Remove ads
From Wikipedia, the free encyclopedia
Kimbunga (kwa Kiingereza: tropical cyclone, hurricane, typhoon) ni dhoruba kali inayoanza juu ya bahari katika maeneo ya tropiki yenye upepo wenye kasi ya zaidi ya km/saa 117. Kimbunga ni dhoruba aina ya tufani yaani kina mwendo wa kuzunguka.
Vimbunga huwa na eneo la shinikizo duni kwenye kitovu chake (low-pressure center). Upepo mkali unazunguka haraka kitovu hiki karibu na uso wa bahari au uso wa nchi (closed low-level atmospheric circulation, strong winds). Mvua za radi zinazunguka kitovu pamoja na mwendo wa kimbunga chote na kuleta mvua nzito (spiral arrangement of thunderstorms that produce heavy rain)[1].
Huanza juu ya bahari ya kitropiki kwenye maji yenye halijoto juu ya 26°C. Hewa joto yenye mvuke nyingi inaanza kupanda juu na kuzunguka. Mzunguko huo unaongezeka kasi kuwa dhoruba. Kasi ikifikia mwendo wa 117 km/saa inaitwa kimbunga.
Vimbunga vinatokea katika bahari zote zenye maji ya moto kaskazini na kusini kwa ikweta. Mzunguko hufuata mwendo wa saa kama kimbunga kinatokea kusini kwa ikweta; ni kinyume cha mwendo wa saa kama kinatokea kaskazini kwa ikweta.
Kimbunga kinaweza kusababisha hasara kubwa kikikubana na meli baharini na zaidi mwambaoni kinapofikia nchi kavu au visiwa. Nguvu ya upepo husukuma maji mengi ya bahari inayoweza kufikia mita kadhaa juu ya uwiano wa kawaida wakati wa kufika mwambaoni. Wimbi kubwa linaleta mafuriko wa ghafla yanayoweza kuvunja nyumba na kupeleka maji ya bahari mita mia kadhaa barani; penye mdomo wa mto wimbi la bahari linaendelea kuenea kwa kufuata njia ya mto.
Hatari zinazofuata ni hasa kasi ya upepo pamoja na kiasi kikubwa cha mvua.[2][3] Kasi ya upepo inaweza kuinua vitu vizito kama miti, mapaa ya nyumba[4] au magari na kuvirusha mbali. Watu huuawa na mali kuharibiwa. Wingi wa mvua husababisha mafuriko yanayofuata njia ya kimbunga juu ya nchi kavu, wakati mwingine kwa kilomita mia kadhaa kutoka mwambao[5].
Huko Amerika ni hasa visiwa vya Karibi na nchi jirani za Ghuba ya Meksiko pamoja na kusini mwa Marekani zinazoathiriwa kila mwaka.
Barani Afrika ndiyo Msumbiji pamoja na nchi jirani iliyoona mara kwa mara uharibifu kutokana na dhoruba. Mwaka 2019 kimbunga kilichoitwa Idai[6] kiliharibu mji mkubwa wa Beira na kusababisha vifo hadi Zimbabwe na Malawi[7]. Kimbunga hiki kilifuatwa na kimbunga kilichoitwa "Kenneth" kilichosababisha maafa kwenye visiwa vya Komori na kufika barani kaskazini mwa Msumbiji karibu na mji wa Pemba na kuathiri pia maeneo ya kusini mwa Tanzania[8].
Kila sehemu ya dunia kimbunga kina jina lake na majina haya yameanza kutumiwa kimataifa:
Vimbunga hutokea mara kwa mara katika majira ya joto. Wataalamu wameanza kuvipa majina kwa kurahisisha maelewano. Katika eneo la kila bahari kuna utaratibu wa pekee wa kutolea majina kwa vimbunga kufuatana na mapatano ya wanasayansi.
Atlantiki inaona takriban vimbunga kumi au zaidi kila mwaka. Hupewa majina kufuatana na alfabeti. Imekuwa kawaida tangu mwaka 1979 kutumia majina ya kiume na ya kike kwa kupokezana (zamani vilipewa majina ya kike tu, lakini wanawake walilalamika).
Wataalamu wanatumia orodha sita ya majina hivyo jina linaweza kurudia baada ya miaka sita.
Kimbunga ya "Katrina" kilichoharibu mji wa New Orleans nchini Marekani katika Agosti 2005 kilikuwa kimbunga cha 11 cha mwaka 2005. Kilifuata kimbunga "Jose" na kufuatwa na "Lee" halafu "Maria". Kama kimbunga kinasababisha uharibifu mkubwa sana jina lake huondolewa katika orodha maana yake jina hili halitarudia. "Katrina" imebadilishwa kuwa "Katia" katika orodha ya mwaka itakayotumika mwaka 2011 (ikitokea itakuwa kimbunga kinachofuata "Jose" ya 2011).
Seamless Wikipedia browsing. On steroids.
Every time you click a link to Wikipedia, Wiktionary or Wikiquote in your browser's search results, it will show the modern Wikiwand interface.
Wikiwand extension is a five stars, simple, with minimum permission required to keep your browsing private, safe and transparent.