Maana ya maisha
From Wikipedia, the free encyclopedia
Maana ya maisha ni mojawapo kati ya masuala makuu kuhusu thamani, madhumuni na umuhimu wa binadamu kuwepo duniani na wa maisha kwa jumla. Suala hilo linaweza kujitokeza katika maswali mengi tofauti yanayohusiana, kama vile Mbona tumekuwepo?, Maisha yanahusu nini? na Ni nini maana ya haya yote?
![Thumb image](http://upload.wikimedia.org/wikipedia/commons/thumb/f/fc/Woher_kommen_wir_Wer_sind_wir_Wohin_gehen_wir.jpg/640px-Woher_kommen_wir_Wer_sind_wir_Wohin_gehen_wir.jpg)
Mmojawapo kati ya michoro maarufu ya msanii Paul Gauguin wa kipindi cha baada ya uimpreshonisti.
Binadamu anajiuliza maswali kama hayo hasa anapokabiliana na kifo, kwa mfano msiba wa ndugu au rafiki.
Limekuwa suala kuu la udadisi wa sayansi, falsafa na teolojia tangu zamani. Kumekuwa na idadi kubwa ya majibu kwa maswali hayo kutoka asili mbalimbali kiitikadi na kiutamaduni.
Maana ya maisha imechanganyikana kwa undani na dhana za falsafa na imani za dini na hugusia masuala mengine mengi, kama vile ontolojia, tunu, kusudi, maadili, hiari, uwepo wa Mungu, roho, na kinachoendelea baada ya maisha haya kwisha.
Michango ya sayansi kawaida ni ya moja kwa moja na inaeleza uhalisia kutokana na mambo yanayopimika kuhusu ulimwengu; sayansi inatoa muktadha na mipaka kwa mazungumzo kuhusu mada zinazohusika.
Mbadala ni mtazamo wa kifalsafa unaokabili swali: "Ni nini maana ya maisha 'yangu'?" Thamani ya swali linalohusu kusudi la maisha huweza kuwiana na kuupata ukweli wa mwisho, au hisia za umoja na utakatifu.