From Wikipedia, the free encyclopedia
Madonda matakatifu (kwa Kilatini na Kiingereza Stigmata, wingi wa stigma, kutoka Kigiriki στίγμα) ni jina linalotumiwa na Wakristo kutaja majeraha au maumivu katika viungo vya mwili ambapo Yesu alipatwa na madonda 5 wakati wa kusulubiwa, yaani mikono, miguu na ubavu, lakini pia kichwa na sehemu nyingine alipotiwa taji la miiba au kupigwa mijeledi.
Mtume Paulo mwishoni mwa Barua kwa Wagalatia aliandika, "Mimi nachukua mwilini mwangu chapa (stigmata) za Yesu."[1] kama zile zinazotiwa juu ya mwili wa wanyama au watumwa ili kutambua ni mali ya nani. Inafikiriwa kwamba alikuwa anadokeza alama za mapigo aliyoyapata kwa ajili ya imani yake.
Watu waliopata alama za namna hiyo lakini bila mapigo ya kawaida walitokea hasa katika watawa wa Kanisa Katoliki kama vile Wadominiko na Wafransisko.[2]
Wa kwanza kujulikana ni shemasi Fransisko wa Asizi. Baada yake kesi hizo ziliongezeka, lakini madonda hayo yanapatikana tu ndani ya wale wanaotoka nje ya nafsi, yakitanguliwa na kuongozana na maumivu makali ya kimwili na ya Kiroho yanayowalinganisha na Yesu msulubiwa.Padri wa kwanza ni Pio wa Pietrelcina.
Je, udanganyifu unaweza kusababisha mwilini hayo madonda ya Bwana katika miguu, mikono, ubavu na paji la uso pamoja na maumivu makali yaliyokumbusha kwa namna ya pekee yale ya Yesu? Hayo yalitokea pasipo sababu ya nje na kutiririsha mara kwa mara damu isiyoharibika.
A. Sempé aliandika vizuri, “Kwa umbile lake madonda halisi, yale ya watakatifu ambayo peke yake yanazingatiwa na Kanisa, si madonda ya kawaida… maendeleo yake ni tofauti kimsingi na yale ya kawaida. Ili tukumbushe tu sifa zake zilizothibitishwa zaidi, tunaweza kusema madonda hayo yanakataa matibabu yoyote na vilevile hayapatwi na uozo wowote: hakuna tiba inayoweza kuyaponya, wala usaha unaopatikana ndani yake, ingawa mara nyingi yanakaa wazi miaka”; kumbe jeraha lolote la kawaida linasababisha usaha, hata katika hao wenye madonda matakatifu. “Pengine madonda yanakauka ghafla kikamilifu, kiasi kwamba ngozi ya kovu inavutika na kuwa imara kama ngozi ya jirani… ingawa inawezesha kutambua sura na ukubwa wa donda la chini yake. Hatimaye madonda halisi yanatonatona mara kwa mara kulingana na maadhimisho ya liturujia” au kwenye Ijumaa, pengine hata siku ambazo mhusika hakutarajia kwa kutojua mwaka huo adhimisho fulani linaangukia siku hiyo. “Je, sifa hizo si za ajabu? Hakuna kitu cha namna hiyo kinachotokea kamwe… kwa msaada wa udanganyifu katika wenye matatizo ya nafsi”.
Pengine mwenye madonda matakatifu akilala chali, damu yanatiririka kutoka madonda ya miguu upande iliotiririka kutoka yale ya Kristo, kwa hiyo kinyume cha elekeo la mvutano. Vilevile wingi wa damu inayotoka hauelezeki: ingawa kwa kawaida madonda matakatifu yako juujuu, mbali na mishipa mikubwa ya damu, yanabubujika kwa wingi.
Katika kueleza madonda hayo sifa hizo za pekee kisayansi zinatajwa pamoja na nafasi za Kiroho za tukio hilo la pekee, hasa huruma kubwa kwa mateso ya Mwokozi. Tuzingatie kuliko yote kwamba madonda matakatifu yanapatikana tu katika watu ambao wanatimiza maadili kishujaa na kupenda msalaba, wanapenya fumbo la ukombozi, mateso ya roho na ya mwili ya Kristo aliyejitoa sadaka kwa wakosefu. Ndilo jambo lisilo na uhusiano wowote na watu wenye ugonjwa wa nafsi: kwamba Msulubiwa anajichagulia watu awalinganishe naye, kwa namna inayoonekana au isiyoonekana, ili atukumbushe sisi tusiojali mateso yake makali. Kusahau jambo hilo ili kufafanua kimaumbile tu madonda hayo ni kutaka kuyazingatia mbali na sababu zake kuu. Ni kama kuzingatia kinyago upande wa ubao ambamo kimechongwa, bila kujali muundo wake wa sasa, lengo lake halisi na msanii aliyejiwekea lengo hilo.
Halafu, tukitaka kupima vema tendo lolote la kibinadamu, ni lazima tuzingatie kwa uangalifu nafasi zake mojamoja kadiri ya mfululizo maarufu ufuatao: Nani, nini, wapi, kwa misaada ipi, sababu gani, namna gani na lini? Vivyo hivyo, ili tupime vizuri maana na uzito wa tukio la pekee kama hili, ni lazima tuzingatie kwa uangalifu mambo yake yote upande wa mwili na wa roho, hasa: yale yanayohusu lengo (sababu gani) likionyeshwa ama mapema kwa sala au ahadi fulani, ama baadaye kwa upendo mkubwa kwa msalaba; yale yanayohusu kitu chenyewe (nini), k.mf. madonda ya mwili yanasababisha pamoja na mateso makali mwilini jeraha tamu rohoni linaloweza kutokana na Mungu tu; yale yanayomhusu mtu (nani), ambaye ni mnyenyekevu, mtiifu na ana upendo mkubwa; yale yanayohusu njia (kwa misaada ipi), ambapo hapana ujanja wala ushirikina; hatimaye yale yanayohusu wakati na mahali (wapi na lini). Mambo hayo yote yakilingana, tunafikia hakika fulani kuhusu asili ya Kimungu ya madonda hayo, kwamba hakuna ugonjwa unaofanya watu hao wafanane na Yesu msulubiwa.
Je, madonda hayo mwilini yanaweza kusababishwa kimaumbile na huruma kubwa ipitayo maumbile kwa mateso ya Bwana ikizidiwa na hali ya kutoka nje ya nafsi? “Upendo ni wa ajabu katika kukuza ubunifu hata ujitokeze kwa nje… Lakini kwa kweli upendo uliokuwemo ndani (ya Mt. Fransisko wa Asizi) haukuweza kutoboa mwili kwa nje. Ndiyo sababu serafi wa moto akija kusaidia alirusha miali miangavu yenye kupenya hivi hata ikasababisha kweli mwilini madonda ya nje ya Msulubiwa ambayo upendo ulikwishachapa ndani ya roho” (Fransisko wa Sales).
Wengi walikuwa na huruma kubwa ipitayo maumbile kwa mateso ya Mwokozi wasipate madonda hayo. Tunaweza kutaja watakatifu waliowahi kuzama katika mafumbo, kutoka nje ya nafsi zao na hata kuwa na jeraha la Kiroho moyoni pasipo madonda mwilini. Kati ya walioyapokea, walio wengi hawakuyatarajia wala kuyataka: Yesu mwenyewe anawapatia wale anaotaka, anapotaka na anavyotaka. Ni neema ya pekee ambayo haipo katika njia ya kawaida ya utakatifu.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.