Remove ads
From Wikipedia, the free encyclopedia
Zaka (kutoka neno la Kiarabu زكاة, zakat, lenye maana ya "kinachotakasa"; kwa Kiingereza: Tithe) ni toleo la sehemu ya mapato ambalo muumini wa dini fulani anapaswa kutoa kwa Mungu, kwa viongozi wa dini husika au kwa maskini.
Desturi ya Mashariki ya Kati ya kutoa sehemu moja ya kumi kwa makuhani iliingia katika Uyahudi kuanzia Abrahamu aliyempa Melkisedek mfalme wa Salem aliyekuwa pia kuhani wa El Elyon (Mungu Mkuu).
Habari hiyo inasimuliwa katika Kitabu cha Mwanzo 14:18-20 [1] na kusisitizwa na Waraka kwa Waebrania 7:5 [2].
Zaka (kwa Kiebrania מעשׂר, ma‛ăśêr, kwa Kigiriki δεκάτη, dekatē) inaagizwa na vitabu vingine vya Biblia ya Kiebrania, kama vile Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Sheria katika Torati.
Baadaye wajibu huo ulisisitizwa na Kitabu cha Malaki 3:8-12 [3]na Kitabu cha Tobiti 1:6–8 (humo zinatajwa aina tatu za zaka zilizozingatiwa baada ya uhamisho wa Babeli [4]).
Katika Agano Jipya, Yesu alilaumu Mafarisayo kwa kulipa zaka kamili hata kwa vitu vidogo kama mboga na viungo pamoja na kupuuzia mambo makubwa zaidi kama haki na huruma (Injili ya Mathayo 23:23 [5]).
Mtume Paulo alifundisha kuwa anayetumikia kwenye altare anastahili kupata riziki zake kwa njia hiyo (Waraka wa kwanza kwa Wakorintho 9:13 [6]). Pia alihimiza waamini kutoa kwa moyo mkunjufu (Waraka wa pili kwa Wakorintho 9:7 [7])
Mwanzoni mwa Kanisa waamini walikuwa wanawajibika, lakini hakuna hata babu wa Kanisa mmoja aliyehimiza zaka.
Baadaye katika Ukristo wa Magharibi zilianza kutolewa sheria ili kuihimiza, kwa mfano huko Ufaransa katika mtaguso wa Tours (567) na ule wa Mâcon (585).
Hatimaye Papa Adrian I alipitisha maagizo hayo mwaka 787 na Mtaguso wa Trento uliyasisitiza[8].
Baadaye njia za kuwategemeza viongozi wa Kanisa zilitofautiana kadiri ya nchi na madhehebu.
Leo Wabaptisti na Wapentekoste ndio wanaoongoza kwa kusisitiza wajibu wa kutoa sehemu moja ya kumi ya mapato yote[9].
Kumbe Wakatoliki wanafundishwa kuwajibika ili kulipatia Kanisa mahitaji yake, kila mmoja kadiri ya uwezo wake, lakini kimataifa zaka haitajwi na Mkusanyo wa Sheria za Kanisa wala na Katekisimu ya Kanisa Katoliki [10].
Vilevile Waorthodoksi, wakiendeleza mapokeo yao ambamo zaka haikushurutishwa kamwe, wanahimizwa kutoa bila kulazimishwa kiasi fulani kilichokwishapangwa[11].
Maana za zaka katika dini ya Uislamu ni nyingi. Kisheria ni kiwango maalumu cha mali kinachotolewa wakati maalumu kwa watu maalumu.
Zaka [12] ni kati ya faradhi za dini ya Kiislamu, na ni ya tatu kati ya Nguzo Tano za Kiislamu. Kadiri ya Kurani, Mwenyezi Mungu anasema: "Na simamisheni swala na toeni zaka". [13]
Akasema Mtume Muhamad: "Umejengwa Uislamu kwa mambo matano: Kushuhudia ya kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni mja wake na ni Mtume wake, na kusimamisha Swala (tano za kila siku), na kutoa Zaka, na kuhiji nyumba tukufu (Al-ka’abah – ilioko Makkah), na kufunga Mwezi wa Ramadhani" [14].
Zaka ni mojawapo ya nguzo za Uislamu, ambayo inadai muumini atoe sehemu fulani ya mapato yake kwa maskini. Masharti ya mtu kulazimika kutoa zaka ni:
1. Iwe Nisabu ni ziada ya mahitaji ya dharura ambayo mtu hatosheki kwa kuyapata mahitaji hayo, kama chakula, mavazi na makazi, kwa sababu zaka ni wajibu kwa lengo la kuwaliwaza fukara. Hivyo basi inatakiwa mwenye kutoa hiyo mali asiwe mhitaji mwenyewe.
2. Iwe Nisabu inamilikiwa na mtu maalumu umiliki mkamilifu, basi haiwajibiki zaka kwa mali ambayo haimilikiwi na mtu maalumu, kwa mfano: mali iliyokusanywa kwa lengo la kujenga msikiti, au mali iliyowekwa wakfu kwa maslahi ya umma, au mali iliyoko kwenye hazina za jumuia za mambo ya kheri.
3. Mali kupitiwa na Mwaka: Ni mwaka wa Kiislamu uliokamilika. Hii ni kwamba ipite miezi kumi na miwili ya kalenda ya mtizamo wa mwezi hali ya kuwa Nisabu iko kwenye miliki ya mwenye mali. Na sharti hili ni peke yake kwa pesa (dhahabu na fedha), na mapato ya biashara, na wanyama wa mifugo. Ama mazao ya kilimo na matunda, na madini, hazina iliyozikwa ardhini si sharti kwa vitu hivi kupitiwa na mwaka.
Tendo hilo muhimu la kutoa msaada linatazamwa na Waislamu kama njia ya kujipatia utakaso wa uroho na ubinafsi na ya kubarikiwa katika riziki zao.
Anayekataa kutoa zaka, ama amekataa kwa kupinga kwamba si lazima kutoa [Juhuud: Ni kukataa kuwajibishwa kwake.], ama kwa ubahili.
Anayepinga wajibu wa zaka basi amekufuru kwa makubaliano ya umma wote – ikiwa mtu huyu anajua vizuri wajibu wa Zaka; kwa sababu atakuwa amemzulia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Atakayekataa kutoa zaka kwa ubahili wake basi huchukuliwa kutoka kwake zaka kwa nguvu wala hawi kafiri kwa kufanya hivyo kukataa kutoa zaka kwa ubahili.
Atakuwa ametenda dhambi kubwa miongoni mwa madhambi makubwa na ni uovu mkubwa sana.
Kwa kauli ya Mtume kuhusu wanaokataa kutoa zaka: “Mtu yeyote aliye na hazina ya dhahabu na fedha na wala haitolei zaka basi atachomwa nayo katika moto wa Jahannam na itajaaliwa kama vinoo ambavyo atapigwa navyo kwenye migongo na vipaji kila akipata ubaridi (yakipoa makali ya moto) anaregelewa tena (kupigwa navyo), mpaka Allaah amalize kuhukumu waja wake siku ambayo ni sawa na miaka elfu khamsini. Kisha ndio ataoneshwa njia yake ikiwa ni ya peponi au motoni” [15].
Lau atapigana na kukataa kutekeleza amri ya zaka basi mpigeni vita mpaka arudi katika kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, na atoe zaka, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu: "Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi iacheni njia yao (waacheni" [16]).
Kwa kauli ya Mtume: "Nimeamrishwa niwapige watu vita mpaka washuhudiye ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na wasimamishe swala, na watoe zaka, watakapofanya hivyo basi imeharamishwa kwangu damu yao na mali yao isipokuwa kwa haki ya Uislamu, na malipo yao yako kwa Mwenyezi Mungu" [17].
Abubakar pia alipiga vita mtu yeyote ambaye alipinga wajibu wa zaka, akasema: "Naapa kwa Mungu ya kwamba nitampiga vita yoyote aliyetenganisha kati ya swala na zaka, kwa hakika hiyo Zaka ni haki ya mali, Wallaahi kama wakinizuilia hata kwa (kamba ya) kutiwa shemere (anayofungwa mnyama kwenye pua zake) nitapambana nao maadamu walikuwa wakiitoa kwa Mtume" [18].
Katika dini ya Sikh muumini anadaiwa kutoa dasvand (ਦਸਵੰਦ) maana yake moja kwa kumi. Inaonekana sheria hiyo ilitokana na Uislamu.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.