Tabakamwamba
From Wikipedia, the free encyclopedia
Tabakamwamba (kwa Kiingereza lithosphere)[1] ni sehemu thabiti ya nje ya sayari ya Dunia. Hiyo inamaanisha ganda la Dunia, pamoja na chini yake sehemu ya juu ya "koti la dunia". Tabakamwamba linakaa juu ya sehemu moto na laini ya ndani zaidi ya koti la Dunia.


Kwenye mpaka kati ya tabakamwamba na koti lenyewe liko tabaka kasiduni (ing. asthenosphere) ambayo ni nyumbufu kiasi.
Tabakamwamba linafanywa na miamba imara, tofauti na sehemu za ndani zaidi ya Dunia ambako mwamba na madini yote vinapatikana kwa hali nyumbufu au giligili kutokana na joto kali na shinikizo kubwa.
Eneo la tabakamwamba linagawiwa kwa vipande vikubwa ambavyo vinaelea juu ya sehemu moto za ndani. Vipande hivyo ni mabamba ya ganda la Dunia au kwa kifupi mabamba gandunia.
Aina za tabakamwamba
Kuna aina mbili za tabakamwamba:
- Tabakamwamba chini ya bahari; mabamba gandunia huachana katika vilindi vya bahari na hapo magma joto inapanda juu na kujenga hivyo miamba mipya ikipoa na kuganda. Hivyo ganda la Dunia chini ya bahari ina umri mdogo zaidi na unene mdogo wa kilomita 50-100.
- Tabakamwamba la bara. Hapa tunakuta miamba ya kale zaidi na unene wake ni km 100 hadi 200.
Mzunguko wa tabakamwamba
Sehemu kubwa za tabakamwamba ziko katika mwendo wa kutokea na kupotea tena. Kenye vilindi vya bahari ambako mabamba gandunia yanaachana, magma inapanda na kuunda miamba mipya. Mchakato endelevu unasukuma mabamba jirani mbali kutoka mistari hii. Kwa upande mwingine kuna sehemu ambako mabamba yanasukumana na hapa bamba moja husukumwa chini ya bamba jingine na kwa namna hiyo kuunda mifereji ya bahari. Kadiri miamba inavyozama chini na kuingia katika vilindi vyenye joto kubwa inayeyushwa tena na kujiunga na magma ya koti la Dunia.
Marejeo
Marejeo mengine
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.