Vita vya kwanza vya Italia na Ethiopia
From Wikipedia, the free encyclopedia
Vita vya kwanza vya Italia na Ethiopia vilitokea kati ya Italia na Ethiopia miaka 1895-1896. Waethiopia walishinda na kuhakikisha uhuru wa nchi yao hivyo kufanya Ethiopia nchi ya pekee ya Afrika iliyofaulu kuzuia ukoloni[1].
Mwaka 1889 mtemi wa Shewa Menelik II alijitangaza Negus wa Ethiopia baada ya kushinda mapigano kati ya watemi wa Ethiopia yaliyofuata kifo cha Negus aliyemtangulia Yohane IV. Katika hilo Menelik alisaidiwa na Waitalia ambao walikuwa wameshika Eritrea tayari.
Mnamo Mei 1889 Menelik alifanya mkataba wa Wuchale alimokubali utawala wa Italia juu ya kanda ya pwani pamoja na maeneo kadhaa ya nyanda za juu za Tigray yakiwemo mazingira ya Asmara ya leo.
Italia ilidai, kutokana na nakala ya Kiitalia ya mkataba huo, haki ya ulinzi juu ya Ethiopia[2]. Nakala ya Kiethiopia haikuonyesha vipengele kuhusu ulinzi wa Italia juu ya ufalme wa Ethiopia[3]. Menelik aliimarisha utawala wake na mwaka 1893 alikana mkataba.
Italia ilijibu kwa kuvamia Ethiopia kwa jeshi kubwa mnamo Oktoba 1895. Menelik aliweza kukusanya takriban wanajeshi 100,000 na kuwaongoza hadi Tigray (jimbo jirani na Eritrea)[4].
Mapigano ya kwanza ndani ya Tigray ya Amba Alagi (7 Desemba) na ya Mekelle hayakuenda vizuri kwa Waitalia. Waethiopia walishindwa kuteka boma la Mekelle, lakini Waitalia walifungwa ndani kwa wiki tatu. Mwishowe waliondoka baada ya mapatano na Negus Menelik II na kurudi Eritrea[5].
Sehemu kubwa ya jeshi la Italia haikuingia bado katika mapigano. Gavana jenerali Oreste Baratieri alikataa kuwashambulia Waethiopia baada ya kujua idadi yao kubwa. Lakini alijua ya kwamba Menelik hataweza kulisha askari wengi hivi kwa muda mrefu katika milima ya Tigray, akataka kusibiri hadi jeshi la Negus litakapoanza kusikia njaa na kupungua.
Lakini serikali ya Roma ya waziri mkuu Francesco Crispi, baada ya kupokea habari za mapigano ya kwanza, iliona aibu ya kushindwa na Waafrika ikamwamuru gavana ashambulie mara moja.