidumu.[10]
Kwa kuwa maneno yaliingizwa bila makubaliano na hayafai kuongezwa katika Kigiriki, Papa Yohane Paulo II na Papa Benedikto XVI walitumia kanuni ya imani ya Nisea-Kostantinopoli bila nyongeza walipoungana na Patriarki Dimitri I na Patriarki Bartholomayo I katika kukiri imani hadharani pamoja.[11][12][13]
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.