Kitabu cha Ezra
From Wikipedia, the free encyclopedia
Kitabu cha Ezra kinapatikana katika Biblia ya Kikristo katika Agano la Kale.
Kiasili kiliandikwa kwa lugha ya Kiebrania lakini kuna pia sehemu fupi za Kiaramu.
Andiko la Ezra lilitunzwa katika Biblia ya Kiebrania pamoja na Nehemia kama kitabu kimoja lakini kimegawiwa baadaye kuwa vitabu viwili ambavyo Vulgata inavitaja kama "Esdras I" na "Esdras II".
Kitabu kinasimulia habari za Wayahudi chini ya utawala wa Waajemi.
Mwaka 587 KK mfalme wa Babeli alikuwa amevamia mji wa Yerusalemu, kubomoa hekalu la Sulemani na kumaliza ufalme wa Yuda. Wakazi walipelekwa Mesopotamia kwa uhamisho wa Babeli. Tangu wakati huo Waisraeli kwa kawaida walijulikana kuwa Wayahudi. Lakini, kwa kuwa utengano wa Israeli haukuendelea, majina hayo mawili, pamoja na jina la Waebrania, yaliweza kutumiwa kwa watu walewale (Yer 34:9; Yn 1:19, 47; 2 Kor 11:22; Gal 2:14).
Mwaka 539 KK Waajemi chini ya mfalme Koreshi walivamia Babeli ambayo ikawa jimbo la milki ya Uajemi. Koreshi aliwaruhusu Wayahudi kadhaa warudi Yerusalemu na kujenga upya hekalu.
Habari hizi na zilizofuata zinasimuliwa katika vitabu vya Ezra na Nehemia.
Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.