From Wikipedia, the free encyclopedia
Antara (kwa Kiingereza na Kilatini Antares; pia α Alpha Scorpii, kifupi Alpha Sco, α Sco) ni nyota angavu zaidi katika kundinyota la Nge (pia: Akarabu) (Scorpius). Ni pia nyota angavu ya 15 kwenye anga la usiku. Mwangaza unaoonekana unacheza kati ya mag 0.75 na 0.95.
Antara ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [1]. Walipokea jina hili kutoka kwa Waarabu waliosema عنترة antarah, ingawa leo wanatumia zaidi قلب العقرب qalb al-aqrab (moyo wa akarabu - nge). Hii „Antara“ ilikuwa namna ya kutamka jina la Ἄντάρης an-ta-res walilokuta kwa Klaudio Ptolemaio katika kitabu cha Almagesti[2]. Lakini Waarabu walichukua maana yake kwa kumtaja Antara ibn Shaddad (ar. عنترة بن شداد ) aliyejulikana kwao kama mshairi na shujaa wa Uarabuni wa Kale kabla ya Uislamu. Ἄντάρης - Antares iliyotumiwa na Ptolemaio inamaanisha "sawa na Ares", ilhali "Ares" ni jina la Kigiriki kwa mungu wa vita (kama Kiroma Mars) na pia jina la sayari ya nne katika mfumo wa Jua yaani Mirihi. Sawa na Mirihi pia Antara inaonekana kuwa na rangi nyekundu kwa macho matupu; mwangaza unafanana pia hivyo si vigumu kuchanganya nyota na sayari hii..
Kwa matumizi ya kimataifa Umoja wa Kimataifa wa Astronomia ulifuata mapokeo ya Kigiriki na kuorodhesha nyota hii kwa jina la "Antares" [3].
Alfa Scorpii (au α Scorpii) ni jina la Bayer kufuatana na utaratibu ulioanzishwa na Mjerumani Johann Bayer katika karne ya 17. Inamaanisha ni nyota angavu zaidi (hivyo inatajwa kwa herufi ya kwanza kwenye alafabeti ya Kigiriki) katika kundinyota la "Scorpius" (kwa Kiswahili Akarabu au Nge).
Antara - Antares ni nyota badilifu na mwangaza unaoonekana wake unabadilika kati ya Vmag +0.6 na +1.6. Mwangaza halisi ni -5.3. Hivyo no nyota angavu ya 15 kwenye anga ya usiku.
Antara iko katika umbali na Dunia wa miaka nuru 550 – 600. Masi yake ni takriban M☉ 15 na nusukipenyo chake R☉ 680 (vizio vya kulinganisha na Jua letu). [4][5]).
Ni nyota jitu kuu jekundu katika kundi la spektra M1.5 Iab-b. Inaitwa jitu kuu kwa sababu masi yake ni kubwa vile, mara 15 ya Jua. Ikiwa nyota jitu kuu jekundu ni nyota iliyopanuka baada ya kuishiwa hidrojeni katika kitovu chake; katika hali hii kitovu cha nyota kinajikaza na myeyungano wa hidrojeni unahamia kwenye tabaka za nje za nyota. Hii inasababisha kupanuka kwa nyota na kuongezeka kwa mwangaza wake. Kama Antara ingechukua nafasi ya Jua letu, sayari za Utaridi, Zuhura, Dunia na Mirihi zingemezwa nayo maana kipenyo chake kinazidi obiti ya Mirihi.
Antara ina nyota msindikizaji kwa hiyo iki katika mfumo wa nyota maradufu. Nyota hii ya pili huitwa α Scorpii B. Ni ndogo kuliko α Scorpii A yaani Antara ikiwa na masi ya M☉ 7 na nusukipenyo cha R☉ 5[6] . Ni nyota ya safu kuu ikiwa katika kundi la spektra B2. Kutokana na mwangaza mkubwa wa Antara yenyewe si rahisi kuiona iligunduliwa wakati Mwezi ulipita mbele ya nyota kuu na kuifunika.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.