From Wikipedia, the free encyclopedia
Mumia (kutoka Kiarabu مومياء mumia; pia: mumiani; kwa Kiingereza: mummy) ni maiti wa binadamu au mzoga wa mnyama iliyokauka bila kuoza. Hali hiyo inaweza kutokea kiasili katika mazingira maalumu au kwa kutumia mbinu fulani. Mchakato wa kuoza huzuiwa na baridi kali, katika mazingira yabisi (pasipo na unyevu hewani) na mwendo wa hewa, kwa kukosa oksijeni au kwa kutumia kemikali fulani.
Jina la mumia lilitumiwa mwanzoni kwa kimiminika cha lami likawa jina la maiti aliyekaushwa kwa kutumia lami yaliyopatikana hasa Misri ya Kale likaendelea kutumiwa kwa maiti wote waliokauka bila kuoza.[1]
Neno la Kiswahili linatokana na Kiarabu مومياء mumia. Kiasili neno hili lilitaja lami ya kumiminika [2] iliyotumiwa kama dawa na pia kwa kuzuia kuoza kwa maiti waliotakiwa kuhifadhiwa kulingana na imani mbalimbali katika dunia ya kale.
Ilhali "mumia" ilikuwa kiasili miminika ya lami pekee, neno hili lilitumiwa baadaye pia kwa maiti waliokaushwa na kupatikana katika makaburi ya Misri ya Kale. Desturi ya kukausha na kutunza maiti kwa kutumia dawa mbalimbali ilikwisha baada ya mwisho wa dini ya Misri ya Kale kutokana na uenezaji wa Ukristo na baadaye Uislamu nchini. Lakini katika tabianchi yabisi ya Misri maiti wa zamani walikaa wakapatikana kwa wingi. Walionekana nyeusinyeusi hivyo watu waliona walitibiwa na "mumia" na kile cheusi kutoka makaburi kilitumiwa pia kama dawa.
Baadaye matabibu wa Misri waliona kwamba ilifaa pia kutumia vipande vya maiti hao kama dawa.[3].
Baadaye tena wataalamu wa Ulaya, waliojifunza mengi kutoka tiba ya Waislamu, walipokea maelezo hayo wakaanza kununua maiti waliokaushwa kutoka Misri. Ilhali matumizi ya maiti kama dawa yalipungua katika nchi za Waislamu kuanzia karne ya 16 yaliendelea katika nchi za Ulaya hadi karne ya 19[4].
Utamaduni wa Misri ya Kale unajulikana kwa dini yake iliyofundisha ni muhimu kutunza mwili ili mtu aweze kuzaliwa upya akiingia peponi baadaye. Wamisri walitumia mbinu mbalimbali kwa kutunza miili ya marehemu. Utumbo na ubongo vilitolewa na kutunzwa katika vyombo vya pekee baada ya kuvikausha katika chumvi. Mwili uliofunguliwa ulipakwa chumvi kwanza, baadaye na mchanganyiko wa nta, utomvu wa miti wenye harufu nzuri na lami. Baadaye mwili uliviringishiwa bendeji za kitambaa kilicholoweshwa kwa dawa mbalimbali, pamoja na lami. Shughuli hizo zote zilitekelezwa na mafundi maalumu waliosimamiwa na makuhani. Wamisri ambao familia zao hazikuwa na uwezo wa kugharamia shughuli hizo zote waliandaliwa kwa mbinu sahili zaidi. Maskini walizikwa kwenye mchanga wa jangwa ambako mara nyingi maiti wao pia walikauka kabisa.
Wamisri walihifadhi pia miili ya wanyama hasa wanyama waliotazamwa kuwa ishara ya miungu yao na kufugwa mahekaluni. Kwa jumla ni zaidi ya mumia milioni moja ya wanyama, hasa paka, zinazojulikana[5].
Wamisri wa kale hawakuwa peke yao kuwa na utamaduni wa kujitahidi kutunza miili ya marehemu. Hasa katika mazingira ambako tabianchi ni yabisi sana kuna mifano ya miili inayohifadhiwa vema bila kuoza. Hasa Amerika Kusini kabla ya kufika kwa Wahispania, watu kama Wainka walijua mbinu za kutunza miili ya marehemu [6]
Mumia asilia hutokea
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.