Shule ya Aleksandria
From Wikipedia, the free encyclopedia
Shule ya Aleksandria ni jina lenye maana pana likihusu maelekeo maalumu katika falsafa, fasihi, tiba na sayansi kwa jumla ambayo yalistawi katika mji wa Aleksandria nchini Misri wakati wa utawala wa Wagiriki na Waroma wa kale.
Kabla ya Misri kutwaliwa na Dola la Roma wafalme Watolemayo wa Misri waliwahi kuunda maktaba maarufu ambayo huaminiwa kuwa wakati wake ilikuwa maktaba kubwa zaidi duniani yenye vitabu 700,000. Kwa hakika ilikuwa maktaba kubwa kote Afrika, Ulaya na Asia ya Magharibi. Hii ilikuwa na thamani kubwa kupita kiasi wakati ambako vitabu viliandikwa na kunakiliwa kwa mkono tu, na hivyo kuwa haba. Aleksandria ilikuwa kitovu cha elimu na uchunguzi wa kitaalamu duniani.