From Wikipedia, the free encyclopedia
Ziwa Nyasa (katika Malawi: Lake Malawi; katika Msumbiji: Niassa) ni kati ya maziwa makubwa ya Afrika ya Mashariki likiwa na nafasi ya tatu baada ya Viktoria Nyanza na Ziwa Tanganyika.
Eneo la ziwa ni km² 29,600.
Lina urefu wa km 560 na upana wa km 50-80, likienea kutoka kaskazini kuelekea kusini. Vilindi vyake vinafikia hadi mita 704 chini ya uwiano wa maji yake.
Ziwa Nyasa linapatikana kati ya nchi za Malawi, Msumbiji na Tanzania.
Katika ziwa hilo kuna mito mbalimbali inayoingiza maji yake humo kama vile mto Lufilyo, mto Mbaka, mto Kiwila, mto Songwe n.k.
Kusini mwa ziwa unatoka Mto Shire unaopeleka maji kwenye Mto Zambezi na hatimaye Bahari Hindi.
Kijiolojia ziwa ni sehemu ya Bonde la Ufa la Afrika ya Mashariki.
Ziwa Nyasa linajulikana kuwa na aina nyingi za samaki (zaidi ya 1500). Aina chache tu zinavuliwa kama chakula, lakini aina mbalimbali zinakamatwa na kuuzwa nje ya Afrika kwa wapenzi wa samaki wa rangi.
Malawi lina ufuko mrefu ziwani upande wa magharibi na kusini, ilhali Tanzania inapakana na kaskazini mwa ziwa na kwenye ufuko wa mashariki, ikifuatwa na Msumbiji.
Kuna ugomvi kati ya Malawi na Tanzania kuhusu mipaka ndani ya ziwa. Mpaka baina ya Malawi (zamani: Nyassaland) na Msumbiji ulipangwa wakati wa ukoloni. Lakini kuna mzozo kuhusu robo ya kaskazini-mashariki inayodaiwa na Tanzania kuwa ni eneo lake, ilhali Malawi inaidai pia.
Malawi imedai ya kwamba maji yote hadi ufukoni upande wa Tanzania ni sehemu ya eneo lake la kitaifa. Tanzania imedai ya kwamba mpaka uwe katikati ya ziwa kufuatana na desturi za kimataifa.
Sababu ya mzozo ni maelewano ya kikoloni. Wakati wa kuanzishwa kwa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani lakini kabla ya serikali ya Ujerumani kuchukua koloni mkononi mwake[1], serikali za Uingereza na Ujerumani zilipatana kuhusu mipaka ya "eneo chini ya athira ya Ujerumani" ("German sphere of influence") kwa kutaja mpaka ulifuata ufuko wa Ziwa Nyasa.[2] Leo inajadiliwa baina ya wanasharia wa kimataifa kama maneno haya yalitaja mipaka halisi ya kiutawala au kama yalikuwa tu mapatano ya awali kuhusu "maeneo chini ya athira" ya nchi husika[3].
Baada ya mwaka 1919 Uingereza ilitawala Tanganyika pamoja na Malawi (Nyassaland), hivyo hakukuwa na shida.
Kabla ya uhuru, wakati wawakilishi wa TANU walichaguliwa tayari kuwa wabunge katika bunge la kikoloni (legislative council) na Julius Nyerere alikuwa waziri mkuu wa Tanganyika tangu 1960, mbunge Chifu Mhaiki alitaka serikali iangalie upya haki za Tanganyika kwa maji ya ziwa. Tarehe 12 Oktoba 1960 waziri mkuu Nyerere alijibu: "Hakuna shaka lolote kuhusu mpaka huu. Tunajua kwamba hakuna tone la maji kwenye Ziwa Nyasa ni mali ya Tanganyika kufuatana na mapatano haya. Hali halisi tungedai serikali jirani ibadilishe mipaka kwa manufaa ya Tanganyika." [4]. Chifu Mhaiki alirudia swali lake alipokuwa mbunge katika Bunge la Kitaifa baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1962 na safari hii waziri mkuu Rashidi Kawawa alijibu tena kwamba hakuna sehemu ya Ziwa Nyasa iliyokuwa ndani ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, kwamba Uingereza haikubadilisha mipaka hii na kwamba hata kama kuna hasara kwa Tanganyika serikali haiwezi kuanza majadiliano juu ya swali hili na Uingereza au serikali ya Nyasaland kabla ya uhuru wa nchi hii jirani[5].
Tarehe 3 Januari 1967 serikali ya Tanzania iliandika mara ya kwanza kwa serikali ya Malawi na kuifahamisha kwamba iliona mpaka baina ya nhci hizi ilifuata mstari wa kati wa Ziwa Nyasa. Malawi ilithibitisha kupokelewa kwa barua hii bila kuijibu rasmi. Hata hivyo rais Banda wa Malawi alikataa madai ya tanzania mbele ya bunge lake. Polisi ya Malawi ilijaribu kutawala wavuvi na feri za Tanzania ziwani. Mzozo huu ulisababisha risasi kufyatuliwa hadi kutulia mwaka 1968.
Hadi leo hakuna mapatano rasmi lakini nchi zote mbili zinaendelea kudai bila kutumia nguvu. Hali halisi Malawi imeheshimu dai la Tanzania, haijasumbua tena wavuvi wala feri za jirani ndani ya robo ya kaskazini-mashariki ya ziwa.
Mzozo ulifufuka tena tangu mwaka 2012 baada ya Malawi kutoa vibali vya upelelezi wa gesi na mafuta chini ya ziwa, tendo linalopingwa na Tanzania.[6]
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.