From Wikipedia, the free encyclopedia
Papa Benedikto XVI ( Marktl am Inn, Bavaria, Ujerumani, 16 Aprili 1927 [1] - Vatikani, 31 Desemba 2022; jina la Kilatini: Benedictus XVI; kwa Kiitalia: Benedetto XVI) alikuwa Papa tangu tarehe 19 Aprili 2005, baada ya kifo cha Papa Yohane Paulo II, hadi alipoamua kung'atuka tarehe 28 Februari 2013 kwa sababu ya afya yake kudodora[2].
Mwandamizi wa 264 wa Mtume Petro na Papa wa kwanza kutoka Ujerumani baada ya miaka 1,000 hivi, amefuatwa na Papa Fransisko.
Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Joseph Alois Ratzinger.
Alipadirishwa tarehe 29 Juni 1951 pamoja na kaka yake Georg.
Baada ya kupata udaktari katika teolojia na kufundisha miaka kadhaa, alishiriki kama mtaalamu katika Mtaguso Mkuu wa Vatikano II.
Tarehe 24 Machi 1977 alichaguliwa na Papa Paulo VI kuwa Askofu mkuu wa Munchen na Frisingen akapewa daraja hiyo tarehe 28 Mei mwaka huohuo.
Tarehe 27 Juni mwaka huohuo Paulo VI alimteua pia kardinali na kutokana na cheo hicho alishiriki uchaguzi wa Papa Yohane Paulo I na Yohane Paulo II mwaka 1978.
Tarehe 25 Novemba 1981 Yohane Paulo II alimteua kuwa mkuu wa Idara ya Mafundisho ya Imani. Hivyo tarehe 15 Februari 1982 aliacha uongozi wa jimbo kuu akashika kazi hiyo mpya mpaka alipochaguliwa Papa.
Katika kutekeleza kazi hiyo aliandaa Katekisimu ya Kanisa Katoliki (tangu 1986 hadi 1992) na Ufupisho Makini wa katekisimu hiyo (tangu 2003 hadi 2005).
Baada ya kuchaguliwa Papa aliendeleza juhudi za mtangulizi wake katika utekelezaji wa Mtaguso pamoja na kupambana na makwazo ya kijinsia yaliyokuja kujulikana kwa wingi wakati wa Upapa wake ingawa mengi yalikuwa ya miaka ya nyuma.
Chini yake idadi ya Wakatoliki duniani iliongezeka kutoka 1,115,000,000 hadi 1,254,000,000.
Baada ya kung'atuka hadi kufariki dunia, Benedikto alishika kwa unyenyekevu mkubwa maisha ya sala tu kwenye monasteri iliyopo ndani ya Vatikani, bila kuingilia kabisa Upapa wa Fransisko.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.