Kupatwa kwa Jua
From Wikipedia, the free encyclopedia
Kupatwa kwa Jua (kwa Kiingereza solar eclipse) ni hali ya Jua kutoonekana (au kuonekana kwa sehemu tu) angani wakati wa mchana kwa muda fulani hata pasipo mawingu. Kunatokea wakati mwezi unapita kati ya Jua na dunia na kufunika Jua. Tokeo lake ni kupungua kwa nuru ya Jua hadi kutoonekana kwa muda wa kufika kwa giza wakati wa mchana. Muda wa kufunikwa kabisa ni dakika chache tu.
![Thumb image](http://upload.wikimedia.org/wikipedia/commons/thumb/f/fd/Solar_eclipse_animate_%282006-Mar-29%29.gif/220px-Solar_eclipse_animate_%282006-Mar-29%29.gif)
Kupita kwa kivuli cha mwezi duniani wakati wa kupatwa kwa Jua. Watu katika eneo kubwa la giza waliona kupatwa kwa Jua kisehemu. Nukta nyeusi yaonyesha sehemu ya "umbra" ambako Jua lilipatwa kabisa. Duara kubwa zaidi ya kijivu linaonyesha maeneo katika "penumbra", yaani kivuli cha kando.
"Central duration" inataja muda wa kupatwa kabisa kwenye kitovu cha kivuli; namba katika kona ya juu huonyesha saa za tarehe 29 Machi kupatwa kulipotokea.
Kuna utofauti kati ya “Kupatwa kiasi” (ing. partial eclipse) na “Kupatwa kikamilifu” (ing. total eclipse). Kupatwa kwa Jua hutokea kila mwaka, angalau mara mbili hadi mara tano. Lakini kupatwa kabisa kwa Jua hautokei zaidi kuliko mara mbili kwa mwaka.[1][2]. Huonekana katika sehemu za Dunia pekee, si kote.