Idi Amin
Rais wa Uganda kuanzia 1971 hadi 1979 / From Wikipedia, the free encyclopedia
Idi Amin Dada (/ˈiːdi ɑːˈmiːn/; 1923–1928 – 16 Agosti 2003) alikuwa mwanasiasa na afisa wa jeshi ambaye alipata kuwa Rais wa Uganda kuanzia mwaka 1971 hadi 1979. Alitawala kidikteta ilhali uchumi wa nchi uliporomoka na makosa mengi ya jinai dhidi ya haki za kibinadamu yalitendwa.
Idadi ya watu waliouawa Uganda chini ya utawala wake imekadiriwa kuwa kati ya 100,000[1] na 500,000.[2]
Katika miaka yake ya kushika serikali Amin alibadilika kutoka uhusiano wa kirafiki na nchi za magharibi, na hasa Israeli, kuhamia upande wa Muammar Gaddafi wa Libya, Mobutu Sese Seko wa Zaire, Umoja wa Kisovyeti na Ujerumani ya Mashariki.[3][4][5] Hata hivyo Amin alipata usaidizi wa ofisi ya upelelezi ya Marekani CIA iliyotuma silaha na vifaa vingine kwa jeshi lake.[6]
Mwaka 1977 Amin alivunja uhusiano wa kidiplomasia na Ufalme wa Maungano (Uingereza) akajitangaza kuwa alishinda na kujiongezea sifa ya CBE ("Conqueror of the British Empire"). Kuanzia wakati ule cheo chake rasmi kilikuwa "His Excellency President for Life, Field Marshal Alhaji Dr. Idi Amin Dada, VC, DSO, MC, CBE".[2]
Jaribio la Amin la kutwaa sehemu za Mkoa wa Kagera wa Tanzania kwenye mwaka 1978 lilisababisha Vita ya Kagera baina ya Tanzania na Uganda na mwisho wa utawala wake. Amin alikimbia kukaa ugenini Libya na baadaye Saudia alipoishi hadi kifo chake mwaka 2003.