From Wikipedia, the free encyclopedia
Wabondei ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi katika wilaya ya Muheza, Mkoa wa Tanga, karibu na Milima ya Usambara. Lugha yao ni Kibondei. Mwaka 1987 idadi ya Wabondei ilikadiriwa kuwa 80,000 [1].
Wabondei ni miongoni mwa watu wenye asili katika kabila kubwa lililojulikana kwa jina la Waseuta. Baada ya hao kupigana na Wareno na kuwashinda katika vita vikali vilivyojulikana kwa jina la "Nkondo ya kutula nyala" (Vita ya kuvunja mawe ya chakula), Waseuta walianza kugawanyika kwa kujimega makundimakundi na kuondoka. Makundi hayo ndiyo makabila yenye asili ya mkoa wa Tanga kwa sasa, isipokuwa Wadigo si miongoni mwa Waseuta [2].
Wabondei ni kundi la nne la Waseuta ambao, baada ya kuwapiga Wareno, waliondoka Handeni kwa lengo la kurudi pwani, yaani Umba, ambapo walikutana na vita vya wavamizi wapya kutoka Kenya ambao si Hettio Aramaio. Wavamizi hao walikuwa Wadaiso, Wasegeju na Wadigo. Vita hivyo vilikua vigumu sana kwa kundi hili la Waseuta kwa kuwa lilikuwa dogo kulingana na idadi ya wavamizi. Kutokana na ugumu wa vita hivyo, wazee wa mila walilazimika kutambika kwenye mlima wa Mlinga, na inavyoaminika baada ya kutambika huko ilitokea mizimu ya Waseuta waliokufa vitani wakati wa mapambano ya Wareno na mizimu hiyo ndiyo iliyopigana na wavamizi ambapo Wadigo Wadaiso na Wasegeju walipigwa vibaya sana na kuuawa. Waliobakia hai wakatekwa na Waseuta hawa.
Kutokana na hofu ya vita hivyo “Nkondo ya kivindo”, Waseuta hao waligawanyika na kusambaa tena, ambapo wengine walifika katika mji wao mkuu wa zamani ulioitwa New Fort-Umba au Umba Mpya Ngomeni, waliishi maeneo mbalimbali hata kufika pPwani kama Tanga ambayo iko chini ya Umba ya zamani ambako ni Horohoro mpaka sehemu za Kenya.
Vilevile Waseuta hao walisambaa kutoka mji mkuu wa zamani yaani Umba na sehemu za Mbwego, ambako leo huitwa Magila, pia waliishi maeneo ya Mkuzi ambako kulikuwa na fundi maarufu wa kucheza njuga aliyeitwa Saudimwe na mwanae Kidungwe, walisambaa sehemu za Jaila ambako ndio Misozwe leo, Bwembwera na Tongwe. Pia Waseuta hawa walifika sehemu za Amani: hapo kundi hili la Waseuta walibadili jina na kujiita Wabondei yaani “Valley Peoples” (Watu wa mabondeni). Mji wao mkuu kwa sasa ni Muheza.
Baada ya vita kumalizika kila familia ilikuwa na umuhimu mkubwa wa kujihami katika maisha inayoishi, hivyo kila mzee wa familia alilazimika kujenga gwegwe na kuishi humo yeye na familia yake. Gwegwe ni uzio mkubwa wa magogo manene unaojengwa kwa kuzunguruka nyumba kadhaa za familia moja ambapo nyumba za familia zinakuwa ndani ya uzio huo, halafu mbele ya gwegwe hilo kunakuwa na lango kubwa la kuingilia. Huko wanafamilia yenye gwegwe hilo wanamuita mganga ambaye anakuja kuweka fingo na mazindiko ili kuzuia watu wenye nia mbaya kama wachawi, wezi, wanaotaka kuleta vita n.k., washindwe kuingia kwenye lile gwegwe. Kila gwegwe moja lilikuwa likiishi familia nzima, babu (baba), wanae wote, wajukuu na hata vitukuu.
Vilevile mtoto wa kiume akitaka kuoa alikuwa na uhuru wa kwenda kuanzisha gwegwe lake kwenye eneo atakalolichagua na haya magwegwe yalikuwa yakiitwa kwa majina ya watu, mfano kwa Sempapayu, kwa Sekiinga n.k. Hivyo magwegwe haya ndiyo asili ya kuanzishwa kwa vijiji vya bonde.
Kimaisha kila mwenye gwegwe alikuwa amezungurukwa na shamba lake kwa ajili ya kilimo, pia kulikuwa na ustaarabu wa kubadilishana mashamba ambapo mtu aliweza kuomba shamba kwa msimu wa kilimo na mwenye shamba akamruhusu alime msimu ule, na alieazimwa shamba analima na baada ya mavuno anarejesha shamba. Shamba hili linaporejeshwa kama aliyeazimwa alipanda miti ya matunda kama mifenesi n.k. inakuwa mali ya mwenye shamba. Kwa ustaarabu huo hakuna historia inayoonyesha kuwa taratibu hizo ziliwahi kuleta usumbufu wa namna yoyote.
Wageni wanapotaka kuingia kwenye gwegwe la familia fulani wanasimama kwenye lango la gwegwe hilo, lango ambalo linakuwa umbali mkubwa na nyumba za familia zilizopo ndani ya gwegwe hilo na hapo mgeni ndipo hupiga hodi na wenyeji wanatoka na kumhoji mgeni huyo kabda ya kumkaribisha. Taratibu za kumhoji mgeni zinafanyika kwa kuhofia kuwa mgeni yule akawa ametumwa kupeleleza na baadaye alete vita. Akionekana kuwa ni mgeni wa kheri, na ukoo alioutokea unajulikana, ama amejieleza vizuri, sasa ndipo anapokaribishwa. Ikitokea mgeni amebainika si mtu mzuri, na pengine amekuja ili kuleta vita, hapo linapigwa gunda (kitu mfano wa pembe linalopulizwa na kutoa sauti ya ishara ili kuwaita Wabondei wote) ama inapigwa ngoma maalumu kama mbiu ya kukusanya Wabondei wote, na hapo vinatokea vita baina ya Wabondei na watu wa jamii ya yule mgeni. Endapo havitatokea vita, mgeni yule wa shari anapigwa na Wabondei kipigo kikali, kisha anaachiwa aondoke zake.
Kwa upande wa wanaume, vazi kubwa ni shuka ya kiunoni (msuli) pamoja na shati, hili ndio vazi kuu la asili ya Wabondei, japo zama za kale walikuwa wakivaa ngozi za chui, simba na wanyama wengine.
Kwa upande wa wanawake, vazi lao kuu la asili ni kaniki na gunya (gunya ni vazi la kienyeji lililo mfano wa kitenge kwa mpangilio wa rangi). Vilevile wanawake wa Kibondei wana asili ya kutoboa masikio yao kwenye ufito wa mwisho wa sikio, wanatoboa kuzunguruka ufito wote vitundu vidogovidogo. Vitundu hivyo wanaviita "utango", kisha wanavaa njewe na mapete. Wanachukua karatasi za Galabosi zinazong’aa, mfano wa karatasi ya ndani kwenye pakiti ya sigara, kisha wanazisokota, zinakuwa nyembamba zilizo mfano wa nyota na mwezi, nyota rangi yake na mwezi rangi yake, kisha wanavaa masikioni.
Vile vile walikuwa wakivaa mikufu na pete za Rupia ambapo walikuwa wakichukua Rupia (hela ya zamani ya Mjerumani iliyokuwa na tundu katikati) kwa kutengeneza pete walitumia sarafu ya Rupia na kisha wanaitengenezea ringi na kuvaa vidoleni. Kwa upande wa mkufu walichukua kamba nzuri kisha wanaingiza zile sarafu na kuvaa.
Endapo kumetokea ugomvi na mtu akampiga mwenzake kiasi cha kumtoa damu Yule aliempiga mwenzie anatakiwa kutoa malipo ambayo ni mbuzi, Mbuzi Yule anapikwa supu kisha ndugu na wazee waliosimamia ile kesi wanakunywa mchuzi.
Endapo aliepigwa hajatoka damu, Mtu aliempiga anatakiwa kulipa faini inayojulikana kwa jina la “Sugusa” (Sugusa uhee/Usuguse mazi - Ukome uache kabisa) Hapa anatakiwa kulipa kiasi cha pesa ama kitu chochote.
Kawaida yanapotokea majanga kwa mtu ama watu, watu wa eneo lile wanawachangia wahanga ili kuwasaidia, Walikua wakitembea kila nyumba kuchangisha hela, mazao nk kwa ajili ya kuwasaidia wahanga.
Mgeni anaetambulika kuwa ni wa kheri katika jamii ya wabondei ndani ya gwegwe aliloingia anakamatiwa jogoo mkubwa anakabidhiwa Yule mgeni nakuambiwa mboga yako hiyo, kisha Yule mgeni anamchinja mwenyewe Yule jogoo na wenyeji wanampikia wanatoa miguu na kichwa tu lakini kuku mzima anapewa Yule mgeni pamoja na chakula anaandaliwa ale, Endapo atam bakisha Yule kuku kinatafutwa kikapu kizuri kisha anahifadhiwa Yule kuku na muda ambao Yule mgeni anaondoka anakabidhiwa kile kikapu anaondoka nacho.
Namna ya kukirudisha kile kikapu cha zawadi: Mgeni Yule eidha akirudishe mwenyewe ila mara nyingi familia ile iliyotoa kile kikapu ikitembelea familia ile iliyopewa kikapu na wao wanawekewa zawadi katika kikapu kile kile (Zawadi hii eidha iwe ni kuku ama kitu chochote kile) kwakua haikuwa sheria ya kubakisha jogoo unaekabidhiwa kama karibu ya mgeni.
Wabonnei nao kama ilivyokua kawaida ya makabila mengi ya kale walikua na kawaida ya kubadilishana mali fulani kwa mali fulani mfano Ndizi kwa Makopa ya mihogo nk, ila baada ya mfumo wa manunuzi kwa njia ya pesa ulipoingia ndipo mila ya mabadilishano ilipoisha na kuanza kutumia manunuzi kwa kutumia pesa.
Kabda ya yote kijana anapotaka kuoa ndani ya familia yake wanaulizana nyumba anayotaka kuoa ni ya nani kisha baadae anatumwa mzee anafanya uchunguzi hasa kwa mambo makuu matatu ambayo wabondei ukoo ukiwa na moja kati ya mambo hayo ama yote huwa ukoo huo watu hawaoi pia hawaolewi
Baada ya kuona kuwa ukoo wanaotaka kuoa hauna matatizo hayo sasa wanatazama kolwa la binti anayetaka kuolewa (kolwa ni asili alipotokea babu wa familia fulani katika bonde) na mbondei ilikua asipojua kolwa la binti anaetaka kumuoa basi hatomuoa tena kwa kuwa mbondei ambae asipotaja kolwa lake alikuwa akiitwa mtumwa na alichukuliwa kuwa atavuruga ubondei.
Baada ya kila upande hasa hasa upande wa mume kuridhika na ukoo wa mwanamke na kukubaliana sasa wanafanya safari kwa mwanamke, ambapo wanakuwa wamebeba Debe la pombe lililokuwa likijulikana kwa jina la Debe da umbuya (Debe la urafiki) Debe hili ndani linakuwa na pombe ya mnazi ama pombe ya mapumba, Wanakaa sasa na kuongea huku upande wa mke wakiwa wanakunywa ile pombe, Hapo sasa upande wa kwa mume wanatajiwa vitu vya kuleta ili ndoa iweze kupita, Vitu vilivyokuwa vikiagizwa sana kwa wakati huo ni:
Siku watakayoleta hivyo vifaa, endapo vikipokelewa basi hapo ndoa ipo, la havikupokelewa basi hapo wanarudi navyo na ndoa inakuwa hakuna.
Taratibu ya kuvipokea: wageni wanaokuja wanapiga kelele na kuuliza “Jamani wia ukundwa?” (Harusi imekubaliwa?) wa kwa mke wanaitikia kwa kusema “Ukundwa” (Imekubaliwa) Baada ya hapo wa kwa mke wanatoka na kusimama kwenye mlango kisha wa kwa mume wanasimama mbali kiasi halafu wa kwa mume wanapiga kelele wakisema Hougai (Ho ugali?) wa kwa mke wanajibu “Ho mguio” (Mumempata mtu wa kumtuma/sokoni/ kuwapikia) Huku kila upande wakikimbia na kukutana katikati mara kadhaa kisha wanazomeana “Haoooooooo…” Wanacheka na kupiga vigelegele hapo ndio imeshakubalika sasa Ndoa inaanza kufungwa siku ileile
Siku ileile mwali wa kike anachukuliwa anawekwa ndani akiwa na kungwi wake ambae kungwi huyu ndie anaekuwa akimfundisha mambo kadhaa awapo kwa mume wake, humo ndani kunakuwa na mtungi wa asali pamoja na ndizi kibungaa zilizoiva (Ndizi kibungaa ni zile ndizi ndogo ndogo ambazo wengine huziita bungala) Mwali anapowekwa ndani anakuwa na miko ambapo mwiko mkubwa hatakiwi kula chakula chochote wala kunywa kinywaji cha aina yoyote ile hadi zitimie siku tano, na hizo ndizi na asali amewekewa ili aweze kupimwa imani yake ijulikane kuwa kweli mke yule ni mvumilivu na ana huruma kwa mume wake? Kwa kua endapo mwali Yule atakula chochote kati ya vile alivyowekewa pale ndani basi mwanaume anaetaka kumuoa huko aliko analegea na kuanguka, Familia ya mume wakijua kuwa mwanamke amekula kabda ya siku tano wanakwenda kuwasema familia ya mke kuwa mwana wenu hana imani na mtoto wetu maana amekula na kupelekea mtoto wetu ameanguka, hapa mwanaume anakua na hiyali ya kumuoa Yule binti ama kumuacha. Kwa upande wa mwanaume siku tano hizo nae pia anakuwa katika sheria ya kutokula, vilevile ilikua akila tu basi mke wake anaanguka.
Siku ya tano inapofika ngoma za kibondei zinakesha, Asubuhi ndugu wa kwa mume wanakuja huku wakiimba Nkondo wakiwa na Fimbo na mapanga wanacheza mduara huku ngoma zikipigwa, Baada ya hapo mume anaingizwa ndani ili kuandaliwa huku nje inapigwa ngoma ya maumbu ambapo wanawake wawili mmoja anajifanya mwanaume na mavazi ya kiume mwengine anajifanya mwanamke, huyu mwanamke anakuwa amebeba kikapu kisha anaigiza kuwa anatoroka anaingia kwenye nyumba Fulani kisha huyu anaecheza kama mwanaume anajifanya akimtafuta mke wake, Kila nyumba anauliza “Jamani hamjamuona mke wangu hapa” wanamjibu “Hatuja muona” Baada ya kutafuta na kuuliza sana ndipo wanapomuambia tumemuona kaingia nyumba ilee..(Kaingia nyumba ida) Anamfuata anamuona anamshika mkono na kutoka nae huku wakipigiwa vigelegele (Igizo hilo kwenye Ngoma hii ya maumbu linawafundisha wanaume kuwa mke akitoroka usimsuse, mtafute umrudishe).
Baada ya sehemu hiyo kupita vinawekwa viti nje kisha maharusi wanatoka na makungwi wao (kungwi ni wapambe wa maharusi) kama kuna viti vinne wote wane wanakaa laa kama kuna viti viwili wanakaa maharusi peke yao na makungwi wanasimama, hapa watakuwa wakiwatazama watu huku ngoma ikipigwa, kama wana mavazi ya kutosha wanaweza kuingia na kubailisha mavazi wakatoka tena hadi mara tatu kisha sasa wanaingia ndani hapo itapigwa ngoma ya kimbungumbungu na bibi harusi peke yake atatolewa na kuzunguruka nyuma ya nyumba ambapo ni ndani ya uzio, Kama huyu bi harusi ni Bikra hapo kila anaeitwa mama, awe mama, mama mdogo ama mama mkubwa watalala kifuifudi chini kwa kujipanga kisha huyu binti atapita juu ya migongo ya mama zake bila kukanyaga chini kuku akicheza kimbungu mbungu, Tukio hili kimila wanaolishuhudia ni mabii wa bibi harusi, mama zake na wale watu wazima wanaopiga ile ngoma, watoto hawaruhusiwi kabisa kuona, Baada ya kimbungu mbungu kukamilika sasa binti Yule anaingizwa ndani anavalishwa nguo vizuri kisha kabda ya kuondoka kwa mume wake anahamishwa nyumba kisha wamama wanaitwa ili wakamfunde mwali ambapo walikuwa wakimuelekeza heshima na namna ya kuishi huko anakokwenda, akiwakuta ndugu wa mumewe ndio ndugu zake pia, mama wa mumewe nae ni mama yake, na namna ya kuitikia huko anakoenda kwa mfano atapewa jina na kuitwa mama fulani basi akiitwa aitikie “Yo mame” baada ya kumfunda mwali hapo sasa anakabidhiwa kwa mume wake na ndoa inakua imekamilika. Ndoa yenyewe hasa ni pale mwanamke anapoweza kuvumilia kukaa na njaa awapo ndani siku tano akifikisha tayari ndoa inakuwa imekamilika.
Baada ya mzazi kujifungua anawekwa ndani huku watu wanaokuja kumuangalia wakilazimika kumchotea maji, Sharti katika kuchota maji ya mzazi safari za kisimani zianzie mbili na kuendelea isiwe moja kisha ndio wanampatia mzazi zawadi yoyote ambayo mtu ameweza kuwa nayo.
Wakati mzazi akiwa ndani kabda ya siku saba kunakuwa na kikapu kidogo (Tezu) ambacho kinatumika kuhifadhia kinyesi cha mtoto huyo, kinyesi hicho hakitolewi kutupwa nje hadi zikamilike siku saba, Baada ya siku ya saba ile haja ya motto inatupwa kisha kikapu kile kinawekea unga kwaajili ya kutumika kumpatia mtoto Yule jina, Mzazi anatolewa nje pamoja na kile kikapu akiwa na wakunga wake ambao ni mabibi, mzazi Yule anakaa juu ya kiti akimpakata mwanae kisha bibi wa mtoto anachukua unga kwa vidole viwili vya kila mkono wake kutoka kwenye kile kikapu kisha anamshika mtoto masikio kwa vile vidole vyenye unga anamwambia “wewe ndie Fulani” (Anampa jina) Kisha anamchukua Yule mtoto anamuelekezea upande lilipo jua anamwambia “Huku juani ukatafute” Kisha anamuelekezea linapozama jua na kumuambia “Huku linapozama jua ukatafute” (Anamgeuzia pande zote nne za dunia) na kumwambia kuwa magharibi ukatafute, mashariki ukatafute, kusini ukatafute, Mashariki ukatafute, Mungu ametoa uwanja huu ukatafute kwa kheri. (Japo pia inasadikika wapo baadhi ya wazee waliokuwa wakiwaambia watoto kuwa “Mungu ametoa uwanja huu ukatafute kwa njia zote”) Baada ya hapo ule unga kwenye kile kikapu (Tezu) unachukuliwa na bibi anakwenda kuutumia kwa matumizi ya kawaida ya chakula.
Kawaida katika bonde ilikua nyumba Fulani inapopata msiba wanatangaziwa kijiji chote, Hapo kila wageni wakija kwenye msiba wanakuja na vyakula vyao, wale wa karibu wanapika kabisa na wambali wanabeba kwaajili ya kuja kupikia pale pale ili mradi msibani kusiwe na shida kiasi kuwafanya wafiwa wasihangaike na chakula cha wageni zaidi ya kujua msiba tu.
Baada ya mazishi siku ya pili kunatokea tukio wanaloliita “Uda ugai” Wabondei wa sasa wanaliita “Mafumbi” Hapa wanakutana ili kujadili namna ambavyo wataumaliza msiba, Hapo watachangishana kutokana na mahitai kisha siku ya tatu wanakuwa wameshajua wanunue nini na siku yanne ni ukaa, ambapo alfajili ng’ombe anachinjwa.
Taratibu za kuchinja Ng’ombe huyo ni lazima anaechinja atokee upande wa baba maana akitokea upande wa kwa mama atachukua nyama nyingi. (Taratibu hii imewekwa pia kutokana na choyo kwa kuwa wabondei wanayo asili ya choyo) Na kawaida kichwa cha huyu ng’ombe kinachukuliwa na mchinjaji.
Baada ya hapo wapishi ni familia iliyooa kwenye familia iliyofiwa nikimaanisha Mashemeji, wakwe, mawifi na wengineo ambapo wanaume wanapika nyama na kukuna nazi kisha wanawake wanagawiwa mchele na wao wanapika vyakula kwenye vyungu.
Kama marehemu alikua ameoa ama kuolewa Linaandaliwa tambiko la kimila ambalo linaitwa kucha au mkucha ambapo mtu anachuku jembe na kikapu kisha panakokwa moto, mtu Yule anakwenda kujificha akishajificha anagonga lile jembe kidogo kisha anasema “Mkucha mkucha” mwengine anaitikia “Eehee” Yule mtu anasema tena “Fulani kafa” (Kwa kulitaja jina la aliekufa) Yule muitikiaji anauliza “Kafa?” kisha “kaolewa/kaoa wakati gani?” Yule mtu anautaja ule wakati “Wakati Fulani” Muitikiaji anauliza tena “Mahali kalipa?” atajibiwa kuwa amelipa ama hajalipa kisha watauliza madeni yake ya ndoa tu na atauliza pia alioa wake wangapi atajibiwa katika mfumo huo huo, ana watoto wangapi.. atajibiwa baada ya ukucha kumalizika sasa inafuata Ngoma ya Tindia na kisha Ngoma ya ukaa
Usiku kuna kukesha na ngoma ya ukaa: watu wanapiga ngoma na kuwa na nyimbo tofauti tofauti ambapo wanaamua muda huu wawalize wafiwa, basi wataimba kiasi wafiwa watalia mpaka basi; ila wanapoamua kuwa muda huu tuwachekeshe wafiwa wanaimba nyimbo ambazo wafiwa watacheka mpaka basi. Sababu hiyo ndiyo iliyopelekea ngoma ya ukaa kuondolewa kwa haraka baada ya ustaarabu wa dini kuingia.
Kama ilivyo kawaida kwa jamii nyengine duniani pia jamii ya wabondei wanazo desturi za kugawa mali za marehemu kwa ndugu watoto na mke ( mirathi).
Katika desturi za Wabondei wakati wa ugawaji wa mirathi wanaosimamia swala zima la ugawaji wa mirathi ni upande wa baba wa marehemu, Kidesturi mali kama mazao na nguo hugawiwa kwa mafungu mawili yaani kwa mama na kwa baba ambapo anatoka mtani wa kabila anachagua nguo moja anaweka kwenye fungu la kwa baba kisha nguo nyengine anaweka kwenye fungu la kwa mama, Anafanya hivyo hadi mazao na nguo zote zinamalizika.
Kwa upande wa mashamba ya marehemu yanakatwa vipande viwili kwa baba kimoja na kwa mama kimoja na kila mtoto atapewa kipande chake, Kama marehemu ameacha nyumba moja hii inakuwa upande wa baba wa marehemu ambao wao watawatunzia watoto wa marehemu (kama ni wadogo) ama kama ni wakubwa watawapatia wao hiyo nyumba.
Warithi wakuu katika Desturi za kibondei ni Watoto na Mke/wake ila kama Marehemu hakuwa na watoto Basi mali zake atapewa mke na nyengine ndugu watagawana, Ki Desturi endapo mjane wa marehemu alikuwa ameishi kwa amani katika familia ya mume wake anaweza kuendelea kukaa hapo bila tatizo lolote pamoja na mali alizopewa na wanae kama ni wakubwa wataendelea kumlea hapo ama kama ni wadogo atawalea hapo, Ila kama Mjane hakuwa akiishi kwa amani katika ile familia basi hapo ndugu zake watamchukua na kuondoka nae. Kipindi hicho hakukua na utaratibu wa Eda kama ilivyo sasa.
Hii ndiyo ngoma kuu ya Wabondei na inapigwa kila kwenye sherehe. Ki uchezaji ngoma ya mnyanyuo. Kwa upande wa mavazi wanaume wanavaa vazi la aina moja kisha wanashika fimbo ama panga, na wanawake nao wanavaa vazi la aina moja kisha wanashika vitambaa, wapigaji wa ngoma hiyo wanavaa kofia za mbega, kofia hii ni lazima iwepo katika ngoma (Kofia ya mbega inatengenezwa kwa ngozi ya mbega)
Ntambo ya muheza niuzani nmyambie, kubua he daaja mamng’anya atunguka katoza mgosi ya npeege kamvokea he ziso funda mwenga imema mkate kamgea he gwaha kwandua kumshindaa, Samaki mgima nae kamgea he gwaha kwandua kumshinda, Kichachiwa kichachiwa nseue makang’ka Samaki mzima nae kamgea he gwaha kwandua kumshinda, Wabwanga tikaue namnae Tikaue namnae…. Tikaue namnaae eeh namnae
Tafsiri: (Safari ya Muheza niulizeni ni waambie kufika kwenye daraja mwanamke asiejitambua anatelemsha, kashika perege mkubwa anakula kamuanzia kwenye jicho huku shavu moja limejaa mkate na samaki mwengine kamtia kwenye kwapa kuongeaa kumemshinda, akicheua anacheua samaki kuongeaa kumemshinda Jamani tuangalieni mandhari yanayopendeza.
Shime ni ngoma ya kishujaa, inapigwa kwenye sherehe hata msiba pia, Wachezaji wa ngoma hii wanavaa njuga na wanaweza kutembea umbali mrefu sana huku wakicheza ngoma hiyo,
Hii ni ngoma inayopigwa katika sherehe za wanawake tu. Hata kama ikipigwa kwenye harusi inapigwa uani na kuhudhuriwa na wanawake pekee
Hii ni ngoma ya vijana, wasichana na wavulana, Ngoma hii inapigwa kwa makopo, Namna inavyochezwa, wanakaa wanaume upande wao na wanawake upande wao, wakati wa kucheza ngoma hiyo anatoka mvulana huku akicheza anaelekea upande wa wasichana anamchagua msichana anaempenda (Wanaita kuchagua chambi) anarudi nae hadi kwa wavulana huku wakicheza kisha Yule msichana anamchagua mvulana nae anaenda nae hadi kwa wasichana huku wakicheza na Yule mvulana anamchagua tena msichana inakuwa ndio mtindo wa uchezaji katika ngoma hiyo, Wapigaji wa ngoma hii ni wanaume.
Kwa kawaida inapopigwa Ngoma ya Ukaa na Tindia ni lazima ifuatie, Hizi ni ngoma za msiba ila pia Tindia ni ngoma ya Matambiko ya kibondei Vilevile ngoma hii ya ukaa inapigwa wakati wawindaji wakienda kuwinda wanyama, katika shughuri zao za kuwinda wakipata wanyama bunduki zao zinamwagiwa unga,
Kama ilivyo ada kwa maeneo mengi hasa vijijini kunakuwa na imani za kishirikina, kwa upande wa Wabondei pia imani hizo zilikuwepo.
Uchawi uliokua ukiogopeka sana bonde ni Usinga, Uchawi huu mume anamtegea mke wake na inapotokea mke Yule kutoka nje ya ndoa basi mwanaume atakaetembea nae huanza kuumwa na kidole cha mguu, kuugua kidole ni kama kumchanganya mgonjwa na wakati akitibu kidole kumbe utumbo wake tumboni unakatika vipande vipande na mwisho anautoa kwa njia ya haja kubwa nayeye anafariki.
Uchawi huu endapo alierogwa amerogwa kwa kuonewa (Hakumchukua mke wa mtu) Basi akiaguliwa na mganga anaweza kupona, Lakini kama alierogezewa amemchukua kweli mke wa mtu hawezi kupona ugojwa huu ni lazima afariki.
Kazi za asili za wabondei ni kulima, kuchunga mbuzi na kuwinda, hasa wawindaji huwinda ndezi.
Kipindi hicho serikali za makabila mengi zilikuwa zikiongozwa na mitemi (Watemi) ama machifu, lakini Wabondei wao hawakuwa na kiongozi wa kabila lao kwa kipindi hicho ukimtoa seuta ambae ki historia alikuwa kiongozi wa waseuta kabda ya waseuta kugawanyika na kutoa makabila kadhaa wakiwemo wabondei.
Wabondei hawakuwa na kiongozi kutokana na choyo, kujiona pia kujivuna kwa kila mtu akitaka awe yeye zaidi ya mwenzie, Kuna kipindi wazungu waliwataka wabondei wawe na kiongozi wao ili wakifika wajue nani watakaeongea nae na huyo aweze kuwafikishia watu wake, Lakini pale wazungu walipowaita wabondei ili wachague kiongozi wao wabondei wote walifika wakiwa wamevaa vilemba na kila mmoja akataka achaguliwe yeye kitu kilichopelekea wazungu kumleta Ashrafu Mohammedi ili awe kiongozi wa Wabondei, Ashrafu alikuwa mmbugu hakuwa mbondei na alijulikana kwa cheo cha Jumbe mkuu nae aliishi eneo la Muheza ikawa ndio maskani yake na makao yake makuu, Kiongozi huyu hakuwa akijua kusoma wala kuandika wakati kipindi hicho tayari elimu ilishaanza kuingia ubondeini Baadae wazungu wakamchukua jumbe mkuu ashrafu na kumpeleka ulaya hata hivyo aliporejea alikuwa bado hajui kusoma wala kuandika, Baadae Ashrafu akaachia ngazi ya uongozi katika bonde
Baada ya wabondei kuona kuwa kujivuna kwao ndio tatizo la kutawaliwa na mmbugu wakaamua kukaa vikao na kupanga wamchague kiongozi wao kutoka kwa wabondei wenyewe, Wakamteua Erasto mang’enya ambae kipindi hicho alikuwa balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Marekani, Kiongozi huyu ki mila aliitwa Mtema wa bonde na mkewe (Mwashiti) aliitwa 'Mamweta.'
Utawala wa Mtema unakadiliwa kuwa ulipita kwenye miaka ya (1946) Siku ambayo Mtema wa bonde alitawazwa ilifanyika sherehe kubwa sana Muheza, watu mbali mbali walialikwa na hapo Erasto Mang’enya akatawazwa na kuambiwa kuwa huyu ndie atakuwa mtawala wa bonde, Mtema alivaa Kaniki na Lubega kisha akakabidhiwa Uta (Upinde), Ngao, Fimbo, Mbuzi, Ng’ombe, Kofia ya Ngozi ya Mbega, wakamvalisha Ngao na Ngozi ya Chui (Mgosi asui) kisha wakaita “Mgosi asui” yeye anaitikia “ Nawezwaangu”.
Baada ya hapo mkewe nae alipandishwa juu ya lile jukwaa na kukabidhiwa kinu. Mchi, Chungu, Ungo, akavalishwa Shanga ya asili (Shanga) na kuitwa 'Mamweta' (Mamweta ni cheo cha mke wa Mtema)
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.