From Wikipedia, the free encyclopedia
Afraate (280 hivi[1] – 346; kwa Kiaramu ܐܦܪܗܛ — Ap̄rahaṭ, kwa Kifarsi فرهاد, Aphrahat, Aphrahas, Pharhad; kwa Kigiriki Ἀφραάτης; kwa Kilatini Aphraates) alikuwa mtawa maarufu kwa kuandika mfululizo wa hotuba ishirini na tatu juu ya mafundisho na maisha ya Kikristo kadiri ya mapokeo ya Kisiria, ambayo yalikuwa hayajaathiriwa na utamaduni wa Ugiriki wa kale.
Tofauti na Efrem wa Syria, aliyeishi ndani ya mipaka ya Dola la Roma kama Wakristo karibu wote wa wakati ule, Afraate aliishi nje yake, upande wa mashariki, katika eneo la Adiabene (Assyria, leo Iraq Kaskazini) lililokuwa chini ya Wasasanidi, Dola la Persia (leo Iran)hata akaitwa ܚܟܝܡܐ ܦܪܣܝܐ, Ḥakkîmâ Pārsāyā, "Mwenye hekima wa Persia".
Kabla ya hayo (336-345) hakuna mwandishi wa jamii hiyo isipokuwa Bardesane wa Edesa.
Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu.
Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 29 Januari, lakini wengine wanasema si mwenyewe, bali somo wake fulani, mkaapweke kutoka Uajemi ambaye alikwenda Bethlehemu na kuongokea Ukristo[2]. Baadaye akaishi katika nyumba ndogo nje ya mji wa Edessa. Mwishoni alikwenda Antiokia kutetea kwa maneno na maandishi imani sahihi dhidi ya Waario akafariki huko mwaka 378 hivi.
Akitokea katika familia ya Kipagani, alichukua jina la Kikristo Yakobo wakati wa kubatizwa,[3] jambo linalothibitisha kwamba jumuia yake ilifuata taratibu za Wakristo wa Kiyahudi.
Labda aliongoza monasteri ya Mar Matti karibu na Mosul na kufikia uaskofu[4].
Maandishi yake (yanayoitwa kwa Kilatini "Demonstrationes", kutoka jina la Kisiria "'Taḥwiyāthā") yanaonyesha alivyoguswa na dhuluma za serikali za Persia dhidi ya Wakristo wake, hasa baada ya adui yake, Kaisari Konstantino Mkuu, kuelekeza Dola la Roma kwenye Ukristo.
Hotuba zake zimepangwa kialfabeti, kufuatana na herufi 22 za Kisiria, ila ya 23 na ya mwisho ni barua inayowaelekea watawa wenzake "Wana wa Agano".
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.