![cover image](https://wikiwandv2-19431.kxcdn.com/_next/image?url=https://upload.wikimedia.org/wikipedia/commons/thumb/b/b6/Croixrouge_logos.jpg/640px-Croixrouge_logos.jpg&w=640&q=50)
Shirika la Msalaba Mwekundu
From Wikipedia, the free encyclopedia
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na lile la Hilali Nyekundu ni mashirika ya kibinadamu yenye wahudumu wa kujitolea takriban milioni 97 duniani kote [1] ambayo yalianzishwa ili kulinda masilahi ya afya ya binadamu, kuhakikisha heshima kwa hulka ya mwanadamu, na kuzuia na kupunguza mateso ya kibinadamu, bila ubaguzi wowote kwa misingi ya utaifa, rangi, jinsia, imani za kidini, daraja la kijamii au maoni ya kisiasa.
![]() The Red Cross and the Red Crescent emblems, the symbols from which the Movement derives its name. | |
Founded | 1863 |
---|---|
Location | Geneva, Switzerland |
Area served | Worldwide |
Focus | Humanitarian |
Method | Aid |
Website | http://www.redcross.int/ |
Jina maarufu la Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu ni dhana tu, kwani hakuna shirika lolote lililosajiliwa rasmi kwa jina hilo. Katika hali halisi, shirika hili lina mashirika tofauti kadhaa ambayo kisheria hujitegemea mbali na lile lingine, lakini yameungana pamoja kupitia kanuni za kimsingi, madhumuni, ishara, masharti na vyombo vya serikali. Vipengee muhimu vya shirika hili ni:
- Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ni taasisi ya kibinafsi ya kibinadamu iliyoanzilishwa mnamo mwaka wa 1863 mjini Geneva, Uswisi na Henry Dunant. Kamati hii inayojumuisha wanachama 25 ina mamlaka ya kipekee chini ya sheria ya kibinadamu ya kimataifa kulinda maisha na heshima ya walioathirika na migogoro mbalimbali ya kimataifa. ICRC imewahi kupatiwa Tuzo ya Amani ya Nobel mara tatu (mwaka 1917, 1944 na 1963). [2]
- Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) ilianzishwa mwaka wa 1919 na kwa sasa huratibu shughuli kati ya 186 za kitaifa za Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu katika Shirikisho. Kimataifa, Shirikisho linaongoza na kupanga, kwa ushirikiano wa karibu wa Vyama vya wa kitaifa , misaada pamoja na kukabiliana na mahitaji ya dharura. Sekretarieti ya Shirikisho la Kimataifa ina makao yake mjini Geneva, Uswizi. Mwaka wa 1963, Shirikisho (likijulikana kama Shirikisho la Vyama vya Msalaba Mwekundu) lilipatiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa pamoja na ICRC. [2]
- Vyama vya kitaifa vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu zipo katika takriban kila nchi duniani. Kwa sasa, Vyama 186 vya kitaifa vinatambuliwa na ICRC na kujumuishwa kama wanachama kamili wa Shirikisho. Kila kipengee hufanya kazi katika nchi yake kwa mujibu wa kanuni za sheria ya kibinadamu ya kimataifa na amri ya Muungano wa kimataifa. Kwa mujibu wa hali na uwezo wake maalum, Vyama vya Kitaifa vinaweza kuchukua kazi za ziada za kibinadamu ambazo hazijatambulikana moja kwa moja katika sheria ya kibinadamu ya kimataifa au katika Mustakabali wa utenda kazi wa Muungano wa kimataifa. Katika nchi nyingi, zimejumuishwa kwa karibu sana na mfumo wa afya kwa kutoa Huduma ya utabibu kwa dharura.