From Wikipedia, the free encyclopedia
Utatu au Utatu mtakatifu ni hali ya kuwa Watatu katika umoja kamili.
Jina hilo la kiteolojia linatumika hasa kufafanulia imani ya Wakristo wengi kwamba Mungu pekee, sahili kabisa, ni Nafsi tatu zisizotenganika kamwe: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.
Kwa agizo la Yesu watakaomuamini wanatakiwa kubatizwa kwa jina la hao watatu (Injili ya Mathayo 28:19). Agizo hilo la mwisho lilifuata na kujumlisha mafundisho yake mbalimbali kuhusu Baba, kuhusu yeye mwenyewe kama Mwana na kuhusu Roho Mtakatifu.
Umoja wa Nafsi hizo unatokana na asili yake pekee, yaani Baba ambaye ndani mwake anamzaa milele Mwana kama mwanga toka kwa mwanga, kama Neno au Wazo lake (Hekima), tena anamvuvia Roho Mtakatifu kama Upendo ambao unamuunganisha na Mwana na kukamilisha umoja wao[1].
Kimsingi ni kwamba Mungu pekee (Baba) anajifahamu milele (Mwana) na kwa kujifahamu anajipenda (Roho Mtakatifu).
Imani hiyo ilizidi kufafanuliwa hasa katika karne IV, mitaguso mikuu ya kwanza ilipochukua msimamo dhidi ya wazushi waliokanusha umungu wa Yesu na wa Roho Mtakatifu. Ilipata muundo wa kudumu katika Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli inayotumika hadi leo katika madhehebu mengi ya Ukristo.
Kwa imani hiyo tunapaswa kusadiki hasa Utatu wa Mungu pekee, kwamba ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Milele yote Baba kwa jinsi alivyo ndani mwake anamzaa Mwana na kumvuvia Roho Mtakatifu, kama vile jua linavyotoa mwanga na joto lisitenganike navyo. Mwana, ambaye “ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake” (Eb 1:3), alisema: “Nimekuja kutupa moto duniani” (Lk 12:49). Naye Roho aliwashukia wafuasi wake “kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu” (Mdo 2:3-4).
Mungu hagawanyiki hata kidogo, bali daima ni Umoja kamili. “Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja” (Mk 12:29). Tumuabudu yeye peke yake katika nafsi tatu, na Utatu wa nafsi katika Umoja wa hali yake, tusichanganye nafsi wala kugawa Umungu. Baba si Mwana wala Roho Mtakatifu. Mwana si Baba wala Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu si Baba wala Mwana. Lakini milele yote nafsi hizo tatu ni Mungu yuleyule pasipo tofauti ya kuzitenganisha: kila moja imo ndani ya nyingine. “Mimi na Baba tu umoja” (Yoh 10:30).
Tumejua kuwa Mungu ni Umoja wa nafsi tatu kwa sababu Baba aliwatuma kwetu Mwanae na Roho Mtakatifu. “Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake. Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, ‘Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye’” (Math 3:16-17). Naye akaagiza, “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu” (Math 28:19). Ni nafsi tatu zenye jina moja, yaani Umungu mmoja tu.
Umoja wa Mungu unategemea hasa kwamba Mwana na Roho Mtakatifu wanachanga Umungu wa Baba, ambaye wanatokana naye pasipo utengano wowote. Baba anajifahamu na kujipenda: wazo analojifahamu ndiye Mwana, upendo anaojipenda katika wazo hilo ndiye Roho Mtakatifu. “Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami popote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu” (Yoh 17:24).
Nafsi tatu za Mungu zina Umoja hata katika utendaji, kila nafsi akiuchangia kulingana na sifa yake maalumu ndani ya Utatu. Baba Mwenyezi sifa yake ni Uwezo. Mwana kama Neno la Baba sifa yake ni Hekima. Roho kama Pumzi ya uhai ya Baba sifa yake ni Upendo. Katika Uwezo wake Baba anafanya yote kwa Hekima na Upendo, hasa katika utume wa Mwana aliyefanyika mtu na katika utume wa Roho kama paji. “Amin, amin, nawaambia: Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vilevile” (Yoh 5:19).
Fumbo hilo linaadhimishwa katika liturujia ya madhehebu mbalimbali ya Ukristo wa mashariki (siku ya Pentekoste) na ya Ukristo wa magharibi (Jumapili inayofuata).
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.