From Wikipedia, the free encyclopedia
Azania (kwa Kigiriki: Ἀζανία) ni jina la kihistoria la sehemu mbalimbali za pwani ya Afrika ya Mashariki[1][2]. Asili yake ni zamani za Waroma na Wagiriki wa kale kwa eneo lililokuwa la watu wa Lugha za Kikushi.[3]
Mara ya kwanza jina hili limepatikana katika mwandishi Mroma Plinio Mzee (Gaius Plinius Secundus) aliyeishi wakati wa karne ya 1 B.K.
Kufuatana na maelezo yake, Azania ni sehemu zile zilizoanza katika eneo la Adulis (leo: Eritrea) na kuelekea kusini.
Kitabu cha mwongozo kwa ajili ya mabaharia "Periplus ya Bahari ya Eritrea" (karne ya 2 BK) kinatoa maelezo zaidi zinazoonyesha ya kwamba jina la Azania labda lilimaanisha pwani ya Afrika ya Mashariki kutoka Eritrea hadi Tanzania ya leo.
Mwandishi Cosmas Indicopleustes wa karne ya 6 B.K. aliandika Azania ni nchi chini ya utawala wa ufalme wa Aksum, basi hapo isingeenea sana kusini kwa pembe la Afrika.
Katika karne zilizofuata umbo la "Azania" halikutumika tena. Inawezekana ya kwamba sababu yake ilikuwa Waarabu Waislamu walichukua nafasi ya Wagiriki na Waroma wakitawala biashara ya nje ya pwani ya Afrika ya Mashariki. Kuna uwezekano ya kuwa Waarabu walitumia umbo tofauti la neno kuwa "Zanj" kwa ajili ya eneo lilelile.
Katika karne ya 20 jina la Azania limefufuka tena. Nchi huru za Tanganyika na Zanzibar ziliungana tarehe 26 Aprili 1964 kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Jina jipya lilitafutwa. Hapo jina lile la kihistoria "Azania" lilikumbukwa tena; kwa kuunganisha maneno ya Tanganyika, Zanzibar na Azania jina la nchi "Tanzania" limepatikana.
Kwa namna tofauti jina la Azania lilitumika pia Afrika Kusini. Wakati wa siasa ya ubaguzi wa rangi sehemu ya wapinzani wa siasa hii hawakutaka kutumia jina rasmi la "South Africa / Zuid Afrika" tena. Walitafuta jina katika historia iliyotangulia kufika kwa Makaburu wakichukua jina la Azania. Ni hasa vyama vya PAC na Azanian People´s Organization waliotaka kubadilisha jina la Afrika Kusini kuwa Azania. Lakini chama kikubwa cha ANC haikukubali, hivyo mipango ilishindikana.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.