Hipoliti wa Roma
From Wikipedia, the free encyclopedia
Hipoliti wa Roma (170–235) alikuwa mwanateolojia muhimu zaidi wa Kanisa la Roma katika karne ya 3. Labda alizaliwa mjini Roma[1], lakini alipendelea kuandika kwa Kigiriki kuliko kwa Kilatini ambacho kilikuwa kinazidi kutumika katika Kanisa hilo badala ya lugha ya kimataifa iliyotumika tangu wakati wa Mitume Petro na Paulo.
Inasemekana alianza kushindana na mapapa wa wakati wake kuhusu toba ya walioasi katika dhuluma za serikali ya Dola la Roma dhidi ya Wakristo. Anatajwa kama antipapa wa kwanza kwa kuanzisha farakano [2]. Hata hivyo habari hiyo na nyingine nyingi juu yake hazina hakika.
Hatimaye alipatana na Papa Pontian wakiwa uhamishoni katika kisiwa cha Sardinia walipofia dini yao.
Ndiyo sababu tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu mfiadini, hasa tarehe 13 Agosti[3] ambayo ndiyo sikukuu yake.