Pangani (mto)
mto kasikazini ya Tanzania From Wikipedia, the free encyclopedia
Kwa matumizi mengine ya jina hili angalia hapa Pangani

Mto Pangani ni kati ya mito mikubwa ya Tanzania. Unabeba maji ya Milima ya Meru, Kilimanjaro, Pare na Usambara kwenda Bahari ya Hindi. Mdomo wake uko mjini Pangani.
Jina
Mto unapita katika maeneo ya jumuiya zenye lugha tofautitofauti, hivyo kuna majina mbalimbali.
Katika karne ya 19 kabla ya ukoloni mwendo hadi maporomoko karibu na Hale (Mnyuzi) ulijulikana zaidi kama "Ruvu", na sehemu ya mwisho kuanzia maporomoko hadi bahari kwa jina "Pangani" kutokana na mji ulipofikia baharini[1] .
Kwenye ramani za zamani za ukoloni majina yote mawili yalitumika kandokando: "Ruvu" na "Pangani". Ramani za zamani za uhuru wa Tanzania mara nyingi huwa na maandishi "Pangani or Ruvu River". [2].
Siku hizi imekuwa kawaida kutumia jina "Pangani" kuanzia bwawa la Nyumba ya Mungu.
Beseni la mto

Beseni la Pangani ni eneo la km2 43,650. Karibu yote imo Tanzania isipokuwa kuna km2 3,914 huko Kenya katika mazingira ya Taveta. Jumla ya wakazi katika beseni la Pangani ni milioni 3.7.
Chanzo cha mto Pangani ni maungano ya matawimto Kikuletwa na Ruvu inayokutana leo katika lambo la Nyumba ya Mungu kusini kwa Moshi. Mto Kikuletwa hupokea maji kutoka Mlima Meru na mitelemko ya Kilimanjaro upande wa kusini. Ruvu hupokea maji kutoka mitelemko ya Kilimanjaro upande wa mashariki pamoja na Ziwa la Jipe.
Mto Pangani unaendelea km 432 hadi Pangani mjini unapoingia katika Bahari Hindi. Kwenye sehemu ya kwanza baada ya Nyumba ya Mungu mto unaitwa wakati mwingine bado "Ruvu".
Uzalishaji wa umeme kwenye mto Pangani

Kuna mahali pawili ambako malambo yametengenezwa kutumia umememaji ya mto Pangani
- Nyumba ya Mungu pale ambako matawimto ya Ruvu na Kikuletwa yanakutana
- Maporomoko ya Pangani karibu na Hale (kata ya Mnyuzi, Korogwe)
Vituo vya umeme vimeathiriwa vibaya na kupungukiwa kwa maji mtoni.[3]
Hifadhi ya mazingira na kupungukiwa kwa maji
Mto Pangani unategemea misitu panapokusanywa maji yake. Misitu hii imepungua sana kutokana na uenezaji wa mashamba, kukatwa kwa miti kwa ajili ya makaa na matumizi ya ubao.
Vilevile machafuko yamekuwa hatari kwa ajili ya afya ya mto na watu wanaotegemea maji yake. Asili ya machafuko ni hasa kilimo, mvua hupeleka mbolea mtoni na kusababisha kukua kwa wingi wa majani yasiyotakika.
Tazama pia
Tanbihi
Viungo vya nje
Wikiwand - on
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.