From Wikipedia, the free encyclopedia
Abrahamu wa Aleksandria (Ebn-Zaraa, Syria - 3 Desemba 978) kuanzia mwaka 975 hadi kifo chake alikuwa Patriarki wa Aleksandria (Misri) na Papa wa 62 wa Kanisa la Wakopti ambalo linamheshimu kama mtakatifu.
Mzaliwa wa Syria[1], alikuwa mfanyabiashara tajiri aliyetembelea Misri mara nyingi.
Hatimaye alihamia Aleksandria, alipofahamika kwa moyo wa ibada na ukarime kwa mafukara.
Kisha kupata daraja takatifu, nusu ya mali yake aliwagawia maskini na nusu aliitumia kujengea visima huko na huko nchini.
Baada ya kiti cha Mt. Marko kukosa Patriarki miaka miwili, ghafla mkutano kwa kauli moja ulimchagua Abrahamu, na ingawa huyo alikuwa akisita, aliwekwa wakfu huko Aleksandria.[2]
Mara moja Abrahamu alipambana na tabia ya usimoni na mitara kati ya wakleri akiwatishia kuwatenga na Kanisa.[2]
Chini ya khalifa Al-Muizz serikali ya Kiislamu ilibadilibadili sera zake kuhusu Wakopti. Inasemekana kwamba Al-Muizz alipenda midahalo ya dini. Kwa shauri la waziri Yaqub ibn Killis, Myahudi aliyesilimu, aliitisha mdahalo kati ya Abrahamu na Moses, Myahudi maarufu. Abraham alikwenda na Severus Ibn al-Muqaffa.
Ibn Killis alimuarifu Al-Muizz kwamba Injili (Math 17:20; Mk 11:23) inasema, "Mkiwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mtaweza kuuambia mlima, Sogea toka huko hadi huko, nao utasogea". Hapo akamhimiza khalifa amuagize Abrahamu asogeze Mlima Mokattam, mashariki kwa Kairo kama ana imani hiyo.[1] Hapo Al-Muizz alidai iwe hivyo, la sivyo atawangamiza Wakopti kwa upanga.
Abrahamu aliomba siku tatu akaagiza maaskofu na mapadri wafunge na kusali wakati yeye anafanya vile kwenye kanisa maarufu la Bikira Maria (kwa Karabu Al Mu'allaqah, kwa Kiingereza "Hanging Church"). Alfajiri ya siku ya tatu, baada ya kuzimia kwa uchovu, alipata njozi ambamo Bikira Maria alimfariji na kumuelekeza kwa mtu chongo mwenye kubeba maji sokoni: ndiye atakayehamisha mlima.
Alipokwenda, alimkuta Simoni Mshonangozi akisomba maji kwa ajili ya maskini na wazee kabla hajaenda kazini. Ingawa kwanza Simoni alisita, alipoambiwa kuhusu njozi alikubali kutoa maelekezo.[1]
Basi, walikusanya umati wa Wakristo na pamoja na khalifa, waziri wake na Waislamu waliokwishachochewa naye dhidi yao walielekea mlimani. Abrahamu aliadhimisha liturujia ya Kimungu. Walipoimba mara tatu "Bwana utuhurumie" huku wakipiga magoti, yeye alifanya ishara ya msalaba kwa upana wote wa mlima. Mara tatu huo ulitikisika kama kwa tetemeko la ardhi ukaanza kusogea juu pamoja na waumini na kurudi chini kwa kishindo kikubwa walipopiga magoti tena. Katikati miali ya jua ilipita na kuwezesha wote kuona ajabu hilo. Wakati huo Simoni alitoweka, na Al Muizz alisema kwa nguvu, "Allahu Akbar!"
Kwa hofu, alimuomba Abrahamu ampe zawadi gani, naye akasema ruhusa ya kukarabati makanisa kadhaa. Pia aliagiza siku hizo tatu za kufunga na kusali ziendelezwe kila mwaka. Hivyo Wakopti wanafunga siku arubaini na tatu kabla ya Krismasi.
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.