Teofilo wa Antiokia
From Wikipedia, the free encyclopedia
Teofilo wa Antiokia (kwa Kigiriki Θεόφιλος ὁ Ἀντιοχεύς, Theofilos o Antiokheus, alifariki 183/185 BK) alikuwa Patriarki wa Antiokia[1] baada ya Eros na kabla ya Maximus I[2][3].
![Thumb image](http://upload.wikimedia.org/wikipedia/commons/thumb/6/64/TheophilusofAntioch.png/220px-TheophilusofAntioch.png)
Kutoka maandishi yake (Eusebi wa Kaisarea na Jeromu walitaja vitabu mbalimbali vya Teofilo vilivyokuwepo nyakati zao, ambavyo kati yake kimebaki kile Utetezi kwa Autolycus[4], rafiki yake msomi lakini Mpagani) tunajua kwamba alizaliwa na Wapagani katika eneo la mito Tigri na Eufrate, na kwamba aliingia Ukristo kwa kusoma Biblia, hasa vitabu vya kinabii.[5]
Kutoka kwa mwanahistoria Eusebius wa Kaisarea tunajua juhudi zake za kupinga uzushi, hasa ule wa Marcion[6], akichangia fasihi ya Kikristo, hoja za dini, ufafanuzi wa Biblia na utetezi wa dini.[7]
Maandishi yake ndiyo ya zamani kuliko yale yote tuliyonayo yanayotaja Utatu Mtakatifu.
Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu.