From Wikipedia, the free encyclopedia
Hassan Rehani Bitchuka ni mwanamuziki wa Tanzania aliyedumu katika fani ya sanaa ya muziki wa dansi kwa miongo mitano na kujipatia umaarufu kupitia kazi zake.
Mwanamuziki huyu anasifiwa kwa sauti yake nzuri. Mashabiki humwita 'Super stereo.' Kwa kauli yake husema kuwa sauti yake ni ya asili na hafanyi chochote kuifanya iwe ilivyo. Pia Bitchuka ni mtunzi na gwiji wa uimbaji[1].
Akihojiwa na mwandishi wa Starehe wa kampuni ya Mwananchi Communications, Bitchuka alisema; "muziki uko damuni mwangu. Nimeurithi kutoka kwa baba na mama yangu. Baba alikuwa akipiga ngoma na mama akicheza ngoma za Warua wa Kigoma"[1].
Bitchuka alizaliwa Kigoma-Ujiji, eneo la Buzebazeba, kati ya mwaka 1955 na 1956. Kipaji chake cha sauti na uimbaji kilijitokeza na kufahamika kwa mara ya kwanza akiwa mdogo akisoma madrasa za akina Shaikh Ali Muhsin na Shaikh Halfani, kwao Kigoma. Mwandishi aliyemhoji anaitaja sauti ya Bitchuka kuwa ya "tajwiid". Kwa kabila yeye ni Mmanyema.
Kuacha kwake shule kulianzia kipindi akisoma madrasa. Alikutana na ushawishi wa rafiki yake aliyekuwa akiitwa Omari (p.k.a)*. Omari alikuwa anajua kupiga gita naye alijifundisha. Hata hivyo upepo ulibadilika: yeye na Omari walitoroka Kigoma na kwenda Ngarenaro, Arusha, kucheza mpira. Hiyo ilikuwa mwishoni mwa 1972. Huko Arusha wakaajiriwa na Tanzania Breweries Limited wakiwa ni wachezaji wa timu ya kampuni (akicheza namba 2 na 3).
Mwanzoni mwa 1973 bendi ya NUTA ilizuru Arusha. Bitchuka na rafiki yake wakaenda dansini. Huko, Bitchuka akamuona Saidi Mabera ambaye alikuwa akimfahamu tangia kwao [Kigoma]]. Bitchuka akapata tashwishwi ya kuwa [mwanamuziki]]. Akamdokeza Mabera ambaye alifikisha ombi lake kwa wanamuziki wa bendi. Awali hawakuonesha kumhitaji wakimuona ni mdogo. Hata hivyo Mabera aliwathibitishia kuwa ataweza. Siku moja wazee (wanamuziki) wa NUTA wakamsikia Bitchuka akiimbia Arusha Jazz kwenye ukumbi. Wote wakashangaa jinsi alivyokuwa mahiri na kusema, " kumbe huyu mtoto ni hatari sana!". Wakamwahidi kumchukua na alipokuja kujiunga nao, safari yake ya kimuziki haikusimama kamwe.
Bitchuka akafanya kazi na NUTA Jazz, bendi iliyomilikiwa na muungano wa vyama vya wafanyakazi kuanzia mwaka 1973; akitunga, akiimba na kurekodi nao nyimbo nyingi. Mwaka 1977 NUTA Jazz ikawa JUWATA Jazz Band kufuatia kubadilika kwa muundo wa NUTA. Aliendelea kumfanyia kazi mwajiri wake hadi miaka takriban miwili baada ya kuanzishwa Mlimani Park, bendi ambayo alihamia. Alifanya kazi na Mlimani Park hadi mwaka 1985 alipohamia OSS. Kwa ufupi, Bitchuka alizifanyia kazi bendi zifuatazo: Arusha Jazz, Nuta Jazz, Juwata Jazz, DDC Mlimani Park, OSS, OTTU Jazz, TFTU Jazz na Msondo Ngoma Music Band. Hata hivyo mzunguko wake ni zaidi ya utajaji huo kwani kulikuwa na 'nenda - rudi' pia.
Si rahisi kuipitia historia ya Bitchuka bila kumzungumzia Muhidin Maalim Gurumo. Wanamuziki hawa wamefanya kazi pamoja kwa zaidi ya miaka 30, wakihama kutoka bendi moja kwenda nyingine kwa pamoja (mpaka miaka ya mwishoni ya 90 au ya mwanzoni ya 2000 ambapo mashabiki walishuhudia kwa mara ya kwanza na kwa mshangao, Bitchuka na Gurumo wakiimbia bendi tofauti).
Kilichonogesha zaidi kwa wanamuziki hawa, ni ule upacha wao wa sauti. Waliimba nyimbo nyingi pamoja na kila wimbo ukawa mtamu masikioni[2]. Mifano ya nyimbo walizoimba pamoja ni Halima, Kilimo cha kufa na kupona (za NUTA), Nidhamu ya Kazi, Mwana Acha Wizi (za JUWATA), Penzi la Fukara, Nalala kwa Tabu (za DDC M.P), Shukrani kwa Mama, Chatu Mkali (za OSS), na nyinginezo.
Bitchuka alipata umaarufu na kupendwa na halaiki ya wapenzi wa muziki wa dansi katika nchi mbalimbali za Afrika ya Mashariki na Kati. Katika miaka hasa ya 80, redio za mataifa ya nje, licha ya za napa nchini, zilizicheza sana nyimbo za DDC Mlimani Park na Juwata Jazz zilizoimbwa na Bitchuka.
Mfano wa vituo hivyo vya redio ni KBC cha Nairobi, Kenya. Hapa nchini, tungo na nyimbo mbalimbali zilizoimbwa na Bitchuka zilikuwa zikishika chati sana kwenye vipindi kama Ombi Lako, Vipindi vya Salamu, nk., pamoja na chati za muziki kama Misakato na Club Raha Leo Show vya RTD na vipindi vilivyohusisha muziki wa dansi vya Sauti ya Zanzibar na redio za Burundi na Uganda.
Bendi alizowika nazo zimekuwa na mitindo ya upigaji muziki na kuucheza iliyokonga nyoyo za wapenzi. Mitindo aliyotamba nayo sana ni Msondo wa NUTA na JUWATA (uliasisiwa na Gurumo), Sikinde Ngoma ya Ukae wa DDC Mlimani Park (uliasisiwa na Gurumo) na Ndekule wa Orchestra Safari Sound (uliasisiwa na Gurumo).
Wimbo ulioweka historia zaidi ni Duniani Kuna Mambo ambao ulivuma sana kwenye mitandao ya kijamii mwaka 2023 kufuatia kuonekana kwa rais mstaafu wa JMT wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete, akiuimba wimbo huo mbele ya Bitchuka mwenyewe.
Sifa za wimbo huo ni pamoja na kuwa katika mahadhi ya ' reggae ' kwenye sehemu yake ya kwanza kabla ya kubadilika na kuwa katika mahadhi ya rumba la kisasa. Pia Bitchuka ameuanzisha wimbo huo katika sauti iliyo kwenye ufunguo upatikanao juu 'sana' kwenye ngazi za sauti. Jambo hilo lilikuwa la kipekee kabisa (Alipata kuulizwa sababu ya kufanya hivyo, jibu lake likawa: alikuwa anatuma ujumbe Kwa waimbaji wengine kuwa kama kuna awezaye kupafikia hapo, na ajitokeze. Miongo minne imepita hajajibiwa)
Pamoja na umaarufu alioupata, linapokuja suala la mafanikio kimaisha, Bitchuka hajioni kama amefaidika vya kutosha na kazi zake. Mfumo wa zamani usiokidhi wa kuwalipa wanamuziki pamoja na wizi wa kazi za muziki amevitaja kuwa vilikuwa vikwazo.
Baadhi ya nyimbo alizoimba, nyingi katika hizo ametunga mwenyewe ni kama; (NUTA) Halima, Kilimo cha kufa na kupona, (JUWATA) Nidhamu ya kazi, Mwana acha wizi, Mpenzi Zarina (aliomtungia mkewe), Sogea karibu, Uzuri si shani, Selemani, Mariamu ninakujibu, (Mlimani Park) Tufanye kazi kwa nidhamu, Duniani kuna mambo, Tucheze Sikinde, Tende Halua, Penzi la fukara, Kupenda sio ndoto, Aija, Hiba, Hasira, Talaka ya hasira, Nawashukuru wazazi, Penzi la mwisho, Fikirini nisamehe, Asiyesikia la wazazi, Shemeji Issa, Mume wangu Jerry, Mv. Mapenzi I, Uhuru wa Zimbabwe, na nyingine nyingi.
Hassan Rehani Bitchuka alifanya kazi na wanamuziki wengine wengi katika bendi mbalimbali. Kwa uchache, wanamuziki hao ni kama; Said Mabera (daktari), 'King' Michael Enock (alijulikana pia kama ' Teacher ')[3], Abel Baltazari, Juma Hassan 'Town', Ahmed Omari, Muhidin Maalim Gurumo, Abdallah Gama, Hamisi Juma, Joseph Mulenga, Joseph Lusungu, Joseph Maina, Joseph/Yusufu Bernard, Suleiman Mwanyiro, Haruna Luwali, Habibu Mgalusi 'Jeff', Ali Jamwaka, George Kessy, Shaaban Dede, Beno Villa Anthony, Max Bushoke, Cosmas Chidumule, Henry Mkanyia, Muharami Said, Ali Makunguru, Charles John Ngosha, Kassim Mponda, Kassim Rashidi, Boniface Kachale, Ibrahim Mwinchande, Moshi William, Abdul Ridhiwani, Mustafa Pishuu, na wengine wengi.
Tarehe 12 Februari 2023 tovuti ya standard media ya Kenya iliandika mtandaoni katika kichwa cha habari: (tafsiri) ' mwimbaji wa DDC Mlimani Park aweka kipaza sauti chini[4]. ' Makala ilitanabaisha kuwa, Hassan Rehani Bitchuka, 77, mwimbaji wa siku nyingi wa DCC Mlimani Park Orchestra, mtunzi na mwimbaji kiongozi, atamatisha safari yake ya kimuziki kufuatia upasuaji wa jicho lake moja ambao ulimsababishia uoni hafifu.
Tarehe 2 May 2023 tovuti ya Global Publishers iliandika mtandaoni katika kichwa cha habari, Mke wa Bitchuka Amwaga Machozi. Mumewe Hali Mbaya[5]. Ujumbe mkuu ulikuwa kuwalilia viongozi watoe msaada kwani kulikuwa na hatari ya kupoteza jicho la pili. Ulikuwa ni ukweli halisi kwani kama jinsi mwenyewe alivyoweka wazi, kazi za thamani alizofanya miaka yote, hazikumpatia kipato cha kumkimu uzeeni au kuonesha maendeleo ya maana.
Taarifa hizo, ni mifano ya taarifa mbalimbali zilizojiri mtandaoni hasa katika 2022 na 2023. Zilikuwa ni taarifa zilizowajuza umma kuwa kutokana na changamoto za maradhi na umri, Bitchuka alikuwa anaweka 'mike' chini.
Namna bora ya kumalizia makala inayomhusu Bitchuka ni kukiri kuwa kuna waandishi waliofanya kazi nzuri ya kuzitafuta habari za mwanamuziki huyo. Mabwana Masoud Masoud, Adam Zuberi, Rajab Zomboko, Wambura Mtani, Jacob Usungu, Muhidin Issa Michuzi, pamoja na matoleo kadha wa kadha ya magazeti, wanastahili pongezi na shukrani.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.