Waluguru
Makabila ya Tanzania From Wikipedia, the free encyclopedia
Waluguru ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi katika mikoa ya Morogoro na Pwani, hasa kwenye Milima ya Uluguru (Wilaya ya Mvomero) na katika wilaya ya Morogoro vijijini ukianzia Matombo kuelekea Dutumi hadi Bwakila Juu.
Kuna makundi makubwa mawili ya Waluguru. Makundi hayo ni Waluguru wanaoishi milimani na wale wanaoishi mabondeni.
Waluguru wa milimani wanapatikana katika maeneo ya Mgeta, Kolero, baadhi ya maeneo ya Matombo na Kiroka, na pembezoni mwa Milima ya Uluguru hasa ile ya Tao la Mashakiri.
Upande wa dini, kwa kawaida wale wanaoishi mabondeni ni Waislamu na wale wa milimani ni Wakristo, hasa wa Kanisa Katoliki. Siku hizi hata mabondeni kuna Wakristo wengi na milimani pia kuna mchanganyiko.
Waluguru wa milimani ni wahanga wa masimulizi ya "mumiani" kiasi kwamba mpaka sasa huweza kuwahusisha wageni na hao "mumiani".
Kama Wasambaa, Wazaramo, Wakaguru, Wakutu na Wakwere, kabila hilo linafuata mfumojike (kwa Kiingereza ''matrilinear'') yaani ukoo wa mama ndio unaoongoza familia na watoto wote wanahesabiwa kuwa wa ukoo huo. Hata hivyo, mtoto wa Kiluguru huitwa jina la ukoo wa baba yake, ambao ndio ukoo wa bibi mzaa baba. Yaani: Waluguru wana 'mtala' na ukoo. Mtala ni jina la ukoo wa baba ambalo ndilo analoitwa mtoto. Kwa mfano: mtoto akiitwa 'Kobero' jina hili ni mtala, si jina la ukoo wake, kwani 'Kobero' ni jina analopewa mtoto ambaye baba yake ni 'Mmadze'. Hali kadhalika, mtoto akiitwa 'Mkude' jina hili ni mtala wa ukoo wa 'Wamwenda', lakini si jina la ukoo wa mtoto. Hivyo basi, kwa Waluguru baba hutoa jina na mama hutoa ukoo: jina ni la ukoo wa baba, na ukoo ni wa mama!
Waluguru wanapenda kuishi pamoja na kushirikiana. Pia hupenda kunywa pombe na kushiriki kwenye sherehe za kimila.
Utamaduni na mila zao hufahamika sana katika suala la kucheza ngoma za asili kati ya Oktoba na Januari, hasa wale wanaoishi katika vijiji vya Longwe, Tegekelo, Mgeta, Kumba, Singisa, Bwakira, Kolero, Nyamighadu na vinginevyo vingi.
Masuala ya jando na unyago yalikuwa ya kawaida sana kabla ya miaka ya 1990. Hata hivyo, maingiliano ya kijamii na kupanuka kwa elimu kumefanya shughuli hizo zisipewe kipaumbele tena.
Mpaka hivi karibuni jamii hii ilikuwa haitilii maanani sana suala la elimu na ndiyo maana idadi kubwa ya Waluguru hawana elimu ya kutosha.
Vyakula vya asili ni magimbi, matuwi na mahimbi pamoja na mihogo.
Waluguru ni maarufu kwa kilimo cha magimbi na wana aina kadhaa za magimbi. Aina mojawapo ni ile ya 'mahimbi' ambayo huchukua muda mrefu kuiva. Iwapo aina hii ya mahimbi italiwa mapema kabla ya kuiva kabisa, mlaji atawashwa midomo na ulimi. Hivyo basi, mpishi hupaswa kuwa mvumilivu kwa masaa kadhaa kabla ya kuepua chungu cha mahimbi na kuyala.
Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Waluguru kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
Wikiwand in your browser!
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.